2017-01-27 10:44:00

Mageuzi ya mahusiano kati ya Maaskofu na Watawa yaanzie moyoni!


Kunako mwaka 1978, Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume baada ya mkutano wake wa mwaka uliochambua pia ushauri kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na Mashirika mbali mbali ya kitawa duniani lilichapisha Waraka unaojulikana kama “Mutuae relationes” yaani “Mahusiano kati ya Maaskofu na Watawa”. Ni Waraka uliojikita katika nyaraka zilizokuwa zimetangulia hapo awali yaani “Christus Domini” “Bwana Yesu Kristo” pamoja na “Perfectae caritatis” ”Mapendo kamili” zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili.

Waraka wa Mahusiano kati ya Maaskofu na Watawa unafafanua kuhusu mafundisho tanzu ya Kanisa mintarafu mahusiano kati ya Maaskofu na Watawa wanaoshiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa, yaani “Watu wapya” waliozaliwa kwa Roho Mtakatifu ambaye ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa; umoja, upendo na mshikamano. Kwa pamoja wanaitwa na Mama Kanisa kuwa ni Sakramenti ya wokovu, yaani alama wazi ya wokovu katika: umoja, utakatifu na utume. Waraka unabainisha utume wa Maaskofu Mahalia kama nguzo msingi katika kudumisha umoja wa watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, Kristo ni kichwa cha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Maaskofu na watawa wanategemeana na kukamilishana katika maisha na utume wao.

Waraka wa Mahusiano kati ya Maaskofu na Watawa unaendelea kufafanua kwamba madaraka ya Maaskofu ni: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Maaskofu na watawa wanatekeleza utume wa watu wa Mungu unaobubujika kutoka katika kisima cha upendo na muungano wa dhati na Mwenyezi Mungu katika utekelezaji wa dhamana, utume na shughuli za kichungaji zinazofanywa na watawa. Maaskofu na wakuu wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume wanapaswa kushirikiana na kushikamana katika malezi awali na endelevu kwa watawa sanjari na kuwa na utaratibu mzuri wa kusimamia shughuli za kichungaji katika ngazi mbali mbali.

Ni katika mwelekeo, huu Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwa msukumo wa Baba Mtakatifu Francisko linapitia upya Waraka wa mahusiano kati ya Maaskofu na Watawa kwa kuzingatia “Taalimungu ya umoja, umuhimu wa karama ya kihierarkia pamoja na karama mbali mbali za mashirika ya kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa. Kazi hii anasema Askofu mkuu Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume inayashirikisha Mabaraza ya Kipapa ili kwa pamoja kuweza kufanya mageuzi yanayojikita katika moyo wa waamini.

Taalimungu ya umoja ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kwamba,  kiini na umuhimu wa kihierarkia umefafanuliwa kwa kina na mapana katika Waraka uliotolewa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, “Iuvenescit Ecclesia” “Upyaisho wa Kanisa” unaoonesha umuhimu wa karama za kihierarkia zinazotolewa kwa njia ya Daraja Takatifu na pili ni karama zinazotolewa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa la Kristo; ambazo zinapaswa kusaidia kukuza na kukoleza umoja na amani katika utekelezaji wa utume na maisha ya Kanisa: kwa kufikiri, kupanga, kutekeleza na kutathmini utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa, kwa kuheshimiana na kukamilishana.

Tunu msingi za umoja wa Kanisa zimefafanuliwa kwa kina na mapana katika Wosia wa Kitume “Vita Consacrata” “Maisha ya Wakfu” unaoonesha kwamba, Kanisa linajikita katika: Umoja, hierarkia na karama mambo yanayosababisha mahusiano kati ya Maaskofu, watawa na waamini walei. Kumbe, Kanisa linataka kuendeleza tasaufi ya umoja matunda makubwa ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kwamba, hapa hakuna ukinzani wala mpasuko. Uelewa makini wa kitaalimungu unaweza kuisaidia familia ya Mungu kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa.

Askofu mkuu Rodriguez Carballo anashauri kwamba, taalimungu ya maisha na historia ya kitawa  vinapaswa kuwa ni sehemu ya masomo na majiundo ya kitaalimungu kwa majando kasisi, wanaojiandaa kupokea Daraja Takatifu. Hawa ni watu ambao baadaye watakuwa ni viongozi wa Kanisa, waweze kutambua na kuthamini uwepo na huduma ya watawa katika maisha na utume wa Kanisa. Katika kipindi cha takribani miaka 40 Waraka wa mahusiano kati Maaskofu na Watawa haujamwilisha vyema katika maisha ya utume wa Kanisa. Hapa kuna haja ya kuanzisha mchakato wa mageuzi yanayojikita katika moyo wa mtu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Lengo ni kujenga na kudumisha utamaduni wa Maaskofu na watawa kukutana na kujadiliana kwa kina na mapana mintarafu hali halisi ya maisha ya Kanisa Mahalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.