2017-02-10 14:51:00

Maadhimisho ya Juma la Wagonjwa Jimbo kuu la Mwanza


Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, Jumamosi, tarehe 11 Februari 2017 yanachukua umuhimu wa pekee kwani hiki ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya 25 ya Wagonjwa Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992. Hii ni siku maalum kwa waamini kusali, kushirikishana na kuwafariji wagonjwa kwa ajili ya mafao ya Kanisa.

Mama Kanisa anawaalika waamini kutambua Uso wa Kristo, kwa wagonjwa na wazee. Ni siku maalum ya kuhakikisha kwamba, wagonjwa wanahudumiwa kwa dhati: kiroho na kimwili! Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, familia ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza inaungana na waamini wengine wote duniani kuadhimisha Siku ya Wagonjwa Duniani. Lakini kutokana na mazingira ya Jimbo kuu la Mwanza, wao wameamua kuadhimisha Juma la Wagonjwa Jimbo kuu la Mwanza.

Lengo ni kuwa karibu zaidi na wagonjwa na wale wote wanaoteseka: kimwili, kiroho, kiakili na kidhamiri, ili kuwaletea faraja na huruma ya Mungu katika shida na mhangaiko yao. Mosi, kwa kuwaombea, pili kwa kusali na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa yaani Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Mpako wa Wagonjwa; tatu kwa kuwapatia misaada ya kiutu pamoja na kuwasikiliza kwa makini, kwani utamaduni wa kuwasikiliza wagonjwa ni dawa inayopatia faraja na kuwatia nguvu!

Maadhimisho ya Juma la Wagonjwa Jimbo Kuu la Mwanza yanapania kuwaenzi wagonjwa kwa kuwasogezea huduma makini katika shida na mahangaiko yao. Kwa kuwapatia ushauri na matibabu, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu kwao. Hiki ni kipindi cha katekesi ya kina, yaani mafundisho bayana kuhusu: maana ya mateso na mahangaiko ya binadamu; maana na nafasi ya Msalaba katika hija ya ukombozi wa mwanadamu. Mambo haya anasema Askofu mkuu Ruwaichi ni muhimu sana kwa nyakati hizi baada ya kuibuka kwa Manabii ambao hawaoni maana ya Msalaba, wanataka kuwapatia watu mbingu ya chapu chapu pasi na mahangaiko! Bila katekesi ya kina, ushirikina na upagani mamboleo vitashamiri sana na badala ya waamini kutafuta majibu ya changamoto zao kwa njia ya mwanga wa Injili, watajikuta wanatafuta majibu ya mkato kwa njia potofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.