2017-02-06 08:52:00

Itifaki ya makubaliano kati ya Vatican na Congo Brazzaville!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na Bwana Clèment Mouamba, Waziri mkuu wa Jamhuri ya Congo Brazzaville, mbele ya Rais Denis Sassou-Nguesso wameweka sahihi katika “Itifaki ya Makubaliano” kati ya Vatican na Serikali ya Congo Brazzaville juu ya ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa Katoliki. Tukio hili limehudhuriwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzavile chini ya uongozi wa Askofu mkuu Anatole Milandou, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville. Tukio hili la kihistoria limetiwa sahihi hapo tarehe 3 Februari 2017.

Kwa upande mwingine, Serikali imewakilishwa na Mawaziri pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali chini ya uongozi wa Waziri mkuu Bwana Clèment Mouamba. Itifaki ya Makubaliano imegawanyika katika Ibara 18 yenye utangulizi na inalitambua Kanisa Katoliki, utume na dhamana yake nchini humo kisheria. Kwa namna ya pekee, viongozi wa Kanisa na taasisi zao, wanatambulikana kisheria. Licha ya pande hizi mbili kujitegemea kadiri ya utume wake, zinapania kushirikiana kwa ajili ya kukuza na kudumisha kanuni maadili, maisha ya kiroho, ustawi na maendeleo ya mtu mzima. Itifaki ya Makubaliano itaanza kutekelezwa pale pande hizi mbili zitakapokuwa zimebadilishana vyombo vya utekelezaji wake.

Kardinali Parolin, katika hotuba yake, amewasilisha salam, matashi mema na baraka za kitume kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, tukio hili linaweka jiwe la msingi la kihistoria katika uhusiano kati ya Vatican na Congo Brazzaville sanjari na maadhimisho ya miaka 40 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili. Uhusiano wa kidiplomasia unaendelea kuimarika; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi kati ya Kanisa na Serikali, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Tunu msingi za maisha ya kimaadili na kiroho zimekuwa ni dira na mwongozo katika hija ya pamoja na zitaendelea kuwa ni vigezo muhimu katika maamuzi ya leo na kwa siku za usoni.

Itifaki ya Makubaliano kati ya Serikali ya Congo Brazzaville na Kanisa Katoliki ni muhimu sana kwa maisha na dhamana ya familia ya Mungu nchini Congo Brazzaville, kwani sasa viongozi wa Kanisa na taasisi zao sanjari na utume na dhamana ya Kanisa vinatambulikana kisheria. Hija ya kitume iliyotekelezwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1980 ni ushuhuda tosha wa upendo wa Kanisa kwa familia ya Mungu nchini Congo Brazzaville. Huu ni ushuhuda wa ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na Kanisa kwa ajili ya huduma makini kwa binadamu pamoja na kuchangia mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.

Kanisa Katoliki halihitaji upendeleo wa pekee, bali linaomba fursa ya kutekeleza dhamana na utume wake kiroho na kimwili kwa uhuru zaidi, ili waamini waweze kuungama na kushuhudia imani yao hadharani. Lakini, ikumbukwe kwamba, uhuru wa kidini ni kiini cha uhuru na haki zote msingi za binadamu. Kumbe, Kanisa na Serikali vinapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kuwahudumia wananchi ambao sehemu kubwa ni waamini pia wa Kanisa Katoliki. “Hapa hakuna haja ya kugombania fito, kwani wote wanapania kujenga familia ya Mungu nchini Congo Brazzaville”.

Majadialiano, ushirikiano na mshikamano kati ya Serikali na Kanisa ni muhimu sana anasema Kardinali Parolin katika kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; pamoja na kusimama kidete kuendeleza tunu msingi za maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu ndani na nje ya nchi! Itifaki ya Makubaliano inafafanua kwa kina na mapana shughuli za Kanisa Katoliki kisheria; uhusiano wake na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini humo, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo. Hii ni Itifaki yenye mchango mkubwa hata katika Jumuiya ya Kimataifa mintarafu haki za kimataifa, hususan uhuru wa kuabudu kwa watu wote.

Mwishoni, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amemshukuru Rais kwa niaba ya watu wa Mungu nchini Congo Brazzaville na kwamba, uwepo wake ni ushuhuda unaopania kuimarisha utawala wa sheria na kanuni msingi za kidemokrasia; mambo msingi kwa ustawi na maendeleo ya nchi kwa leo na kwa siku za usoni. Amewashukuru na kuwapongeza wadau wote waliofanikisha mchakato na hatimaye, utiaji wa sahihi kwenye Itifaki ya Makubaliano kati ya Congo Brazzaville na Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.