Mkutano wa 28 wa Umoja wa Afrika umeanza Jumatatu 30 Januari 2017 ambapo wanahudhuria
wakuu wa nchi na viongozi wa serikali wa nchi 54 kutoka bara la Afrika. Viongozi hawa
wanatazamiwa kujadili maswala muhimu yanayoigawanya jumuiya ya Kiafrika wenye Kaulimbiu
"kupata faida kamili ya mgao wa watu kwa kuwekeza katika vijana.
Maandalizi ya Mkutano huo yalianza 22 Januari 2017 katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis
Ababa na kikao cha kawaida cha Kamati ya wawakilishi wa kudumu (kuanzia tarehe 22
-24 Januari), ilifuatiwa kikao cha Baraza Kuu wakiwepo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa
nchi wanachama (kuanzi Januari 25 hadi 27), na mwisho Kikao cha Wakuu wa nchi na viongozi
wa serikali ambacho kimefunguliwa rasmi Jumatatu, Januari 30.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Ethiopia, serikali imetoa wito kwa jeshi ili
kuhakikisha usalama umeimarika katika mji wa Addis Ababa wakati wa mkutano huo.Msemaji
wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia amesema zaidi ya viongozi 4,000 wa ngazi ya
juu wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo, ikiwa ni pamoja na Wakuu wa nchi na
viongozi wa serikali 37 na Mawaziri wa Mambo ya Nje wasiopungua 49.
Aidha katika ufunguzi wa Mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
katika hotuba yake amesema kuwa umoja huo upo tayari kufanya juhudi za kuona amani
inapatikana barani Afrika.Hali kadhalika Bwana Guterres ameashiria namna baadhi ya
nchi za Kiafrika zilivyoshindwa kupiga hatua kubwa kiuchumi na kuongeza kuwa, umoja
huo unafanya juhudi za kuanzisha mashirika kwa ajili ya ustawi endelevu katika nchi
za Kiafrika.Vilevile Katibu Mkuu ameongeza kwamba, hitilafu zilizopo kati ya nchi
za Kiafrika zinaweza kupatia ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo kwa kuungwa mkono na
nchi wanachama wa umoja huo na ule wa kimataifa.
Hali kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amemhakikishia Rais
John Magufuli wa Tanzania ushirikiano kutoka chombo hicho ikiwemo usaidizi kwenye
tatizo la wakimbizi.Ametoa hakikisho hilo wakati wa mazungumzo kati yao, kando ya
mkutano wa wakuu wa Muungano wa Afrika,AU huko Addis Ababa, Ethiopia.Amesema Umoja
wa Mataifa utatia msisitizo zaidi katika kuhimiza wadau mbali mbali wa maendeleo wa
jumuiya ya kimataifa kuchangia juhudi zinazofanywa na Tanzania za kuwapatia hifadhi
wakimbizi wa nchi mbalimbali tangu mwaka 1971.
Kwa upande wake Rais Magufuli ameelezea juhudi za Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki
za kushughulikia mzozo wa Burundi, akisema harakati hizo zinazoongozwa na Rais mstaafu
wa Tanzania Benjamin Mkapa zinaendelea vizuri.
Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
All the contents on this site are copyrighted ©. |