2017-02-13 07:24:00

Maisha ya binadamu ni matakatifu hayawezi kugeuzwa kuwa ni kichokoo!


Maisha ya binadamu ni matakatifu na kamwe hayawezi kuwa ni bidhaa inayoweza kuuzwa na kununuliwa sokoni au kichokoo cha kuchezewa na wajanja wachache katika jamii. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kikamilifu katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na kupiga rufuku utalii wa upandikizaji wa viungo vya binadamu, kwani madhara yake ni makubwa sana kwa utu na heshima ya binadamu. Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye Makao yake Makuu mjini Geneva, Uswiss, wakati akichangia hoja kwenye mkutano wa 140 wa Baraza kuu la Shirika la Afya Duniani lililokuwa linajadili kuhusu kanuni msingi za uchangiaji wa damu, uratibu wa damu na sehemu yake pamoja na viungotiba kutoka kwa mwanadamu.

Kutokana na kucharuka kwa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, hali ambayo imeibua pia utalii wa upandikizaji wa viungo vya binadamu,anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na Serikali husika kuwajibika barabara ili kulinda na kudumisha viwango vitakavyosaidia kuweka uwiano mzuri kwa watu wanaojitolea damu ili kuokoa maisha ya watu na wagonjwa wanaopokea damu pamoja na viungo tiba kutoka kwa Wasamaria wema. Hapa kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na viwango vitakavyosaidia kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu; afya, ulinzi na usalama kwa wagonjwa wanaohitaji kupewa msaada wa viungo tiba.

Haya ni mambo msingi yaliyojadiliwa pia hivi karibuni mjini Vatican kuanzia tarehe 7 – 8 Februari 2017 kuhusu utumwa mamboleo na madhara yake na hatimaye, wajumbe wakachapisha tamko linalopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa ili kulinda utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Hili ni janga kubwa linalohitaji Jumuiya ya Kimataifa kulivalia njuga ili kuhakikisha kwamba, biashara ya binadamu, viungo vyake na utalii wa kupandikiza viungo vya binadamu unakomeshwa katika uso wa dunia.

Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuwa mstari wa mbele kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati na kuanza kutekeleza kwa vitendo mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, kwa ni huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Upendo na mshikamano vioneshwe kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kugharimia viungo tiba pamoja na kusimama kidete kuwadhibiti watu wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake.

Kimsingi waathirika wakubwa wa biashara hii ni maskini na wale watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wengi wao ni wakimbizi na wahamiaji wanaojikuta wakitumbukizwa kwenye magenge ya uhalifu wa kutupwa! Ili kupambana na vitendo hivi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu anasema Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye Makao yake Makuu mjini Geneva, Uswiss kwamba, kuna haja ya kuzingatia sheria, kanuni, viwango vya tiba ya mwanadamu, kwa kujikita katika usawa katika mchakato wa kutoa na kupokea damu pamoja na viungotiba kutoka kwa mwanadamu. Lengo ni kusimama kidete kulinda, kudumisha na kuenzi utu na heshima ya binadamu; kwa kuwalinda na kuwatetea watu ambao wako kwenye hatari kubwa ya kutumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na utalii wa upandikizaji wa viungotiba. Hapa kuna umuhimu wa kukazia kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, upendo katika ukweli, ili maisha ya mtu yaweze kuwa ni zawadi safi isiyokuwa na mawaa, inayomwezesha mtu kufikia utimilifu wake kwa kujisadaka kwa ajili ya upendo kwa jirani zake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.