2017-02-03 11:28:00

Ukarimu na upendo kwa maskini wanaoishi mijini


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa nia zake za jumla kwa Mwezi Februari 2017 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo kwa jirani zao hasa katika miji inayoendelea kukua na kupanuka kama uyoga, kiasi cha kuzalisha makundi  makubwa ya maskini wa hali na kipato! Mshikamano wa upendo kwa kumpatia mtu mwenye baridi kikombe cha kahawa ya moto kunaweza kuleta mabadiliko katika maisha ya mtu mwenye shida na mahangaiko ya ndani!

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali pamoja naye kwa ajili ya kuwaombea watu wanaokabiliana na changamoto za maisha, ili waweze kupata msaada na kuonja ukarimu kutoka katika Jumuiya za Kikristo. Itakumbukwa kwamba, nia za Baba Mtakatifu zinasambazwa na Utume wa Sala Kimataifa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini katika mwezi Februari kuonesha upendo na ukarimu kwa maskini na wanaoteseka sehemu mbali mbali za mijini. Licha ya maendeleo makubwa ya vitu, lakini kuna mamilioni ya watu wanaoteseka kutokana na umaskini. Hawa ni watu wasiokuwa na fursa za ajira wala makazi. Kimsingi hawa ni watu wanaopaswa kusaidiwa anasema Baba Mtakatifu Francisko. Mshikamano wa upendo hauna mipaka, vikwazo wala umri, kila mtu kwa kadiri ya nafasi na uwezo wake anaweza kuchangia mchakato wa urafiki, upendo na mshikamano wa dhati. Ujumbe huu wa Video umeandaliwa na Kampuni ya ”La Machi” kwa kushirikiana na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.