2017-01-28 14:29:00

Heri za Mlimani zinavyochambuliwa kama karanga!


Jambo muhimu analoliwania binadamu hapa duniani ni kuwa na furaha. Hali ya kutaka furaha imewekwa na Mungu ndani ya kila mmoja wetu. Yabidi daima kujiuliza maana ya maana yetu. Lakini mara nyingi swali hilo linaweza kusahauliwa kutokana na furaha nyingi za muda za hapa duniani.Katika Injili ya leo Yesu anatufundisha kwa njia ya heri nane jinsi ya kuyafanya maisha yetu kuwa na maana na kutuletea furaha inayodumu. Yesu anatuletea picha ya mtu aliyefanikiwa kuyapa maana maisha yake. Mtu huyo anapongezwa na kuambiwa ameulamba! Amefaulu, ameweza, amevuka, ameula, amefanikiwa, amebahatika ni Mwenye heri. Ukweli wa mambo, pongezi na hongera hizi zinamhusu Yesu wa Nazareti kufaulu katika maisha. Kabla ya kuzisikia pongezi hizo tuyaone kwanza mazingira zilipotolewa.

Heri hizi zilitolewa mlimani.“Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani.” Kadiri ya mapokeo mlima huo ni ule mwinuko uliojitokeza sana Kapernaumu. Lakini kidhati mlima unaosemwa hapa na Mwinjili Mathayo siyo wa kijiografia unaoonekana kwa macho, bali ni mlima wa kiteolojia. Kadiri ya fikra za watu wa Mashariki mlima ulikuwa ni makao ya miungu, kama Afrika, baadhi ya makabila wanatambika chini ya mlima. Kumbe, kwa Wayahudi mlimani ni mahali  pa kukutana na kusikiliza neno la Mungu na kujua anakichotaka. Kwa hiyo kupanda mlimani ni kuachana na mambo ya bondeni wanakoishi watu na wanakomwona mtu aliyefanikiwa kadiri ya fikra zao. Lakini kupanda mlimani maana yake kuangalia mambo kwa fikra za kimungu. Kwa hiyo kuna fikra aina mbili. Mosi, kadiri ya maisha ya watu wa bondeni, na pili kadiri ya Mungu aliye mlimani. Lakini isieleweke kwamba wale waliokwea mlimani na wanaofikiri kadiri ya Mungu hawawezi tena wakafikiri kiulimwengu. Hebu sasa tuone pongezi anazomwagia Yesu mtu aliyefaulu na ahadi zake.

Mosi, “Heri walio maskini wa roho  maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Tunaposikia umaskini tunaelewa mara moja kukosa makazi, wakimbizi, wasio na nguo nk. Kumbe heri hii haiwahusu kabisa watu aina hii. Aidha wengine wanafikiri heri maana yake kutoa mali na kuwasaidia maskini. Kumbe Yesu anasema maskini wa roho maana yake ni nguvu (roho) aliyoitoa Mungu kwa waana wake inayotusukuma kuwa maskini. Watu walio na fikra za bondeni wanajiona kuwa ni wamiliki wa mali ya ulimwengu huu. Kumbe mali yote ni ya Mungu kama isemavyo Zaburi: “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake.” (Zaburi 24). Kama Mungu ni mmiliki wa mali yote basi binadamu ni mtunzaji tu, hivi yabidi kumtolea hesabu mali yake. Kumbe tukitumia mali kadiri ya mpango wake, hapo ulimwengu utakuwa paradisi. Kwa hiyo mwenye heri ni yule anayekabidhi mali yote kwa mmiliki.

Pili, “Heri wenye huzuni, maana hao watafarijika.” Mara nyingi heri hii inafasiriwa vibaya hasa pale tunapompa pole mgonjwa tunamwambia: “mtolee Mungu mateso yako. Unganisha mateso yako na ya Kristu!” Lugha hii ni nuksi kwa mgonjwa, kwa hoja kwamba Mungu hahitaji kabisa mateso yetu na wala havumilii kuona tunateseka na kuhuzunika. Mwinjili Luka anasema: “heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka – mtatulizwa.” (Lk. 6:21). Neno la kigiriki lililotumika hapa la huzuni ni penthountes maana yake ni uchungu ule mkali sana anaoupata mtu aliyefiwa mzazi, au mtoto au ndugu yake mpendwa sana. Unaweza pia kusema: “Heri waliovunjika moyo, heri wanaolia.” Ama kweli, hata Yesu alilia mara mbili. Mosi, alilia mbele ya kaburi la Lazaro. Hapo alionesha jinsi alivyokuwa karibu na mpendwa wake aliyempoteza.

Pili, Yesu aliangua kilio baada ya kuutafakari mji wa Yerusalemu. Aliulilia mji ule kwa sababu aliupenda sana pamoja na watu wake. Lakini kwa bahati mbaya watu hao waliamua kuchukua maamuzi ya kufuata mambo yatakayoupeleka kwenye maangamizo. Ingawaje kwa upande wake amejaribu alivyoweza kutoa mapendekezo mapya ili kuusevu mji huo lakini watu walichagua tofauti. Ni sawa na nchi mbili zinazokataa kufanya mazngumzo ya amani na kuamua kupigana vita. Kwa hiyo mwenye huzuni, ni yule aliye na upendo wa hali ya juu kwa ulimwengu mpya hadi kulia anapoona kwamba watu wamekosea kuchagua. Tujihoji kama sisi tunaupenda ulimwengu mpya alioupendekeza Kristo kiasi cha kuangua kilio tunapoona kuwa ulimwengu umeamua kufanya mambo kinyume, kama vile vita, uonezi, kukoseana haki. Ahadi anayotoa Yesu ni kwamba wanaolia kutokana na upendo wa aina hiyo watafarijika. Maana yake Mungu mwenyewe ndiye atakayewatuliza na kuwachekesha, yaani hawatakatishwa tamaa kwa sababu siku moja ulimwengu utakuja kung’amua mapato mazuri ya upendo, kwa sababu Mungu yuko upande wa wale walio na upendo kama huo.

