2017-02-01 08:29:00

Changamoto za maisha ya kitawa! Uaminifu!


Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya 21 ya Watawa Duniani inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican majira ya saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya. Maadhimisho ya Mwaka huu wa 2017 yanabeba umuhimu wa pekee, kama shukrani kwa Mwenyezi Mungu na muda wa sala kwa ajili ya kuombea mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayofanyika mjini Vatican, Oktoba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”.

Askofu mkuu Josè Rodrìguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, maisha ya kitawa yanakabiliwa na changamoto nyingi, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, watawa wanakuwa waaminifu wakati wa majaribu katika maisha na wito wao. Ili kufikia hatua hii, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kweli mtawa ana wito wa kitawa, unaopaswa kukuzwa, kudumishwa na kuendelezwa kwa njia ya majiundo ya awali na endelevu.

Bado kuna changamoto za jumla zinazoyakabili Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, mintarafu Waraka wa “Mahusiano kati ya Maaskofu na Watawa” “Mutuae relationes” unaopyaishwa kwa sasa ili hatimaye, kuibua Waraka mpya utakaokidhi changamoto mamboleo. Tayari Baba Mtakatifu Francisko amekwisha agiza kwamba, Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu yapitie upya Waraka huu ili uweze kupyaishwa zaidi. Waraka mpya unaoandaliwa utajikita zaidi katika mahusiano kati ya: Maaskofu, Wakleri na Watawa katika ujumla wao!

Waraka mpya utajikita zaidi katika kanuni, sheria na taratibu za maisha na utume wa Kanisa, kielelezo makini cha Kanisa kama chombo cha umoja kinacho thamini karama za kihierarkia zinazojikita katika Daraja Takatifu na karama za Roho Mtakatifu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Katika mazingira haya, bado kuna kinzani kati ya uhalisia wa maisha, Wakleri na Watawa hasa katika Makanisa mahalia. Kumbe, hapa jambo la msingi ni mchakato wa mpito kutoka katika nadharia na kumwilisha katika uhalisia wa maisha na utume wa watawa katika Makanisa mahalia.

Hapa Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa Wakleri na Watawa kujenga utamaduni wa kusikilizana kwa dhati pamoja na ukarimu; majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji pamoja na kufahamiana kwa undani zaidi. Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliliomba Kanisa ili kuwepo na majiundo makini ya Kanisa mintarafu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Taalimungu ya maisha ya kitawa liwe ni somo la msingi katika seminari za majimbo. Watawa kwenye nyumba za malezi wanapaswa kufundishwa kuhusu: Taalimungu ya Kanisa mahalia; Dhamana na Utume wa Askofu Mahalia, ili kujenga na kudumisha madaraja ya Wakleri na Watawa kukutana katika maisha na utume wa Kanisa, badala ya mwelekeo wa sasa wa kuwaona watawa kuwa kama ni “wafanyakazi” kwa Makanisa mahalia!

Umiliki wa mali kwa watawa kwenye Makanisa mahalia, imekuwa ni changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi kwa dhati kabisa ili kuweza kupata maoni kutoka kwa wadau mbali mbali anasema Askofu mkuu Josè Rodrìguez Carballo. Waraka mpya unapaswa kuzizingatia: Sheria za Kanisa, Kanuni za Kitaalimungu pamoja na Mwongozo wa shughuli za kichungaji na kwamba, wahusika wakuu hapa ni Maaskofu pamoja na watawa.

Uaminifu kwa maisha na wito wa kitawa pamoja na karama za Mashirika husika ni cheche muhimu sana ya utakatifu wa maisha; unaowajengea uwezo watawa kushuhudia karama za mashirika yao katika maisha na utume wa Kanisa. Ni ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha watawa kuweza kujisadaka bila ya kujibakiza. Ikumbukwe kwamba, kila mwaka kuna watawa wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya utakatifu wa maisha na utume wa Kanisa. Changamoto kubwa inayowakabili watawa katika maisha na wito wao ni hali ya wito wa kitawa kunyauka na kukauka kama kigae!

Mapungufu na udhaifu wa kibinadamu katika masuala ya mahusiano ya ndani; ugumu wa kuishi mashauri ya Kinjili yanayofumbatwa katika maisha ya kijumuiya, kutokana na ubinafsi na baadhi ya watawa kutaka kumezwa mno na malimwengu. Hapa jambo la msingi ni malezi na makuzi ya maisha ya kiroho, kiimani na kimaadili. Watawa thabiti ni mashuhuda pia wa imani inayomwilishwa katika matendo! Maisha ya kiroho yanajikita katika ari na mwamko wa kinabii, kitume na ushuhuda makini! Ikiwa kama imani ni legelege, maisha ya kiroho yatakuwa hoi na matokeo yake ni kinzani na mipasuko katika maisha ya kijumuiya ndani ya mashirika. Udhaifu wa imani una madhara makubwa katika maisha ya kiroho pamoja na mahusiano ya kidugu ndani ya mashirika.

Ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi, kuna haja ya kuwa na maamuzi mazito katika maisha ya kitawa na kazi za kitume, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa badala ya kuwa na watawa wasiokuwa na msimamo katika maisha. Changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia hazina budi kufanyiwa kazi, ili watawa wasimezwe mno na malimwengu. Majiundo makini ya awali yawasaidie watawa kufanya maamuzi ya busara katika maisha yao ili kuweza kuwa na uwiano mzuri wa ekolojia ya maisha ya kiroho, maisha ya kijumuiya sanjari na utume wa uinjilishaji.

Takwimu za watawa walioacha maisha ya wakfu zinatisha! Hawa ni watawa wenye umri kati ya miaka 30 hadi 50. Watawa walioacha utawa katika kipindi cha mwaka 2015- 2016 ni 2300. Watawa 271 wameondolewa Mashirikani na Mapadre 518 wamefunguliwa kifungo cha Useja sasa wanaweza kuishi maisha ya ndoa. Idadi ya Mapadre watawa wanaoacha Mashirika yao na kujiunga na Majimbo inazidi kuongezeka, ingawa idadi ya Mapadre wanaoacha kabisa maisha ya kitawa inaendelea kupungua kwa sasa ni Mapadre 225 ambao wanadai kwamba, hawakuwa na wito wala maisha ya Kipadre.

Ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi anasema Askofu mkuu Josè Rodrìguez Carballo kwamba, kuna haja ya kuwa na mang’amuzi ya dhati katika wito na maisha ya kitawa bila kusahau majiundo awali na endelevu ya kiroho, kiutu, kiimani na kiakili. Nia na lengo ni mambo msingi badala ya Mashirika ya kitawa kuangalia idadi ya watawa wa Mashirika yao. Si kila mtu anaweza kuwa mtawa. Waombaji wanaotoka seminari moja na kujiunga na seminari nyingine au shirika moja na kujiunga na shirika jingine, wanapaswa kuangaliwa kwa umakini zaidi. Mang’amuzi makini yasindikikwe na wadau mbali mbali katika safari ya maisha ya kitawa na kazi za kitume. Majiundo makini ya awali na endelevu yapewe kipaumbele cha kwanza, bila kusahau majiundo katika uaminifu, utamadunisho na mahusiano kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.