2017-01-30 10:51:00

Maaskofu kutoka Serbia, Kosovo, Macedonia na Montenegro wako Vatican


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu alisitisha hija za kitume zinazofanywa na Mabaraza ya Maaskofu mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Utaratibu wa Baba Mtakatifu kukutana na Maaskofu unaendelea tena kwa mwaka huu 2017 na tayari amekwisha kutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Cambodia na Laos.

Jumatatu, tarehe 30 Januari 2017, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Watakatifu Cyril na Methodi, CEICEM. Hawa ni Maaskofu wanatoka: Montenegro, Kosovo, Serbia na Macedonia. Waamini wa Kanisa Katoliki ni wachache sana katika maeneo haya ikilinganishwa na idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam na Makanisa ya Kiorthodox. Kumbe, hapa changamoto kubwa ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene.

Haya ni maeneo ambayo yameguswa na kutikiswa na vita, kinzani na mipasuko ya kisiasa, kidini na kijamii, changamoto kubwa ni kuendeleza mchakato wa haki, amani na upatanisho, ili kuganga na kuponya madonda ya chuki na uhasama, ili kujenga mazingira yatakayosaidia kukoleza mchakato wa maridhiano kati ya watu. Kanisa Katoliki katika maeneo haya linaendelea kujielekeza zaidi katika utume kwa vijana wa kizazi kipya hasa katika sekta ya elimu ambayo ni ufunguo wa maendeleo ya wengi.

Sekta ya elimu imekuwa pia ni uwanja wa majadiliano ya kidini na kiekumene katika nchi hizi bila kusahau wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Haya yamesemwa na Askofu Ladislav Nemet, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu ya Watakatifu Cyril na Methodi, CEICEM katika mahojiano maalum na Radio Vatican. Kuna wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Macedonia na Serbia, linalotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Baada ya Jumuiya ya Ulaya kuweka Mkataba wa kudhibiti wakimbizi na wahamiaji na Uturuki, idadi ya wakimbizi na wahamiaji inaendelea kupungua! Shirikisho hili linasema. kutokana na changamoto mbali mbali limependekeza ligawanywe na kuwa ni Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yanayojitegemea. Hadi hapo, yatakapogawanya na Vatican, Maaskofu wataendelea kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu katika maeneo yao. Changamoto ni kuendelea kuimarisha Kanisa Katoliki katika maeneo haya kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko sanjari na kujikita katika mchakato wa upatanisho kati ya Croatia na Serbia, ili kujenga na kudumisha Injili ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.