2017-02-03 11:01:00

Furaha ya upendo unaomwilishwa kila siku katika familia!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anashiriki katika mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki India lenye madhehebu ya Kilatini. Mkutano huu umefunguliwa rasmi hapo tarehe 27 Januari na unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 8 Februari 2017 huko Bhopal, Madhya Pradesh. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “umuhimu wa kutangaza Furaha ya upendo ndani ya familia zetu”.

Kardinali Baldisseri ametumia fursa hii kupembua kwa kina na mapana Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Huu ni Waraka unaopania kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu wa ndoa, ili kuwawezesha kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia na wala si ufundi wa kufafanua taalimungu. Leo hii familia inakumbana na changamoto nyingi zinazotishia maisha na utume wa familia, kumbe, hapa changamoto ni kuungana na Mtakatifu Paulo katika utenzi wake wa upendo! (Rej. 1Kor. 13: 4- 7).

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume anakaza kusema: upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; haoni uchungu; hauhesababu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, hutumaini yote, hustahimili yote. Pale ambapo uvumilivu na upendo vinatoweka, familia inageuka kuwa ni uwanja wa vita na hapo ni patashika nguo kuchanika! Hapa kuna haja ya kuvumiliana, kusaidiana, kurekebishana na kuthaminiana, ili kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha.

Wanandoa wajifunze na kufundishana namna ya kutenda kwa upendo, uvumilivu na msamaha, daima kila mwanafamilia akijitahidi kujisadaka ili kutekeleza na kumwilisha Agano la Ndoa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Wajitose kimasomaso bila kudai fidia, daima wakitahidi kuwa wakweli na wa wazi katika safari ya maisha yao ya pamoja kama wanandoa. Wakubali karama ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha pamoja na kutambua mapungufu yao, tayari kujisahihisha na kujirekebisha ili waweze kuwa ni watu wema zaidi. Wanandoa wajitahidi kusamehe na kusahau, changamoto ambayo inahitaji kweli neema na baraka ya Mungu, ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya upatanisho na msamaha kwa kutambua kwamba, hata wao wamesamehewa na kupatanishwa na Mungu.

Wanandoa wajenge utamaduni na tabia ya kuaminiana, kuthaminiana bila ya kuwa na woga wala wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko, tabia ambayo wakati mwingine inajikita katika hali ya kudhaniana vibaya, hatari katika maisha ya ndoa! Kutokana na udhaifu wa kibinadamu, wanandoa wanapaswa kusaidiwa na Mama Kanisa katika hija ya maisha yao; kwa kuwaongoza, kwa kuwapatia nafasi ya kufanya mang’amuzi ya maisha na wito wao na pale waliolegea na kuanguka, waweze kusimama tena na kuingizwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Baldisseri anakaza kusema, wakati wa kufunga Ndoa, wanaharusi wanaahidi kuwa waaminifu kwa wenzi wao wa ndoa katika taabu na raha; katika magonjwa na afya; kwa kupendana na kuheshimiana siku zote za maisha.

Wanandoa watarajiwa wanapaswa kupewa majiundo makini ya awali na endelevu kwa kutambua kwamba, Sakramenti ya Ndoa ina uzuri, wema, utakatifu pamoja na changamoto zake zinazopaswa kufumbatwa katika imani, matumaini na mapendo ya dhati kwa Kristo na Kanisa lake! Kanisa liendelee kuwa karibu katika maisha na utume wake na wanandoa waliotalakiana na hatimaye, kuoana kiserikali. Huruma ya Mungu ni kiini cha Injili ya Kristo na kwamba, ni dhamana na wajibu wa Kanisa kuwaonjesha waamini huruma hii katika maisha yao.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anakaza kusema, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu, amejifungamanisha na kila familia ya binadamu na kuendelea kuwepo kati ya wanafamilia, ili kuwaenzi na kuwategemeza katika furaha, magumu na changamoto za maisha na utume wa familia, kwa kuwaamshia fadhila ya matumaini. Yesu anaendelea kuwa ni msafiri mwenza wa wanafamilia kwa kutambua kwamba, wao ni wadhambi, daima wanahitaji huruma, upendo na msamaha wake, ili siku moja waweze kuishi utimilifu wa maisha ya familia ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.