2017-02-13 09:13:00

Leo ni kimbembe cha Sheria!


Torati na Manabii ni mihimili miwili ya maisha ya Wayahudi. Katika Torati na manabii Mungu aliwaahidia watu wake baraka ya kuwa taifa kubwa kupita yote, na ya kutawala ulimwengu mzima. Mathalani nabii Natan alimtabiria Daudi ufalme usio na mwisho. Kadhalika zaburi zilisema: “Wafalme wa Sheba na Saba, na wafalme wa visiwani, watatoa zawadi, na kulipa kodi kwa taifa la Waisraeli.” Kitabu cha Talmud kinatabiri kuwa kila mwisraeli atakuwa na watumishi elfu mbili na mia nne themanini. Hii ndiyo fikra ya Wayahudi iliyokuwa wakati wa Yesu juu ya katiba hii ya Agano la kale, yaani Torati na manabii. Kwa hiyo hakuna Myahudi aliyeweza kuthubutu kutangua isipokuwa Mungu peke yake. Kwa vile Yesu alikuwa Myahudi, naye hakutegemewa kabisa kuibatilisha.

Kadhalika Wayahudi walimngojea Masiha atakayetawala kwa mabavu kama simba. Ndivyo pia Yakobo alivyowabariki watoto wake, akionesha kwamba kutaibuka simba wa Yuda atakayewasambaratisha maadui na kutawala kwa nguvu. Kinyume chake Yohane Mbatizaji anamtambulisha Mwanakondoo atakayewakomboa. Hata Yesu mwenyewe anatangaza katiba ya unyenyekevu isiyotisha.  Kwa hiyo hadi hapa waisraeli walikanganyika, hawakujua tena jinsi ya kumwona huyo Masiha  ajaye aidha walidhani kuwa Yesu anataka kufutilia mbali Torati na Manabii.

Kwa hiyo, leo Yesu anatoa tamko la msimamo wake juu ya torati (sheria) na manabii ili kufuta sintofahamu hiyo. Anasema: “Msidhani kwamba nimefika kufuta sheria na manabii. Sikuja kufuta, bali kukamilisha.” Kumbe Yesu anaitambua torati na manabii, na kwamba Yeye ni ukamilifu wa yale ambayo Mungu alitaka yakamilike katika torati na manabii. Neno Torati linatokana na neno-tendo la lugha ya kiebrani yaraa lenye maana ya kurusha mshale ili kuonesha upande wa kuelekea. Kwa hiyo Torati ilikuwa ni mshale unaoongoza upande mzuri wa kuelekea lakini haikuwa ni kikomo cha mwisho. Ilibidi kutoka hapo ilipofikia Torati kupiga hatua nyingine zaidi kuelekea inakoongoza hadi kufika kikomo chake komesha. Kumbe safari bado mbichi na Yesu amefika kuikamilisha na kuipelekesha hadi kwenye kikomo chake komesha. Yesu anaendelea kusema kwamba kila kitu kitatekelezeka kama Mungu anavyotaka: “mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka hata yote yatimie.”

Kisha katika mifano sita Yesu anatupatia maelezo ya safari inayobidi binadamu aifanye ili awe na utu wa kweli. Leo Yesu atatupatia mifano minne tu na mingine miwili tutaiona dominika ijayo. Mfano wa kwanza unahusu thamani ya maisha ya binadamu. Yesu alisema: “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa: usiue; na mtu akiua itampasa hukumu.” Maisha ya mtu yana thamani kubwa sana hivi hayatakiwi kuguswa wala kuchezewa. Katika Torati Mungu anakataza kuua au kuchezea maisha ya binadamu kwa sababu ameumbwa kwa mfano wa Mungu. Hata Yesu hakanushi ukweli huo na wala hasemi kama ilivyoandikwa hapa“bali mimi nawaambia.” Hili neno bali au ila limekosewa kwani neno lililotumika hapa la kigiriki ni ego de lego, maana yake mimi ninawaambia.

Kila mmoja anafikiri kuua maana yake kutoa maisha kimwili, (kibaolojia), kumbe kuna mahusiano mengine yanayoua maisha mathalani, hasira. Yesu anaiboresha Torati na kuyakamilisha maisha ya binadamu anaposema: kila amwoneaye ndugu yake hasira ameshaua huyo. Agano la kale linazungumza juu ya hasira ya Mungu. Hasira kwa yenyewe ni nzuri, kwa sababu Mungu anaitumia ili kuleta haki. Aidha hasira ya Mungu inachukia uovu ila inampenda mwovu. Hasira ni hali aliyoweka Mungu ndani mwetu na kutusukuma kutenda mambo. Kwa bahati mbaya hasira ya binadamu haitawaliki na haileti haki bali chuki na uonevu. Hasira ya binadamu haina upendo kwa sababu inatafuta kulipa kisasi.

Kwa hiyo Yesu anasema: “Na mtu akimfyolea (akimtusi) ndugu yake, itampasa baraza.” Kadiri ya haki mpya ya Yesu, kuna namna nyingine pia ya kuua kama vile kutukana matusi ya rejareja au matusi ya jumla jumla, kutukana matusi ya kijanja kijanja au utani, usengenyaji, umbeya nk. Matusi hayo yanamwua mtu kwani yanampotezea hadhi yake na kumnyima furaha ya maisha.  Aidha Yesu anaagiza kupatana kwanza na ndugu kabla ya kutoa sadaka kwa Bwana: “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu uende zako upaane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.” Kwa Wayahudi ilitakiwa kujitakasa kabla ya kutoa sadaka. Picha hii inaweza kueleweka vizuri zaidi ukijua fikra ya Myahudi juu ya kusali na kutolea sadaka. Marabi walisema kwamba unaposali, usiache sala yako hata kama nyoka anakutekenya miguuni.

