2017-02-06 08:38:00

Papa Francisko: Maisha ni matakatifu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 5 Februari 2017 aliungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuadhimisha Siku ya 39 ya Maisha Kitaifa iliyoongozwa na kauli mbiu “Wanawake na wanaume kwa ajili ya maisha kwa kuiga mfano wa Mama Theresa wa Calcutta”. Baba Mtakatifu amekaza kwa kusema maisha ya binadamu ni matakatifu, kumbe kuna haja ya kuendeleza utamaduni wa maisha kama jibu makini dhidi ya utamaduni wa kifo usiojali watu na matokeo yake ni kuporomoka kwa idadi ya watoto wanaozaliwa.

Kanisa liko karibu na lina Sali kwa ajili ya kuwaombea watoto ambao wako hatarini kutolewa mimba wangali tumboni mwa mama zao; Kanisa liko pamoja na watu ambao wako kufani, kwani maisha ni matakatifu na kwamba, upendo ni fadhila inayolinda na kudumisha maisha, kumbe asiwepo mtu anayeachwa peke yake. Baba Mtakatifu amenukuhu maneno ya Mama Theresa wa Calcutta aliyesema: maisha ni uzuri unaopaswa kupendwa; maisha ni maisha yanapaswa kulindwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu, kwani maisha ni matakatifu.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wadau mbali mbali wanaoendelea kusimama kidete usiku na mchana kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Amewakumbuka kwa namna ya pekee, Maprofessa kutoka vyuo vikuu na taasisis za elimu ya juu mjini Roma, wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya malezi ya vijana wa kizazi kipya, ili waendelee kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara kwa kujenga jamii inayojikita katika ukarimu na inayomthamini kila mtu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.