2017-01-23 14:50:00

Dr. Buzzonetti aliyewahudumia Mapapa wanne amefariki dunia!


Dokta Renato Buzzonetti ambaye tangu mwaka 1978 alikuwa ni daktari binafsi wa Mtakatifu Yohane Paulo II kwa muda wa miaka ishirini na sita na baadaye daktari binafsi wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa muda wa miaka minne, amefariki dunia, usiku wa kuamkia tarehe 21 Januari 2017 akiwa na umri wa miaka 92. Lakini, itakumbukwa kwamba, aliwahi pia kuwa ni daktari msaidizi wa Mwenyeheri Paulo VI na Papa Yohane Paulo I kwa kipindi kifupi cha maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Hayati Dokta Renato Buzzonetti alizaliwa tarehe 23 Agosti 1924 mjini Roma, baada ya kazi ngumu na nyeti ya kuwahudumia viongozi wakuu wa Kanisa, kunako mwaka 2009 aling’atuka katika huduma na kutunukiwa nishani ya huduma iliyotukuka kutoka kwa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Akihojiwa na radio Vatican kuhusu Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na uhusiano wake na Fumbo la mahangaiko ya mwanadamu katika ugonjwa alisikika akisema, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni shuhuda wa imani katika mateso na mahangaiko ya mwanadamu, si haba kwamba, aliweza kushuhudia yale aliyokuwa yanamgusa kutoka katika undani wa maisha yake katika Waraka wake wa Kitume, “Mateso yanayookoa” “Salvific dolores”.

Madaktari ni watu ambao kwa taaluma yao wamebahatika kuwasindikiza wagonjwa wao kutoka katika dunia hii na kuingia katika usingizi wa amani na maisha ya uzima wa milele, mahali ambapo wanakumbana na Fumbo la Kifo na uwepo wa Mungu anayedhihirisha nguvu yake na mwanadamu anayeonesha udhaifu wake mbele ya Fumbo la Kifo. Mtakatifu Yohane Paulo II ni kiongozi ambaye Fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo vilikuwa daima mbele ya macho na akili yake. Dokta Buzzonetti anakaza kusema, kushuhudia kifo cha Khalifa wa Mtakatifu Petro si haba, yataka moyo kweli kweli kwani huyu ndiye aliyekabidhiwa “Ufunguo wa mbingu na dunia”.

Daktari aliyeshuhudia kifo cha Yohane Paulo II ameshuhudia pia madonda na mateso yaliyomwandama katika historia, maisha na utume wake. Mtakatifu Yohane Paulo II ni kiongozi aliyeitupa dunia akiwa na siri kubwa moyoni mwake! Hii ni siri ya mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanayokoa na kukomboa, changamotokubwa hapa ni kuwapekelea wengine ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! Yohane Paulo II alikuwa ni mgonjwa aliyejitahidi kushirikiana vyema na madaktari wake, kwa kuwaelezea kwa kina mapana yale yaliyokuwa yanamsumbua mwilini mwake!

Yohane Paulo II ni mgonjwa alikuwa ni mgonjwa aliyetaka kuwasaidia madaktari wake kumpatia dawa ambayo ingeweza kumponya na hatimaye kurejea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kama ilivyo kwa wagonjwa wengi, Yohane Paulo II hakuwa ni mgonjwa ambaye hakupendelea sana kudungwa sindano, lakini kwa tiba nyingine zote, alionesha ushirikiano mkubwa haya ni mambo ya kawaida kabisa. Dokta Renato Buzzonetti anasema katika maisha na huduma yake kama daktari wa binadamu amepata changamoto kubwa ya kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa weledi mkubwa kwa kutambua kwamba, kila mgonjwa ana haki sawa kwani mbele yako unaweza kuwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini pia ukakutana na mgonjwa ambaye ni maskini na aliyesahulika, wote hawa wanapaswa kuheshimiwa na kuhudumiwa katika upendo, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, ni ndugu na jamaa zake Kristo Yesu.

Ikumbukwe kwamba, madaktari wa watu wanatoa huduma kwa watu, jambo kubwa ambalo amejifunza katika huduma kwa viongozi wakuu wa Kanisa. Hii ni huduma ambayo inapaswa kurutubishwa kwa imani thabiti, upendo na unyenyekevu mkuu! Huu ndio ushuhuda ambao amekutana nao katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II ambao unashuhudiwa katika sinema na kuandikwa kwenye vitabu mbali mbali, lakini zaidi, imani ambayo imechapwa katika akili na nyoyo za watu waliobahatika kukutana na Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Dr. Renato Buzzonetti, RIP. Amina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.