2017-01-31 08:54:00

Yanayoendelea kujiri katika ziara ya Kardinali Parolin Barani Afrika!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anaendelea na ziara yake ya kikazi nchini Madagascar kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Madagascar. Jumamois, tarehe 28 Januari 2017, Kardinali Parolini pamoja na ujumbe wake, walitembelea Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Madagascar kilichoanzishwa kunako mwaka 1952 na kwa sasa kuna wanafunzi kutoka katika mataifa 13.

Padre Marc Ravelonantdandro, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Madagascar akizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Chuo hiki, alifafanua vitivyo vilivyopo Chuoni hapo pamoja na masomo yanayotolewa kama sehemu ya mchango wa Kanisa katika mchakato wa kumuunda mtu mzima: kiroho na kimwili; tayari kuwajengea uwezo wanafunzi, ili wanapohitimu masomo yao Chuoni hapo waweze kuwa ni raia wema watakaowajibika barabara katika ujenzi wa nchi zao.

Kardinali Parolin katika hotuba yake, Kanisa lilipokuwa linafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Thoma wa Akwino, Mwalimu wa Kanisa, aliwataka wasomi nchini Madagascar kujizatiti zaidi katika kutafuta ukweli; kujiandaa kikamilifu ili waweze kuwa kweli ni raia wakomavu na wanaowajibika katika ustawi na maendeleo ya nchi zao. Amewataka wanafunzi kujizatiti kikamilifu katika masomo ili kupata ujuzi, maarifa na stadi za maisha bila kusahau “kujichimbia pia” katika Maandiko Matakatifu, ili kuwa na ukomavu! Wasomi wajenge utamaduni wa kusikiliza, kujadiliana na kuheshimiana hata katika tofauti zao, daima wakilenga mafao ya wengi.

Jumamosi jioni, Kardinali Pietro Parolin, alitembelea eneo la Chuo Kikuu cha Kikatoliki nchini Madagascar na baadaye kutembelea na kuzindua Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Madagscar, CEM. Amepata pia bahati ya kutembelea eneo la Chuo kikuu linalotoa makazi kwa wanafunzi maskini kutoka katika Majimbo 21 yanayounda Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar. Hapa wanafunzi wanatakiwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa masomo kama sehemu ya mchakato wa kupambana na umaskini wa hali na kipato. Vijana hawa wametakiwa kutambua na kuheshimu mchango wa Kanisa katika mapambano dhidi ya baa la umaskini, ili hata wao waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato ili kujenga jamii inayomsikiwa katika matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Kardinali Parolin, amebahatika pia kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Madgascar katika makao makuu mapya. Amesikiliza kwa umakini: mafanikio, fursa, changamoto na matatizo yanayoyalikabili Kanisa nchini Madagascar. Kardinali Parolin amewataka Maaskofu kuwa wachungaji waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kuendelea kuwa ni Mababa wa imani na mashuhuda wa Injili ya Kristo; tayari kusimama kidete kuwalinda na kuwahudumia maskini wanaounda asilimia 95% ya idadi ya wananchi wote wa Madagascar. Kanisa liendelee kujipambanua katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Maaskofu wametakiwa kuwa karibu sana na Mapadre ambao ni wasaidizi wao wa kwanza katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina. Wawe makini katika majiundo ya awali na endelevu; kwa kuwa na mang’amuzi makini katika maisha na wito wa Kipadre. Maaskofu wasaidie mchakato wa kuwafunda waamini walei, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa haki, amani na maridhiano katika Jamii kwa kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi; daima wakisimana kidete kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa liendeleze mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumapili tarehe 29 Januari 2017 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu akisaidiana na Kardinali Maurice Piat wa Jimbo Katoliki la Port- Louis, nchini Mauritius, Askofu mkuu Paolo Gualtieri, Balozi wa Vatican nchini Madagscar; Maaskofu na Mapadre zaidi ya 200 kutoka Madagascar. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Uwanja wa michezo wa “Mahamasina” ulioko mjini Antananarivo na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali na familia ya Mungu nchini Madagascar katika ujumla wake. Maadhimisho haya yalikuwa ni kilele cha Jubilei ya miaka 50 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Madagascar.

Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amekumbusha kwamba, kunako mwaka 1989, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Madagscar. Amefafanua kwa kina na mapana kuhusu Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu katika Agano Jipya. Waamini wanatumwa kwenda duniani kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kuwashirikisha na kuwamegea watu Furaha ya Injili, kwa kukutana na kukaa na watu, ili kuwaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Waamini wajifunze kumsikiliza Kristo kwa makini na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, kielelezo makini cha imani tendaji! Waamini wamekumbushwa kwamba, daima Mwenyezi Mungu anatenda kwa ajili ya kuwasaidia na kuwa enzi maskini ambao kimsingi ni wapole na wanyenyekevu wa moyo! Waamini washiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Heri za Mlimani ni tema ambayo pia ilitumiwa na Maaskofu Katoliki Madagascar katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo nchini humo kwa muda wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2014 na kuhitimishwa mwaka 2016 huko, Jimbo kuu la Cracovia, nchini Poland.

Kardinali Parolin amewakumbusha waamini kwamba, Jumapili tarehe 29 Januari 2017, Jumuiya ya Kimataifa imaeadhimisha Siku ya 64 ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukoma Duniani. Amewashukuru wadau mbali mbali wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wakoma nchini Madagascar. Mwishoni amemwomba Mtakatifu Jacques Berthieu na wenyeheri Victoire Rasoamanarivo pamoja na Louis Rafiringa kuwaombea ili kweli Heri za Mlimani ziweze kuwa ni utambulisho wao wa Kikristo! Jumapili jioni, Kardinali Parolin, ametembelea Monasteri ya Watawa wa Karmeli na kuwaalika kusali kwa ajili ya Baba Mtakatifu na Kanisa katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.