Tatu, “Heri wenye upole, maana hao watairithi nchi.” Heri hii pia inafasiriwa vibaya, kwa sababu kwetu wapole ni wale watulivu, wasiokasirika wanapochokozwa, wasiohoji mambo, wasionung’unika wanapokosewa haki. Heri hii hapa baada ya ile ya huzuni, yaani ya yule anayelia kwa vile anaupenda sana ulimwengu mpya na mapendekezo ya Yesu, lakini anashindwa kuutangazia ulimwengu kwa vile umekithiri ukatili na ubaya. Yesu mwenyewe ni mpole na mnyenyekevu wa moyo lakini alipambana na upinzani hasa dhidi ya mfumo mbovu wa kidini. Kwa hiyo, mpole ni yule ambaye mbele ya madhulumu, ukatili na uovu hageuki kuwa mbaya na kufanya tena uovu. Hali ya mtu mpole ni mapato ya nguvu ya Roho Mtakatifu. Mpole hataki kubadili maisha ya mwingine bali anampenda. Ahadi inayotolewa kwa mpole ni “kurithi nchi.” Hii siyo nchi ya kiyakinifu, bali ni ulimwengu mpya ambao Kristu anauahidi kwa vile Mungu yuko upande wa mpole.

Nne, “Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa.” Chakula na maji ni mahitaji muhimu ya maisha. Heri hii haimaanishi njaa na kiu ya chakula na maji ya kawaida bali haki. Aidha haki siyo ile ya kulipa ovu kwa mwovu, au falsafa ya jino kwa jino mtageuka wote kuwa vobogoyo! Bali ni haki  mpya ya Mungu ambayo ni upendo. Kwa hiyo kuwa na njaa na kiu ya haki maana yake kutamani sana haki ya Mungu ambayo ni upendo na amani itawale ulimwenguni. Ahadi anayotoa Yesu ni “Kushibishwa au kutosheka kabisa.” Mtu ukiwa na njaa na kiu ya kujilisha haki yaani upendo utashibishwa na upendo kwani Mungu ndiye huo upendo.

Tano “Heri wenye rehema, maana hao watapa rehema.” Tunaelewa rehema  au huruma maana yake kusamehe au kuwa na huruma. Tunapenda kusamehe ili nasi tuweze kusamehewa. “Utusamehe makosa yetu kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea.” Tafsiri hii ya rehema ni rahisi sana na wala haina uhusiano na heri hii. Tukitaka kuielewa vizuri budi tuanze kujitambua kuwa sisi ni watoto wa Mungu. Kama Mungu ni mwenye rehema yabidi nasi tufanane naye. Mungu ni Rehema kama inavyosema Agano la kale: “Mimi ninampenda binadamu kama mama anavyompenda mwanaye aliye ndani ya tumbo lake.” Mungu anapenda bila mipaka, wala masherti. Kwa hiyo mwenye rehema anapenda kama Mungu bila mipaka wala masherti. Heri yao watu hao kwani wamepata mfano wa jinsi ya kuwa na rehema. Mungu anawapongeza kwani wanafanana naye aliye na rehema.

Sita, “Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu.” Kadiri ya biblia moyo ni makao ya maamuzi ya hekima na ufahamu. Yesu anapomponya aliyepooza anawahoji Wafarisayo: “Kwa sababu gani mnawaza hivi mioyoni mwenu.” Moyo safi ni ule unaoongozwa na Mungu katika kufanya maamuzi yake bila kuathirika na miungu mingine. Mwenye moyo safi namna hii anamwona Mungu, yaani anaweza kuona zaidi ya kile wanachoona wengine.

Saba, “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Maana nyingine inasema: “Heri wenye kuleta amani,” yaani wasiotaka ugomvi. Neno la kupatanisha la Kigiriki ni eirEnopoioi kutoka maneno mawili: eirene na poione maana yake kufanya amani, kutengeneza amani. Mtu anayepatanisha familia, au mataifa yanayogombana hapa ulimwenguni ndiye mwenye heri. Lakini amani inayozungumzwa hapa ni zaidi kwani shalom au amani kwa kiebrania maana yake maisha yaliyojaa furaha. Kwa hiyo mtu anayewapa wengine furaha, huyo ameshinda na amebarikiwa. Ahadi wanayopewa watu hao ni kuitwa watoto wa Mungu. Ni furaha iliyoje kuitwa na Mungu: “wewe ni mtoto wangu.”

Nane. “Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao.”Anayepokea ulimwengu mpya wa Yesu, hatashabikiwa kamwe na wale wanaotaka kuendeleza ulimwengu wa kale. Hivi mkristu asitegemee kushabikiwa na ulimwengu wa kale. Ukishabikiwa inamaanisha upo bado katika ulimwengu huo. Ahadi anayopewa mtu anayeudhiwa kwa ajili ya upendo, ni ufalme wa mbinguni. Hivi madhulumu ni kama alama inayoonesha kwamba mtu hausiki na mambo ya ulimwengu wa kale bali ulimwengu mpya ambao Mungu ataudhihirisha. Heri yako wewe unayepokea mapendekezo haya nane ya Kristo na kuyaishi.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.