Kumbe Yesu anasema, si tu unaposali bali hata kama upo altareni unamtolea Mungu sadaka ya kondoo, na hapo unakumbuka kwamba ndugu yako analo jambo na wewe, hapo uache yote altareni uende ukapatane naye kwanza. Katika kitabu cha Didake, kuna makala inayohusu jumuia ya Antiokia kwamba ni unajisi kujiunga na jumuia kabla ya kupatana na mwenzako uliyekoseana naye. Kadhalika huko Siria, karne mbili baada ya Didake kulikuwa na kitabu cha Didaskalia, kilichotoa maagizo kwa Askofu juu ya watu waliogombana katika jumuia yake kwamba: “Wewe Askofu yabidi utatue matatizo haya yaliyokuwepo kati ya wanajumuia wako siku ya jumatatu, ili kwamba kwa muda wa wiki nzima waweze kupatana. Haitegemewi siku ya Bwana watu wakutane bila kupatana.”

Mfano wa pili: “Mmesikia kwamba imenenwa, usizini:” Hivi ndivyo ilivyosemwa katika agano la kale. Naye Yesu anakubaliana nayo kabisa lakini anaongeza kusema: “sasa mimi niwaambia: kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.” Marabi walikuwa wagumu sana katika mahusiano yao na wanawake. Kumbe Yesu alikuwa na marafiki wengi sana wanawake kwa sababu alikuwa na moyo safi akawaacha hata wamshike na kumkumbatia. Kwa hiyo Yesu anataka tuwe na moyo safi kwani moyoni ndiko kunakoanza uzinzi. Usipokuwa na moyo safi huwezi ukaona mambo yasiyoonekana kama anavyosema Yesu: Heri wenye moyo safi maana watamwona Mungu. Kuna urafiki na mahusiano ambayo ni uzinzi wa rohoni au moyoni. Yesu anataka tujitawale moyoni kwa sababu kuna msukumo mwingine unaoweza kuchafua mahusiano yako na wengine hadi kukupelekea kuzini kimwili. Hapo itakuwa “majuto ni mjukuu.”

Kwa hiyo, Yesu anaendelea anasema: “Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika Jehanum.” Jehanum siyo motoni, bali ni shimo kubwa la takataka zilizooza na kunuka vibaya. Yesu anatutahadhalisha, kutoyaharibu maisha, kama vile kuyatupa kwenye hilo shimo la takataka. Katika mazingira ya kuzini, unaweza kuamua kuchangamkia masuala au kuacha. Yesu anasema, ukiwa katika mapambano ya aina hiyo ya kibinadamu, jaribu kutumia kisu na kukata mara moja, yaani ujipe nguvu kabla hujatelezea kwenye shimo hilo la takataka. “Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali; kwa maana yakufaa kiungo chako kioja kipotee, wala mwili wako mzima usitupwe katika Jehanum.” Kumbe hata mikono inaweza kukupelekesha mbali na maisha mazuri. Hapa jehanum maana yake unaweza kuharibu hata jumuia inayokuzunguka, au hata familia, watoto na wajukuu kutokana kuanguka kwako wewe mtu mmoja.

Mfano wa tatu Yesu anasema: “Imesemwa pia: mtu akimwacha mkewe na ampe hati ya talaka.” Kwa ajili ya kumlinda mwanamke Musa aliagiza katika torati kuandika hati ya talaka ili mwanamke aweze kuendelea na maisha yake asije akauawa kwa kupigwa  mawe. Kwa hiyo Yesu hakanushi sheria hii ya Musa. Lakini hiyo haikuwa ndiyo kikomo cha mahusiano ya watu wa ndoa kama alivyotaka Mungu kutoka mwanzo wa uumbaji. Neno hili talaka kwa kiebrania get lina maana ya kidonda au jeraha katika upendo. Kwa hiyo hapa Yesu anataka kutuambia kwamba uchaguzi wetu unaweza kuharibu maisha. Sanasana ndoa namna hiyo unadhalilisha utu kwani jinsia iliwekwa na Mungu kwa ajili ya kujenga upendo. Namna nyingine ya kudhalilisha utu unaweza kuhoji katika namna zetu za kuvaa, za kutembea, za matumizi ya madawa ya kuumua sehemu za mwili, kama zinampa binadamu heshima yake au zinamdhalilisha. Kadhalika lugha anayotumia mkristu, kama inampa heshima binadamu au inamdhalilisha.

Mfano wa nne Yesu anasema: “Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa. Usizuri (usiape), ila mtimizie Bwana nyapo zako; lakini mimi nawaambia: Usiape kabisa.” Zamani watu walipokuwa bado na mioyo migumu waliruhusiwa na Mungu kuapa, ili waweze kutimiza ahadi zao, kama inavyosemwa: Nitamtimizia Bwana kiapo changu. Kwa vyovyote hata Yesu hakatazi kuapa. Lakini Yesu anasema msiape akimaanisha kwamba kila neno la mkristu ni kama ahadi na linayo thamani ya kiapo, yaani kila anachokithibitisha mkristu kinageuka kuwa kama kiapo. Sababu nyingine ya kukataza kuapa hii ni kwamba mara nyingi viapo ni kujilaani. Mathalani viapo vya baadhi ya makabila ya wabantu vinatisha, mmoja anaweza kuapa eti: “Haki ya Mungu, nipasukane msamba, au niunguzwe kwa radi.” Kiapo cha mtindo huo hakina maana yoyote, kwa vile Mungu hawezi kamwe kufanya kazi kama hiyo ya kumshushia mtu radi. Hivi Yesu anahitimisha kwa kusema: “Bali maneno yenu yawe, Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.