2017-02-07 10:47:00

Congo Brazzaville dumisheni haki, amani na umoja wa kitaifa!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amehitimisha safari yake ya kikazi Barani Afrika kwa kuombea amani, umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Congo Brazzaville, pamoja na kuwaweka watu wake chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Tukio hili la kihistoria, limeadhimishwa Jumamosi tarehe 4 Februari 2017 na kutangazwa mubashara na Kituo cha Televisheni cha taifa.

Askofu mkuu Francisco Escalante Molina, Balozi wa Vatican nchini Congo Brazzaville, Wakleri, Watawa na umati mkubwa wa waamini ulishiriki maadhimisho haya katika Kanisa kuu la Mtakatifu Anna, ili kuiweka wakfu nchini yao chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Rais Deniss Sassou Nguesso, viongozi wa Serikali na wanadiplomasia wameshiriki pia katika tukio hili ka kihistoria. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amekazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa; mambo yanayofumbatwa kwa namna ya pekee katika majadiliano; huruma, ukweli na uwazi.

Lengo ni kudumisha ushirikiano, umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kubomoa kuta za ubinafsi, udini na ukabila, mambo ambayo kimsingi yanagumisha na kuhatarisha mafungamano ya kijamii kati ya watu. Familia ya Mungu nchini Congo Brazzaville inapaswa kujikita katika mshikamano wa upendo dhidi ya cheche za utengano na utamaduni wa kutojali wengine kutokana na uchoyo pamoja na ubinafsi. Amewakumbusha waamini kwamba, Mkristo safi ni yule anayejitahidi kufanya hija na Mwenyezi Mungu katika maisha yake, kwa kutenda mema na kukimbia dhambi na nafasi zake.

Askofu mkuu Anatole Milandou, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville aliandaa chakula cha mchana kwa ajili ya heshima ya Kardinali Pietro Parolin na wageni waalikwa kama kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa Kardinali Parolin, kuhitimisha safari yake ya kikazi Barani Afrika, iliyomwezesha kutembelea Madagascar, Kenya, Ethiopia na mwishoni Congo Brazzaville. Kardinali Parolin, mwishoni mwa juma alipata pia nafasi ya kuweza kufanya mazungumzo na Rais Deniss Sassou Nguesso kwa muda wa saa moja na nusu.

Mazungumzo haya yalihudhuriwa pia na viongozi wa Serikali pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville. Masuala ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao; hali tete ilivyo nchini Libya, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na DRC. Viongozi hawa wameridhishwa na uhusiano mwema uliopo kati ya Kanisa Katoliki na Serikali, mahusiano ambayo kwa sasa yameimarishwa zaidi kwa Itifaki ya ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa Katoliki nchini humo. Kanisa Parolin amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kama chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.

Kardinali Parolin amepata bahati pia ya kutembelea na kusali kwenye kaburi la Mtumishi wa Mungu Kardinali Emile Biayenda aliyeishi kati ya mwaka 1927 hadi mwaka 1977 alipouwawa kikatiliki kwa ajili ya imani yake kwa Kristo na Kanisa lake. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville kwamba, mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Kardinali Biayenda utaweza kusonga mbele kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kardinali pia amepata nafasi ya kutembelea kituo cha kuwatunza wazee wagonjwa na kuwafariji wote wanaopata huduma kituoni hapo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.