2017-02-10 15:36:00

Kuna wasi wasi mkubwa kwa Nigeria kukumbwa na baa la njaa!


Umoja wa Mataifa unasema kwamba,  kuna wananchi zaidi ya lakini moja na ishirini wanaokabiliwa na uhaba wa chakula nchini Nigeria. Ikiwa kama hakutakuwepo na juhudi za makusudi ili kuhakikisha kwamba, chakula cha dharura kinapatikana kwa wakati muafaka katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, watu zaidi ya milioni kumi na moja watakumbwa kwa baa la njaa. Hii inatokana na mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kufanywa na kikundi cha Boko Haram, kilichoanza kupandikiza mbegu ya kifo nchini Nigeria tangu mwaka 2014. Bei ya nishati ya mafuta pia imeshuka kiasi cha kusababisha kuyumba kwa uchumi wa Nigeria.

Katika kipindi chote hiki, takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu elfu ishirini wamekwisha kupoteza maisha yao na wengine zaidi ya milioni mbili wamelazimimka kuyakimbia makazi yao. Tangu aingie madarakani kunako mwaka 2015 Rais Muhammadu Buhari ameendelea kupambana na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, lakini hadi sasa bado kinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Chakula cha dharura kinahitaji kuanzia mwezi Juni hadi Agosti.

Shirila la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linasema, kwa sasa hali ya chakula inaendelea kuwa mbaya siku kwa siku. Watoto wanaendelea kupoteza maisha na wengine wengi kuathirika kutokana na utapia mlo mkali. Zaidi ya watu nusu milioni wako hatari kufa kwa baa la njaa ikiwa kama chakula cha dharura hakitaweza kupatikana kwa wakati! FAO inaendelea kusema, hali ya chakula pia huko Niger mpakani mwa Nigeria si shwari sana, kwani hata huko kuna wananchi wanaoathirika kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.