2017-01-31 15:25:00

Juma la Watawa nchini Ureno!


Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kujenga na kudumisha maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, upendo na mshikamano katika maisha ya kijumuiya ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo! Maisha ya kitawa yanapaswa kuwa ni sauti ya kinabii na ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Watawa watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika karama na utume wao!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno kwa kutambua na kuthamini mchango wa watawa katika maisha na utume wa Kanisa linaadhimisha Juma la Maisha ya Kitawa nchini Ureno kwa kuongozwa na kauli mbiu “Watawa katika huduma ya uhai”. Maadhimisho haya yanafanyika kuanzia katika ngazi ya Jumuiya, Parokia, Kijimbo na hatimaye, kilele chake ni tarehe 2 Februari 2017, Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya 21ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2017.

Huu ni muda wa sala, tafakari na shuhuda kuhusu maisha ya kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa. Lengo ni kuwajengea waamini walei uwezo wa kutambua na kuthamini mchango wa watawa katika maisha na utume wa Kanisa hususan katika huduma ya afya, elimu, ustawi na maendeleo ya wengi, huko kuna umati mkubwa wa watawa wanaoendelea kujisadaka hospitalini, shuleni na kwenye nyumba za watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi! Kwa hakika, watawa ni majembe ya huduma ya uhai! Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya watawa ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.