2017-01-26 08:54:00

Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana 2018: Moto wa kuotea mbali!


Vijana wanapaswa kutoka katika ubinafsi wao badala ya kuwa ni watazamaji na watu wanaoshangaa nje ya maisha na utume wa Kanisa, kuanza kuzama ndani kabisa katika maisha na utume wa Kanisa kwani wao ni chachu kubwa ya maendeleo kiroho na kimwili. Vijana wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Uinjilishaji wa kina kati ya vijana wenzao kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia!

Vijana wanapaswa kutumia vyema karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao kiroho na kimwili! Vijana wasomi na wafanyakazi wasisite “kujichanganya” na vijana wenzao Parokiani iuli kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kiutu, kiroho na kijamii, kwani sasa umefika wakati wa kuwa kweli ni wadau wakuu katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Elvis do Ceu e Federica Ceci vijana wasomi kutoka Roma, walioshiriki kikamilifu katika uzinduzi wa Hati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya XV ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu“Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hii inaonesha dhamira ya Kanisa kutaka kuwasikiliza vijana kwa dhati kabisa!

Vijana hawa wametumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa hakika amekuwa ni Baba mwema kwa vijana kwa kuamua kuitisha Sinodi ya Maaskofu itakayojadili na kupembua maisha, utume, changamoto za vijana wa kizazi kipya katika mwanga wa Injili ya Kristo! Baba Mtakatifu kwa nyakati mbali mbali amegusia changamoto za maisha ya vijana hususan: ukosefu wa fursa za ajira, umuhimu wa imani katika maisha ya ujana pamoja na mang’amuzi yao kuhusu miito.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia waligusia changamoto za maisha ya ujana katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai, sasa ni wakati muafaka kwa Mababa wa Sinodi kutafakari kwa kina na mapana kuhusu maisha ya vijana wa kizazi kipya, kama kielelezo cha Kanisa linatoka ili kukutana, kujadiliana na kuambatana na vijana katika hija ya maisha yao hapa duniani katika mwanga wa Injili! Vijana wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwaandikia vijana barua kama mwanzo wa mchakato wa maandalizi ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018. Kwa hakika anawawasaidia vijana kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa; yaani viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Baba Mtakatifu anaonesha imani, matumaini na mapendo, yanayoweza kuwasaidia vijana kuwa ni wajenzi na mashuhuda hodari wa Kanisa; kwa kuonesha ukarimu na upendo; Kanisa daima likijitahidi kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, binadamu na mahitaji yake msingi, akipewa kipaumbele cha kwanza! Vijana wana matumaini makubwa kwamba, Maaskofu mahalia sehemu mbali mbali za dunia watawasikiliza kwa makini, tayari kuwaendea vijana ambao kwa miaka mingi wamesahau mahali ulipo mlango wa Kanisa, ili nao pia waweze kuonja furaha ya Injili kwa kukutana tena na Kristo Yesu kwa njia ya mikakati makini ya maisha na utume wa Mama Kanisa kwa vijana.

Vijana wanawataka Maaskofu kupoteza muda kwa kuzungumza na kuwasikiliza vijana ili kwa pamoja waweze kushikamana katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kristo Yesu; Kanisa ambalo ni kijana lenye malango wazi, tayari kukutana na vijana katika ukweli na uwazi! Kimsingi vijana wengi wanakiri kwamba, katika uhalisia wa maisha yao, wanatambua uzuri wa kuwa Mkristo wanataka kuwashirikisha vijana wenzao furaha, amani na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, ili kweli ulimwengu wa vijana uweze kuguswa na chachu ya furaha ya Injili, familia, haki na amani.

Vijana wanavitaka vyombo vya mawasiliano ya jamii kutoa kipaumbele cha pekee kwa maisha na utume wa vijana, kwa kukazia: Uzuri, utakatifu na mchango endelevu wa vijana katika maisha ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Vijana wanatambua kwamba, wanasumbuliwa sana na madhaifu, changamoto na kinzani kibao, lakini sasa wanataka kuwa kweli ni wadau kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kuwa ni vyombo vya ujenzi wa utamaduni wa upendo na mashuhuda wa furaha ya Injili ya familia, haki na amani; kwa kutumia karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.