2017-02-08 14:37:00

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na biashara haramu ya binadamu!


Mama Kanisa tarehe 8 Februari 2017 anaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, sanjari na Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hili ni janga na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Mtakatifu Bakhota alizaliwa nchini Sudan kunako mwaka 1869, akatekwa nyara akiwa na umri wa miaka saba na kuuzwa utumwani mara kadhaa na hatimaye akakombolewa kutoka utumwani na kuingia katika Shirika la Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Wacanossa na kutangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane Paulo II wakati wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu kwa mwaka 2017 inaongozwa na kauli mbiu “Mimi ni mtoto na wala si mtumwa!” Mtakatifu Bakhita anaendelea kuwa ni kielelezo makini cha mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Itakumbukwa kwamba, hata Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2017 aliyaelekeza mawazo yake katika mateso ya watoto wanaojikuta wakiwa ni wakimbizi na wahamiaji pasi na kusindikizwa na wazazi au walezi wao. Watoto hawa wako hatarini kutumbukizwa katika biashara ya haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaowadhalilisha watu kati ya milioni 21 hadi 35 sehemu mbali mbali za dunia.

Hawa ni watoto wanaotumbukizwa kwenye biashara na utalii wa ngono; kazi za suluba kwa mshahara kiduchu! Watoto wanaofanyishwa kazi majumbani na hata wakati mwingine kuolewa wakiwa na umri mdogo, yaani kutumbukizwa kwenye ndoa za shuruti! Kuna watoto wanaopelekwa mstari wa mbele kama chambo wakati wa vita na machafuko ya kisiasa na kijamii! Wote hawa ni waathirika wa utumwa mamboleo unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kutokana na changamoto zote hizi, kunako mwaka 2015, Kanisa likaanzisha Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu Duniani, changamoto iliyovaliwa njuga kwa namna ya pekee na Mtandao wa “Talita Kum”. Huu ni mtandao wa Mashirika  ya Kitawa Kimataifa unaoshirikiana bega kwa bega na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu, Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis; Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO; pamoja na Tume ya Haki na Amani ya Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, nchini Italia.

Sr. Gabriella Bottani kutoka Shirika la Wacomboni anasema, biashara ya utumwa ilifutwa kwenye uso wa dunia miaka mingi iliyopita, lakini leo hii kuna utumwa mamboleo unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyaumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu milioni thelathini wamekwisha tumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu pamoja na viungo vyake. Biashara hii imekuwa ni chanzo cha faida kubwa kwa watu hawa ambao wamefilisika kimaadili kiasi hata cha kushinda faida inayopatikana kwenye biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na silaha duniani. Kuna watu ambao wana ujasiri kiasi hata cha kuthubu kuwataja kwa majina wahusika wa biashara hii, ili waweze kushughulikiwa kisheria kama alivyofanya Blessing Okoedion kutoka Nigeria, baada ya kukombolewa kutoka katika utumwa mamboleo, huyu ni mwanaharakati mzuri sana katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu!

Mtandao wa “Talita Kum” unatekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 70 duniani; wakipewa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama, uhalifu dhidi ya ubinadamu unaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu; kwa kuwatambua waathirika, kuwasaidia pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatendewa haki, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na sheria iweze kuchukua mkondo wake. Hapa kuna haja ya kujikita katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato kwa kutoa elimu makini; kwa kuendesha kampeni za uragibishaji sanjari na kuwalinda watu ambao wanaweza kutumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, haya ni mapambano ya kiuchumi, lakini vita hii zaidi ni ya kimaadili, kwani wafanyabiashara hawa wanatumia umaskini kunyanyasa utu na heshima ya binadamu! Huu ni wakati wa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu kwa wale wote wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuunganisha nguvu ili kupambana na uhalifu huu dhidi ya ubinadamu, kwani unatishia tunu msingi za maisha ya kijamii, ulinzi na usalama; uchumi pamoja na mafungamano ya kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.