2017-01-25 08:40:00

Papa Francisko: tangazeni na kushuhudia matumaini na kuaminiana


Siku ya 51 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni itaadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 28 Mei 2017, Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni kwa kuongozwa na kauli mbiu “Usiogope, maana mimi ni pamoja nawe” Is. 43:5: Kutangaza Matumaini na Kuaminiana katika nyakati zetu”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu, anawaalika wadau mbali mbali katika sekta ya mawasiliano ya jamii kuvunjilia mbali mnyororo wa habari za “udaku” na kuanza kutoa nafasi kwa habari njema.

Wafanyakazi katika vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa kwa namna ya pekee wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya uhai wa Injili na habari njema inayowaangazia watu katika medani mbali mbali za maisha, hata katika hali tete zinazomkabili mwanadamu katika ulimwengu mamboleo! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kujikita katika kutangaza habari njema; kuwa na imani katika Ufalme wa Mungu pamoja na matumaini kwa Roho Mtakatifu anayewawezesha kuwa kweli ni vyombo, mashuhuda na watangazaji wa ubinadamu mpya, uliokombolewa hadi miisho ya dunia.

Baba Mtakatifu anawataka wadau wa vyombo vya mawasiliano ya jamii kuwa ni watangazaji wa mawasiliano yanayojenga kwa kuthamini utu na heshima ya wengine, ili hatimaye, kukataa kishawishi cha kuwa na maamuzi mbele wakati wa kutekeleza dhamana na majukumu ya mawasiliano ya jamii. Lengo ni kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana kwa kuvunjilia mbali mnyororo wa mateso na mahangaiko ya watu kutokana na habari za “udaku na fitina” zinazopikwa kila kukicha katika vyombo na mitandao ya mawasiliano ya kijamii. Ni dhamana na wajibu wa wanahabari kuhakikisha kamba, kweli wanawasaidia wateja wao kupata habari nzuri na zinazowajenga: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anawahimiza wafanyakazi na wadau katika sekta ya mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba, wanaondokana na mnyororo wa hofu ambayo ni matunda ya habari za udaku na uchochezi kwa kukazia mambo msingi juu ya mateso na mahangaiko ya binadamu, kiasi hata cha kugusa kashfa ya ubaya unaomwandama mwanadamu. Hapa wanahabari wanapaswa kuvuka kuta za kukata na kujikatia tamaa na kuanza kujielekeza katika mchakato wa utayarishaji wa habari njema yenye mvuto na mashiko, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu kwa kuwa makini na mateso pamoja na mahangaiko ya watu; mambo ambayo wakati mwingine yanatumiwa kwenye vyombo vya habari kiasi cha kusahau Fumbo la mateso na mahangaiko ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawahamasisha wanahabari kuhakikisha kwamba, wanajielekeza katika mchakato wa mawasiliano ambayo yanajikita katika kipaji cha ugunduzi; ukweli na uwazi, ili kuwasaidia watu kupata suluhu ya changamoto na matatizo yanayowaandama kwa kuwajengea dhana ya uwajibikaji watumiaji wa njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii. Umefika wakati wa kuwapatia watu wa nyakati hizi habari njema zinazojikita katika uzuri wa habari bila kificho. Hali hii inategemea kwa kiasi kikubwa miwani inayotumiwa kutazama na kuipokea habari husika.

Baba Mtakatifu anasema, Injili ni habari njema juu ya Kristo Yesu, inayopaswa kuwa ni kiini na msingi wa upashanaji habari duniani. Kristo Yesu mwenyewe aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na hivyo kumwezesha Mwenyezi Mungu kuanzisha mchakato wa mshikamano na binadamu mdhambi, ambaye Mwenyezi Mungu anapenda kumwambia hata leo hii kwa maneno ya Nabii Isaya ”Usiogope, maana mimi ni pamoja nawe”. Maneno ya Mungu yanayofumbata faraja ya Mungu katika historia ya watu wake, chemchemi ya matumaini ya uwezekano wa kuwa na habari njema, kwa kuruhusu upendo kupenya katika maisha ya jirani.

Baba Mtakatifu anawataka wadau mbali mbali katika tasnia ya habari kujivika fadhila ya unyenyekevu wa Ufalme wa Mungu kama alivyokuwa anafanya Kristo kwa njia ya mifano yake. Hata leo hii ushuhuda wa Habari Njema ya Kristo Yesu inayowilishwa katika matendo una mvuto zaidi katika maisha ya watu, kuliko maneno matupu ambayo kamwe hayawezi kuvunja mfupa! Baba Mtakatifu anaendelea kuwasihi wadau wa vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kuwa na imani katika mbegu ya Ufalme wa Mungu sanjari na mantiki ya Fumbo la Pasaka linalowawezesha wadau wa mawasiliano ya jamii kupambanua uwepo wa habari njema katika ukweli wa kila historia ya maisha ya kila mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya 51 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa kukazia kwamba, hata leo hii, Roho Mtakatifu anaendelea kupandikiza mbegu ya hamu ya Ufalme wa Mungu kwa kutumia vyombo hai, yaani, binadamu kwa kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu anayewaongoza kwenye kiini cha Habari Njema, katika majanga ya historia, kiasi cha kuwawezesha kuwa ni mwanga katika giza la dunia. Huu ni mwanga anasema Baba Mtakatifu unaoangazia mapambano ili hatimaye, kuwa na imani pamoja na matumaini mapya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.