2017-01-25 15:06:00

Heri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo!


Mtakatifu Jerome anasema ni tajiri wa kutosha yule aliye maskini katika Kristo. Ushuhuda huu ni mkubwa sana kwani Kristo ndiye mwana mrithi wa Mungu aliye Muumba wa yote na yule amfuataye Kristo atapata yote yaliyo yake Mungu. Mwandishi mmoja Anon anasema kama huna au huwezi kuwa na kila kitu, basi tumia vizuri kile ulichonacho. Fundisho fupi na lenye maana kubwa. Mungu ametuumba kwa mfano na sura yake. Sisi ni warithi pamoja na Mwanae. Hakuna heri kubwa zaidi ya nafasi hii aliyotujalia Mungu kwa njia ya Mwanaye.

Ndugu zangu dhana ya heri/utajiri/mali/furaha na/au umaskini inaweza ikapata maana na sura mbalimbali pengine kadiri ya mila, desturi, mahali na wakati na pengine mahitaji ya watu. Padre Jack alikuwa Padre mmisionari aliyefanya utume wake kati ya Wasukuma. Anasema wazi kuwa hakujisikia vizuri katika parokia yake kwani alijiona kuwa na vitu vingi kama umeme jua, tenki la maji, nyumba ya bati n.k. Siku moja alimshirikisha katekista Charles kuhusu alivyojisikia. Yeye alijiona akiishi kama tajiri miongoni mwa watu maskini. Hata hivyo jibu la Katekista Charles lilimshangaza sana. Katekista Charles alimshirikisha Padre jinsi watu wanavyomuona pale kijijini. Katekista alimwambia kuwa kati yao pale kijijini, yeye padre ni maskini zaidi  kwani hana watoto wala wajukuu.

Mtazamo huu unaweza pia kugusa uelewa wetu juu ya utajiri na umaskini wa kiroho. Katika injili tunasikia juu ya heri, heri maskini wa  roho – Mt. 5:1. Tukisoma mahali pengine katika injili tunasikia habari ya jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia mbinguni – Mt. 19:16-30. Je utajiri na umaskini wa kweli ni upi? Biblia yatuambia nini? Jibu la kibiblia kuhusu utajiri wa kweli liko wazi. Tajiri wa kweli na mwingi wa fadhila ni Mungu Baba peke yake. Yote tuliyo nayo yatoka kwake na ni mali yake.

Tendo la uponyaji katika Mdo. 3:1-10 laweza kutupa jibu na mwongozo juu ya kitu au namna gani tunaweza kuomba na kutupatia heri ya kweli. Yule kiwete alimwona Petro na Yohani wakiingia hekaluni na anawaomba pesa. Alitegemea kupata kitu kutoka kwao. Petro anamwambia wazi hana dhahabu wala almasi. Ila kwa jina la Yesu wa Nazarethi anamwamuru atembee. Hii ikawa heri yake mpya na yenye kudumu. Hii ndiyo heri ya kweli.  Sisi waamini tunatambua kuwa ufalme wa Mungu haununuliwi kwa fedha wala dhahabu. Sisi hatukukombolewa kwa fedha wala dhahabu bali kwa damu yake Kristo.

 Kutoka Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika kipengele ‘Ufunuo’  tunaambiwa kuwa Mungu, mwanzo na mwisho wa yote, aweza kufahamika kwetu kwa njia ya viumbe tukitumia mwanga wa akili ya mwanadamu. Hakika fundisho hili lamtaka mwanadamu kuutambua ukuu wa Mungu na uweza wake. Hakika yule anayefahamu hilo basi katika maisha yake atakiwa kumchagua Mungu. Kwa kutumia akili aliyojaliwa na yenye uwezo wa kujua na kufahamu basi anaweza kumchagua huyo ambaye ni asili na chanzo cha utajiri wote na heri ya kweli.

Furaha ya kweli kama anavyotaka Yesu ni ile ya kuurithi uzima wa milele. Neno lingine mbadala wa furaha ya kweli na inayodumu ni heri. Ni hali ya kimbingu ambayo ulimwengu hauwezi kutoa. Hii hupatikana tu kama tukipata fadhila za kimbingu. Hizi heri katika injili ya leo ni mwongozo wa kufika mbinguni.  Kila mtu anatafuta au kutaka kupata furaha. Ila njia ziko tofauti. Kwa uhakika ulimwengu una majibu tofauti kuhusu furaha ni kitu gani. Pale Yesu asemapo heri maskini wa roho, ulimwengu ungesema heri walio tajiri n.k. Kama ingeundwa kamati kulinganisha kati ya heri zake Yesu na heri za ulimwengu tungepata majibu ya ajabu na yanayotofautiana kabisa.

Croesus, 590 KK, mfalme wa Lydia alikuwa na utajiri mwingi na aliishi maisha ya ufahari. Alijaza nyumba yake na vitu vya kifahari. Aliamini kuwa yeye ni mtu mwenye furaha kuliko binadamu wote. Siku moja alitembelewa na Solon, ambaye alikuwa mmoja wa watu saba wenye hekima huko Ugiriki. Croesus alimpokea kwenye moja ya vyumba vyake vya kifahari. Solon hakuonesha kushangaa wala kuvutwa na utajiri alioona pale. Mfalme akiwa amekasirishwa na ubaridi wa Solon alimwuliza kwa ukali kwa nini hasemi cho chote kuhusu ufahari wake na kwa nini hamwoni yeye kuwa mtu mwenye furaha kuliko watu wote. Soloni akajibu, hakuna aliye na furaha ya kweli isipokuwa yule ambaye furaha yake iko kwake Mungu.

Katika maandiko matakatifu Agano la Kale Mhubiri 1:2 anasema ni ubatili mtupu. Mwandishi mmoja anasema ‘fedha yaweza kununua kila kitu isipokuwa furaha, kulipa gharama zako zote, isipokuwa mbingu’. Kwa hakika Yesu anajua kuwa tuko ulimwenguni. Hasemi tuachane na ulimwengu ila anatuambia tumtangulize Mungu kwanza katika kuishi na kuenenda katika ulimwengu. Anatudai tumweke Mungu mbele kwani kwake hupatikana heri na amani ya kweli. Mtakatifu Augustino anasema mioyo yetu haitatulia mpaka itakapompata Mungu.  Tunaambiwa kuwa ili kukamilika na kuzipata heri hizi hatuna budi kuziishi katika ujumla wake. Swali laweza kuwa Je, tunaishi maisha tukifuata mitindo ya ulimwengu ili kupata furaha au tunaishi kadiri ya mafundisho ya Yesu ili kupata heri kamili?

Mwanafalsafa Aristotle anasema watu wote hutafuta furaha. Ila anasisitiza kuwa mtu wa maadili mema ni yule anayejua na kutenda kile kimleteacho siyo tu furaha, starehe au vionjo vya muda bali kile kiletacho furaha ya kweli na inayodumu.

Tumsifu Yesu Kristo

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.