2017-01-31 15:05:00

Jiandaeni na wajibikeni vyema kukabiliana na baa la njaa Tanzania


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, watanzania wengi kwa sasa wanasumbuliwa na hofu ya kuchelewa kwa mvua kunyeesha kwa wakati muafaka, hali ambayo inatishia nchi hapo baadaye kugubikwa kwa baa la njaa. Hii ni hofu na changamoto kwa Serikali na wadau mbali mbali ili kujiandaa barabara kukabiliana na baa la njaa kwa siku za usoni kwa kuwajibika vyema.

Askofu mkuu Ruwaichi anaiomba Familia ya Mungu nchini Tanzania katika ujumla wake kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuijalia Tanzania mvua ya kutosha, kusudi waweze kupata mahitaji yao msingi na hatimaye, kuendelea kumtumikia. Anatoa mwaliko na kuwakumbusha watanzania kwamba, hali mbaya ya hewa inayotishia maisha ya watu wengi ni matokeo ya uharibifu wa mazingira. Watanzania wanapaswa kujifunza kuwa ni sehemu ya majibu ya changamoto zinazowakabili, kwa kuhifadhi mazingira nyumba ya wote; kwa kutunza na kudumisha vyanzo vya maji pamoja na kuendelea kujizatiti kutunza na kuhifadhi mazingira. Pale ambapo wameharibu mazingira waanze mchakato wa kuyarekebisha na kuyaboresha zaidi kwa kupanda miti inayofaa, kwa kutunza vyanzo vya maji na kuondokana na uchafuzi wa mazingira, ardhi na hali ya hewa!

Askofu mkuu Ruwaichi anawashauri wanasiasa kuwa wanyofu wanapokabiliana na changamoto katika utumishi wao na kamwe wasiogope kuzikabili changamoto hizi kwa ukamilifu. Serikali itumie kodi inayokusanywa kutoka kwa wananchi ili kufanya maandalizi mapema ya kupmbana na baa la njaa linalotishia maisha ya wananchi wengi Tanzania. Viongozi wa Serikali wajizatiti kusimamia na kutekeleza kwa dhati sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi. Anawashauri wanasiasa na Serikali katika ujumla wake kufikiri kwa makini, ili kutenda kwa uwazi, ukweli, uzalendo na uwajibikaji wa dhati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.