2017-01-28 13:52:00

Jifunzeni kwa Papa Francisko juu ya utunzaji bora wa mazingira!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland kuanzia tarehe 29 Januari hadi tarehe 4 Februari 2017 linaadhimisha Juma la Shule za Kikatoliki kwa kuongozwa na kauli mbiu “Shule za Kikatoliki jifunzeni kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Hii ni changamoto inayoibuliwa kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira, uliotolewa kunako mwaka 2015.

Mama Kanisa anakumbusha kwamba katika kazi ya kuelimisha, familia zinamjenga mtu katika ukamilifu wa utu wake; katika upendo na mshikamano; kwa kurithisha tunu za kiutamaduni, kimaadili, kijamii, kiroho na kidini kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Elimu inayotolewa na taasisi zinazoongozwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki zinapania pamoja na mambo mengine kuwajengea wanafunzi kanuni maadili, utu wema; uaminifu na uzuri; huduma, umoja, upendo na mshikamano wa kidugu. Kumbe, wazazi ni walimu wa kwanza wa watoto wao, dhamana inayotekelezwa na Serikali pamoja na wadau mbali mbali kama vile Kanisa! Maadhimisho ya Juma la Shule Katoliki Ireland ni kuiwezesha familia ya Mungu nchini humo kutambua na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Kanisa Mahalia katika sekta ya elimu kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Juma hili linafunguliwa rasmi, Jumapili tarehe 29 Januari 2017 kwa Ibada ya Misa Takatifu inayongozwa na Askofu Denis Nulty wa Jimbo Katoliki Kildare e Leghlin na kuhudhuriwa na wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali za Ireland.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.