2017-02-06 13:31:00

Majadiliano ya kidini yanajikita katika udugu na uhalisia wa maisha!


Majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam kimsingi ni suala changamani linalohitaji sadaka na majitoleo ya waamini wote, ili kujenga na kudumisha umoja, udugu, mshikamano na upendo, kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Tofauti zao za kidini na kiimani zinapaswa kuwa ni utajiri mkubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kuwa ni kikwazo na sababu ya utengano kati ya watu!

Majadiliano ya kidini yanapania pamoja na mambo mengine kukuza maridhiano, haki na amani sanjari na kuondokana na hali ya kudhaniana vibaya, chuki na uhasama pamoja na misimamo mikali ya kidini ambayo imekuwa ni chanzo cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sehemu mbali mbali duniani. Uhuru wa kuabudu, umoja, udugu na ushirikiano ni mambo msingi katika kukuza na kudumisha Injili ya amani duniani, chachu ya maendeleo ya kweli: kiroho na kimwili! Huu ndio mfano bora wa kuigwa unaojikita katika uhalisia wa maisha ya watu, unaoshuhudiwa na Kardinali Diudonnè Nzapalainga, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati pamoja na Imam Omar Kobine Layama wa Msikiti mkuu wa Bangui. Hawa ni viongozi wa kidini ambao wamekita majadiliano ya kidini katika urafiki, udugu na upendo, kiasi cha kuwa ni mvuto kwa waamini wa dini zao. Viongozi wa madhehebu mengine nao wanaendelea kuiga mfano huu bora ili kweli Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati baada ya kinzani na mipasuko ya kidini, iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Kardinali Nzapalainga na Imam Layama ni viongozi ambao wamejipambanua kwa kusimama kidete kukoleza majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini hizi mbili nchini mwao, kiasi hata wamepewa tuzo na Wamissionari wa Comboni ijulikanayo kama “Mundo Negro a la fratenidad 2016” kutoka Hispania. Maadhimisho haya yamefanyika hivi karibuni huko Madrid, Hispania na kumshikirisha Kardinali Carlos Osorro Sierra, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Madrid pamoja na Riay Tatary, Rais wa Jumuiya ya Waamini wa Dini ya Kiislam nchini Hispania pamoja na viongozi wengine wa kidini.

Maadhimisho ya Mwaka 2017 yameongozwa na kauli mbiu “Wakristo na Waislam, Majadiliano ya kidini chini ya paa moja”. Huu umekuwa ni ushuhuda wa kile ambacho viongozi hawa wa kidini wanawahubiria waamini wao na kwamba, ni changamoto inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Tangu mwaka 2013, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ilijikuta ikiingia katika vita na mipasuko ya kidini iliyogubikwa na uchu wa mali na madaraka kiasi hata cha kufumbatwa na udini usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa wananchi wengi!

Makundi ya Seleka na Balaka yakapimana nguvu kiasi cha kutishia na hatimaye, kuharibu mafungamano ya kijamii katika misingi ya udini. Lakini, viongozi wa kidini wanakiri kwamba, kamwe hii haikuwa ni vita ya kidini bali ujanja wa wanasiasa uchwara waliogeuza dini kuwa kama mbereko ya masilahi yao kisiasa: ilikuzima kiu ya uchu wa mali na madaraka. Kardinali Nzapalainga anakaza kusema, kumekuwepo na uhusiano mwema kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Wakristo; mahusiano yanayofumbatwa katika maisha ya kawaida kabisa kwa kuthaminiana kama ndugu wamoja.

Makanisa yamekuwa ni mahali pa kuwahifadhi wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanataka kusalimisha maisha yao wakati wa mipasuko ya kivita na kijamii nchini humo. Imam Omar Kobine Layama wa Msikiti mkuu wa Bangui, kwa muda wa miezi tisa alipewa hifadhi nyumbani kwa Kardinali Nzapalainga, kiasi cha kuonekana kama ndugu wamoja na mfano bora wa kuigwa! Wapiganaji walikuwa wamechoma moto msikiti pamoja na makazi yake na hivyo kuonesha kwamba, majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam yanafumbatwa katika maisha na wala si nadharia tu!

Bangui, ukawa ni mji wa mfano wa kuigwa katika mchakato wa kumwilisha huruma ya Mungu kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha na utume wa Kanisa, tarehe 29 Novemba 2015 akazindua maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Watu wameonja na kugudundua kwamba, majadiliano ya kidini ni dhana inayowekezana kabisa. Jumuiya ya Kimataifa imetambua mchango mkubwa uliotolewa na viongozi hawa wawili katika kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini.

Viongozi hawa wa kidini wanasema, kuna haja kwa waamini kusimama kidete kupinga misimamo mikali ya kidini na kiimani; kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini yanayojikita katika uhalisia wa maisha, ili kujenga misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kwa upande wake, Imam Omar Kobine Layama anasema, majadiliano ya kidini ni kiini cha maisha ya waamini wa dini hizi mbili. Watu wawe na ujasiri wa kukataa kishawishi cha kutumbukizwa katika malumbano, kinzani na mipasuko ya kidini, ambayo mara nyingi inatumiwa na baadhi ya viongozi wenye uchu wa mali na madaraka. Umoja wa Afrika unaiangalia Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini li kuondokana na: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.