2017-01-29 09:36:00

Ziara ya Kardinali Parolin Barani Afrika!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 26 Januari hadi tarehe 4 Februari 2017 anafanya ziara ya kwanza ya kikazi Barani Afrika kwa kutembelea Madagascar, ili kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Madagascar. Anatembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, ili kuweka sahihi mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa Katoliki na baadaye atapata nafasi ya kusimama kwa kitambo kidogo nchini Kenya. Kardinali Parolin katika ziara hii anaambatana na Monsinyo Gianfranco Gallone, afisa mwandamizi kutoka katika idara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Tarehe 27 Januari 2017 Kardinali Parolin amewasili nchini Madagascar na kupokelewa na viongozi wa Serikali, Kanisa na umati mkubwa wa familia ya Mungu uliojitokeza kwa nyimbo na shangwe, kama kielelezo cha ukarimu, upendo na mshikamano kutoka kwa Familia ya Mungu nchini Madagascar. Baadaye alikutana na kuzungumza na Rais Hery Martial Rajaonarimanampianina kwenye Ikulu ya Madagascar pamoja na kubadilishana zawadi. Kardinali Parolin alikuwa ameambatana na Askofu mkuu Paolo Gualtieri, Balozi wa Vatican nchini Madagascar  na wajumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar waliokuwa wanaongozwa na Kardinali Maurice Piat, Askofu wa Jimbo Katoliki Port-Lous, nchini Mauritius. Rais Hery katika hotuba yake, ameoneshwa kuridhishwa na mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Madagascar. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, uhusiano kati ya Vatican na Madagascar umeimarishwa maradufu.

Rais amesema, Kanisa limeendelea kuchangia katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii pamoja na majiundo endelevu kwa wananchi wote wa Madagascar. Mchango wa Kanisa umesaidia kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili kwa kujikita pia katika mapokeo, mila na tamaduni njema za Kiafrika. Lengo ni kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili! Serikali itaendelea kutoa ulinzi na usalama kwa taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa ili ziweze kutekeleza dhamana yake kwa amani na utulivu. Serikali kamwe haitakubali “kupigishwa magoti” na waamini wachache wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani na kwamba, mchakato wa majadiliano ya kidini hauna budi kukuzwa na kudumishwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi! Kumbe, maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Madagascar ni fursa makini ya kuimarisha mafungamano yaliyokwishafikiwa kati ya nchi hizi mbili!

Kardinali Pietro Parolin kwa upande wake, amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu nchini Madagascar, Papa anayependwa sana na vijana wa kizazi kipya nchini humo. Ameishuruku familia ya Mungu nchini Madagascar kwa mapokezi makubwa ya kukata na shoka waliyomfanyia. Kanisa litaendelea kuimarisha uhusiano wa dhati na Serikali ili kwa pamoja kuweza kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: haki msingi za binadamu; huduma makini kwa maskini, wanyonge na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa litaendelea kuchangia ustawi na maendeleo ya wengi: kiroho na kimwili. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, Serikali itaweza kutia sahihi mkataba unaolitambua Kanisa na taasisi zake kisheria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.