2017-01-23 14:10:00

Wakristo wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho!


Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo; maadhimisho ambayo kwa Mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “Upatanisho: upendo wa Kristo unatuwajibisha”. Wakristo wakitumia vyema neema na baraka inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanaweza kufanikisha mchakato wa umoja wa Wakristo duniani kwa kusimama kidete ili kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ambayo kwa sasa inaonekana kushika kasi kubwa katika maisha ya watu wengi duniani!

Huu ni ushauri unaotolewa na Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani wakati huu wakristo wanapoungana kwa ajili ya kuombea umoja sanjari na mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Itakumbukwa, vitini vya sala na tafakari za Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo vimeandaliwa na Wajumbe wa Makanisa ya Kikristo kutoka Ujerumani, kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo sanjari na Baraza la Makanisa Ulimwenguni.

Dr. Junge, anakaza kusema, tema ya upatanisho inayoongoza maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo litakalohitimishwa, hapo tarehe 25 Januari 2017 kwa Sherehe ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa inakwenda sanjari na malengo yaliyotolewa na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani pamoja na Kanisa Katoliki la kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene kutoka katika kinzani na kuanza kujikita zaidi na zaidi katika upatanisho na umoja wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, kuna mambo mengi msingi yanayowaunganisha Wakristo pengine kuliko hata yale yanayowagawa! Ni wakati wa kushukuru, kuomba msamaha kutokana na dhambi ya utengano pamoja na kuendelea kuwa na matumaini ya mwendelezo wa mchakato wa kiekumene unaofumbatwa katika: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezni mwa jamii!

Kwa upande wake, Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikan duniani anasema, kuna haja kwa Wakristo kutakasa kumbu kumbu zao, tayari kuanza mchakato wa kuombana msamaha. Askofu mkuu John Sentamu wa Kanisa Anglikan, Jimbo kuu la New York, Marekani anasema, Mageuzi ya Kiluteri Duniani yalikuwa ni chachu ya kulipyaisha Kanisa, lakini pia yamekuwa ni chanzo cha kugawanyika na kusambaratika kwa Kanisa la Kristo. Katika mwelekeo huu, Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani iwe ni fursa ya kuomba msamaha kutokana na kusababisha utengano ndani ya Kanisa. Mchakato huu uwasaidie Wakristo kutoka Makanisa mbali mbali kukutana na kusali pamoja!

Na Padre Richard Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.