2017-02-04 15:36:00

Papa Francisko: Lengo ni huduma ya imani na msaada kwa jirani!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu  Giovanni Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican kuwa mjumbe wake maalum kwenye maadhimisho ya mkutano mkuu wa Shirika la Kijeshi la Malta lenye mchango mkubwa katika kulinda na kushuhudia imani sehemu mbali mbali za dunia. Askofu mkuu Becciu atashirikiana kwa karibu zaidi na Mheshimiwa Balì Fra' Ludwig Hoffmann von Rumerstein, mkuu wa Shirika la Kijeshi la Malta. Lengo ni kuendeleza mafanikio yaliyokwisha kupatikana, ustawi na upatanisho kati ya wajumbe wake yaani: wakleri, watawa na waamini walei.

Askofu mkuu Giovanni Angelo Becciu atashirikiana kwa karibu na Fra' Ludwig Hoffmann von Rumerstein katika mchakato wote wa maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya mkutano maalum mintarafu Katiba ya Shirika hili. Kwa namna ya pekee, atajikita katika masuala yanayogusa upyaisho wa maisha ya kiroho na kimaadili katika Shirika, lakini zaidi kwa wanachama wa kudumu, ili kuwawezesha kuendeleza utukufu wa Mungu kwa njia ya utakatifushaji wa wanachama wake kwa ajili ya huduma ya imani na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na msaada kwa jirani. Baada ya maadhimisho ya mkutano mkuu, Askofu mkuu Becciu ndiye atakayekuwa msemaji mkuu kati ya Shirika na Vatican. Baba Mtakatifu amemkabidhi madaraka yote yatakayomwezesha kutekeleza dhamana na wajibu wake kama mjumbe maalum wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mwishoni, Baba Mtakatifu anatanguliza shukrani zake na kumpatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.