2017-01-27 14:48:00

Papa Francisko asikitishwa na ajali ya Bus la wanafunzi!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda Kardinali Peter Erdo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria, anapenda kutoa salam zake za rambi rambi kutokana na ajali ya Bus iliyotokea huko Verona, tarehe 20 Januari 2017 na kusababisha wanafunzi 16 kufariki dunia na wengine 26 kujeruhiwa vibaya wakiwa njiani kutoka Ufaransa kuelekea Hungaria.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia mshikamano na uwepo wake wa karibu wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito. Kwa wale waliofariki dunia, Baba Mtakatifu anawaombea huruma  ili waweze kupumzika kwa amani na wale waliopata majeraha wapate faraja na kuimarishwa na huruma ya Mungu, ili hatimaye, waweze kupona na kurejea tena kuendelea na shughuli zao. Wakati huo huo, Serikali ya Hungaria tarehe 23 Januari 2017 ilitangaza kuwa ni Siku ya Maombolezo Kitaifa kutokana na msiba huu mzito!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.