2017-01-31 14:51:00

Yesu hakutafuta umaarufu katika maisha na utume wake!


Mama Kanisa Jumanne tarehe 31 Januari 2017 ameadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco, Padre na Baba aliyejisadaka kwa ajili ya utume kwa vijana. Neno la Mungu linawataka waamini kuwa na subira katika majaribu, kwa kutambua kwamba, wanazungukwa na wimbi kubwa la mashuhuda wa imani, changamoto ni kuweka kando zigo la dhambi, ili kumtazama Kristo na kuanza kutimua mbio katika imani inayofumbatwa na kupata utimilifu wake kwa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican anaendelea kukaza kwa kusema, Yesu uko kati pamoja na watu wake, ili kuwapatia nafasi ya kuweza kushikamana na kuchangamana pamoja naye. Yesu katika maisha na utume wake, daima alikuwa anawatafuta watu, ili kuwakazia uso wa huruma na mapendo; aliwakazia wote uso wake, lakini daima kila mtu alikuwa na nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Yesu!

Hakuvutwa sana na umati mkubwa wa watu, bali mtu mmoja mmoja aliyetamani kukutana naye katika hija ya maisha yake. Hivi ndivyo alivyofanya yule mwanamke aliyetokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akajikaza na kugusa upindo wa vazi la Yesu na kupona! Ndio mwelekeo kama huu, alipomhurumia Mkuu wa Sinagogi na kumfufua binti yake aliyekuwa amelala kwenye usingizi wa amani! Binti akafufuka na kupewa chakula. Yesu alikuwa anawaangalia wote, wakubwa kwa wadogo; aliguswa na furaha, mahangaiko na matumaini ya watu, kwani alikuwa daima kati pamoja na watu!

Hakuwa ni mtu aliyegutuka kwa kuona mambo makubwa, lakini alithamini pia mambo madogo madogo katika maisha ya watu, ili kuwarejeshea tena furaha na amani ya ndani. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kupiga mbio za imani kwa saburi pamoja na  kumtazama Yesu, ili aweze kuwashangaza kama alivyofanya siku ile alipomfufua Binti wa Yairo. Waamini wajibidishe kutembea huku wakiangaliana na Kristo Yesu, hapo kweli watashangazwa wanapokutana uso kwa uso na Yesu. Waamini wasiogope kumwendea Yesu, wawe na ujasiri kama alivyofanya yule mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili! Hatimaye, Baba Mtakatifu anasema, inapendeza kukutana uso kwa uso na Kristo Yesu, jaribu utashangazwa katika maisha yako!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.