2017-02-04 16:01:00

Ebo! Washeni taa badala ya kulaani giza!


Ndugu zangu leo tutasoma sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka kitabu cha Nabii Isaya, Waraka wa Mtume Paulo na Injili ya Mathayo. Somo la kwanza latoka katika sehemu ya mafundisho makuu ya Isaya kuhusu kufunga ambapo matokeo yake ni kusaidia yule mwenye shida ambao ndio ukamilifu wa tendo lenyewe la kufunga. Bila hilo ufuasi wetu wa dini hubaki kuwa mapokeo na mambo tu ya nje. Kwetu sisi wakristo ni wajibu wa pekee. Ndiyo maana katika somo la kwanza tunaambiwa kuwa kufunga na kusali hakuna maana kama hatutoi haki kwa ndugu zetu.

Katika somo la pili tunasoma sehemu ya barua ya Paulo kwa Wakorintho. Mtume Paulo anaandika kuhusu upendo na anasimulia machungu yake kwa jumuiya ya Wakorintho na anawaalika kufanya malipizi.  Jumapili iliyotangulia tulisikia habari juu ya heri nane. Leo tunasoma sehemu ya injili ambapo utume wa mitume unalinganishwa na chumvi na taa. Ili kuishi na kushuhudia mafundisho ya Yesu, mitume wanatakiwa kutoa ushuhuda juu ya uzuri na ukuu wa Mungu.

Ndugu zangu, inaonekana katika somo la kwanza kuwa Nabii Isaya aliwaelewa vizuri watu wake na inaonekana kuwa ni watu wa sala, kufunga na matendo mengi. Ila katika kufanya hayo ni kama vile wanamtaka Mungu asikilize sala na maombi yao, ila kadiri walivyofanya na kutaka wao. Ndipo hapa nabii anasema – yafaa nini yote hayo? Anawageuzia kibao. Anasema wazi, ingefaa sala zenu na kufunga kwenu kuwe ni kwa manufaa yenu na wengine pia – walisheni wenye njaa, wavisheni walio uchi na wapeni malazi. Mwanga uonekane kwa matendo yenu mema.

Dhamira ya mwanga ni dhamira tajiri katika Biblia. Katika historia ya uumbaji, Mungu aliumba kwanza mwanga, hivyo mwanga una asili yake kwa Mungu na ye yote anayeshiriki mwanga huu anashiriki uzima wa Kimungu. Ndicho anachotushirikisha Nabii Isaya leo. Dhamira hii pia iko wazi katika injili ya leo – chumvi na mwanga. Chumvi ikiharibika haina faida tena. Hivyo kwa mkristo pia. Mwanga unafananishwa na mkristo na si na shughuli anayofanya. Kutoa mwanga kama mkristo ni kusaidia wengine. Yesu ndiye mwanga aliyekuja kwa watu walioishi kwenye giza nene – Mt. 4:13-16. Kwa maana hiyo basi wamfuatao hawana budi kweli kuwa ni mwanga wa ulimwengu.

Ndugu zangu, Nabii Isaya na Mwinjili Matayo wanatupa changamoto ya ufuasi na wanatuonesha kwa namna nyingine ni upi wajibu wa watu wa Mungu hapa duniani. Je leo hii ni kipi kikwazo kikubwa cha ufuasi/ukristo katika dunia yetu? Katika injili ya leo, Kristo anasema mimi na wewe ni mwanga wa ulimwengu. Iko wazi kuwa Yesu anasema yeye ni mwanga wa ulimwengu – Yoh. 8:12. Na katika Mt. 5:14 anasema ninyi ni mwanga wa ulimwengu. Je ni yupi mwanga hapa? Yesu au wafuasi? Katika Yoh. 9:5 anasema wazi, nikiwa bado ulimwenguni mimi ni mwanga wa ulimwengu, hivyo wakati asipokuwepo, wafuasi wake wanachukua nafasi. Huu ndiyo wito na changamoto iliyopo mbele yetu leo. Yesu ametupa nafasi ya kuwa chumvi na mwanga. Wajibu wa wakristo unaelezwa au unaorodheshwa katika maneno mawili – chumvi na mwanga. Kama chumvi ilivyo kwa chakula, vivyo hivyo wakristo kwa ulimwengu. 

Katika Mk. 9:50 tunasoma, chumvi ni njema, lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Muwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi. Kama chumvi tunaalikwa kuwa wafuasi wapole, marafiki na wenye ukarimu kwa wote. Pia kama mwanga, tunaalikwa kuonesha njia. Bila mwanga, hatutaonana, tutagongana na kutumbukia kwenye mashimo. Mwanga watuonesha njia na twaepuka hatari, bila mwanga na chumvi ulimwengu ungekosa sura, usingeonekana, usingependeza na ingekuwa vigumu kuishi. Mwanga na chumvi hufanya ulimwengu uwe mzuri na mahali panapopendeza. Ni wajibu wetu wakristo kutafakari hilo.

Ukristo wetu, ufuasi wetu haupo katika maneno au katika nembo tuliyonayo vidoleni, vifuani, mabegani, vichwani au mwili mzima. Vazi halimfanyi mtu mtakatifu. Katika Yoh. 13:35 twasoma – hivyo watu wote watawatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafuzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi. Ulimwengu wetu wahitaji chumvi na mwanga – ni lazima sisi tuwe hiyo chumvi na huo mwanga – wewe na mimi tunaomfuata Yesu.

Katika kipindi cha kwaresima, Yesu hutualika tufunge na kusali tena kwa siri. Katika fundisho hili la leo Yesu anabadili somo. Anasema ili ulimwengu uwe na mwanga ni lazima tutende wazi kwa matendo mema. Mungu ni mwanga usiozimika. Katika Lk. 2:2 tunasoma kuwa Mungu amemtuma mwanae, ambaye ni mwanga wa ulimwengu. Na wakristo, wanaalikwa katika Efe. 5:8 kuwa watoto wa mwanga na kwamba hawana budi kuwa chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu kupitia matendo ya upendo na haki yanayompendeza Mungu. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI anasema – mtu humkuta/humpata Mungu kupitia mtu aliyekutana na Mungu. Ndiyo maana Mtume Paulo katika somo la pili anasema kuwa mwanga wa Mungu utaangaza duniani kupitia kazi za watoto/watu wake. Injili ya leo hakika yatuweka njia panda – eti kama kuna giza na machungu ulimwenguni ni kosa letu sisi wafuasi. Tunakumbushwa kuwasha taa, badala ya kulaani giza.

Tumsifu Yesu Kristo. Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.