2017-02-09 13:24:00

Maaskofu Kenya: Watu wanakufa kwa baa la njaa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limeishauri Serikali nchini humo kutangaza hali mbaya ya ukame kuwa ni janga la kitaifa ili kuweza kupata msaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa kwani kuna watu ambao wanateseka, wamekata tamaa na wengine wameanza kupoteza maisha kutokana na makali ya njaa katika baadhi ya maeneo nchini Kenya. Haya yamesemwa na Askofu Philip Anyolo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, Jumanne, tarehe 7 Februari 2017 kufuatia taarifa kutoka kwenye Majimbo mbali mbali nchini Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wenye uwezo, kuonesha mshikamano wa upendo, ili kuunga mkono juhudi za kuokoa maisha ya watu zaidi ya milioni 2. 7 wanaohitaji chakula cha msaada, ikilinganishwa na watu milioni 1.3 waliopatiwa msaada wa chakula cha dharura katika kipindi cha mwaka 2016. Maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa ni: Turkana, Marsabit, Samburu, Mto Tana, Isiolo, Mandera, Garissa, Wajir pamoja na Baringo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika tamko lake linakaza kusema, limekua likifuatilia kwa ukaribu athari za ukame sehemu mbali mbali na sasa inaonekana wazi kwamba, watu wengi wanateseka, kumbe, kuna haja ya kutangaza kwamba, Kenya inakabiliwa na maafa kutokana na ukame wa kutisha! Serikali na mashirika ya misaada ya kiutu yamekuwa yakitoa huduma, lakini bado huduma hii haifui dafu kwa mahitaji yaliyopo kwa wakati huu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.