2017-01-21 18:23:00

Wakristo mnaitwa kuwa ni mashuhuda wa mwanga wa Kristo duniani!


Wapendwa taifa la Mungu, leo Mama Kanisa anatualika kutafakari pamoja naye tena neno lake la uzima. Kwa kifupi katika masomo yetu ya leo tunaona kuwa Nabii Isaya anaona mwanga mkubwa, Matayo anamtangaza Kristo kama huo mwanga mkubwa na Mtume Paulo anapambana na wale wanaotaka kuzima kuenea kwa mwanga huo sababu ya mipasuko kati yao. Nabii Isaya aliishi wakati wa mifarakano na vita katika nchi yake. Lakini pamoja na hayo alikuwa ni mtu wa matumaini makubwa. Kama tungeendelea mbele kidogo kusoma sehemu ya maandiko inayofuata baada ya somo hili la kwanza tungeona jinsi anavyoona kuzaliwa kwa mtoto mfalme.

Huyu mtoto ataleta ushindi na amani. Kadiri ya Isaya, historia ya kweli ni historia ya Mungu na huku kuzaliwa mtoto mfalme ndiyo uthibitisho wa historia ya kweli. Hata hivyo kile ambacho Isaya anakiona kwa mwanga hafifu, Matayo anakiona waziwazi. Yesu aliyeanzisha utume wake katika maeneo yanayotajwa na Nabii Isaya ndiye ule mwanga halisi na chanzo cha furaha iliyongojewa tangu zamani. Matayo hakuwa na wasiwasi kushuhudia hilo sababu ya mwanga wa kipasaka aliokuwa nao.

Ule utabiri wa ujio wa mtoto mfalme unakamilika wakati Yesu akiwa kazini akihubiri habari njema. Huku kuitwa kwa mitume katika somo la injili ya leo kwaonesha ukamilifu wa mpango wake wa ukombozi na utayari wake kumshirikisha mwanadamu. Tunaona kuwa huku kuitwa kwao kumewekwa katika hali ya kawaida kabisa. Yesu anawakuta katika mazingira yao, anawaita na wanaitika. Hatusikii mahojiano yo yote katika hili, yaani toka kwa waitwao wala kwa anayeita. Matayo alikuwa na lengo hapa. Kwa upande wa Yesu yaonesha ukuu wake na toka kwa walioitwa kwaonesha uaminifu wao na uthabiti katika imani. Na katika injili yote ya Matayo tunaona akisisitiza ukuu wa Kristo na utayari wa imani ya mitume/wafuasi.

Kanisa lasisitiza kuwa wito na jibu ni sehemu ya ukamilifu wa tangazo la kinabii la mwanga mkubwa na furaha kuu. Waitwao wanatumwa kutangaza habari njema kwa watu wote. Kama mwanga wa ulimwengu – Mat. 5:14, wanashiriki katika maisha ya mwanga mkuu, yaani Yesu Kristo. Wafuasi wanaitwa kuwa wavuvi wa watu.  Katika  Mat. 9:36-39 - tunasikia habari juu ya kilio cha Yesu kwa watu waliokuwa wanahitaji upendo wake – kondoo wasio na mchungaji. Hatuna budi kujiuliza ni kwa kiasi au namna gani sisi tunaotambua tayari mapenzi haya ya Mungu tunashiriki kikamilifu katika kueneza mwanga huu. Ndicho mtume Paulo anacholaani katika somo la pili, kwamba ufahamu duni waweza kusababisha mifarakano.

Ndugu zangu, hatuna budi kutambua kuwa Mungu huita kwa namna yake na kwa mpango maalumu bila kutegemea uelewa wa kibinadamu - 1Fal. 19:16,19-21; 2 - angalia jinsi nabii Eliya anavyomtupia Elisha vazi lake la kinabii ikimaanisha wito wake na jibu la Elisha kumtumikia Mungu. Elisha alikuwa katika shughuli zake. Hakutegemea kuitwa namna hiyo katika maisha yake. Kwa kupakwa mafuta, anakuwa mfuasi wa Eliya na mrithi wake. Na tangu siku hiyo maisha yake yanachukua mtindo mwingine kabisa. Mipango na harakati zake zote zinachukua mkondo mpya. Anamtumikia Mungu.

Injili ya Luka toka sura ya 9 na kuendelea yaonesha mwenendo mzima wa maisha ya utume wa Yesu, kwamba ni njia endelevu kwenda Yerusalemu, ambapo atapata mateso, kifo lakini pia ufufuko wake. Akiwa safarini anawafundisha wafuasi wake. Kwa ustadi mkubwa anawaita wafuasi wake na anawataka kuwa makini na wavumilivu. Pia anawakumbusha juu ya nguvu ya maamuzi – au kumfuata yeye au kumkataa. Anawaalika kuwa waangalifu na nguvu au vifungo binafsi, mali, familia na hali yo yote ile inayoweza kuzuia kumfuata. Anaonesha wazi kuwa ufalme wa Mungu una thamani kubwa zaidi kuliko hali zetu, chaguzi zetu na yote tuliyonayo au tutamaniyo kufanya.

Swali la kibinadamu laweza kuwa, je yawezekana kumfuata Bwana? Mtume Paulo katika Gal. 5:1,13-18  anasema kuwa ni roho ya Kristo inayotuita tuwe huru na inayotuwezesha kutoa jibu katika huo ufuasi. Wito wa ufuasi hautegemei kusikia sauti ya roho zetu bali twaitwa kusikiliza sauti ya roho yake Kristo. Maisha ya umisionari ya David Livingstone yaweza kutusaidia kuelewa namna ya kuitika na kuishi wito. Huyu alikuwa mmisionari, mvumbuzi na tabibu. Alifanya kazi na kufariki maeneo ya Afrika Mashariki na Kati. Stanley alisikia habari zake na alifunga safari toka Ulaya kumtafuta mtu huyu maarufu duniani. Walikutana Ujiji na tangu hapo Stanley akabaki naye. Stanley alishiriki utume wa Livingstone na maisha yake ya kila siku. Stanley hakuwa mkristo na anashuhudia mwenyewe jinsi Livingstone alivyotumia muda wake kuwasilikiliza watu na kuwatibu na kuwapa nafasi ya kutambua upendo wa Mungu. Namna hii ya utendaji ilitosha Stanley kuomba kubatizwa. Hakuhitaji kufundishwa katekisimu. Huu ni ushuhuda tosha wa maisha ya wito wa kikristo.

Ndugu wapendwa, tukumbuke kuwa hatuwi wakristo kwa hiari yetu bali ni neema ya Mungu inayofanya hilo liwezekane. Hata maendeleo ya ukristo wetu hayategemei nguvu zetu wenyewe. Ni upendo wa Mungu unaotujalia nguvu. Ni uwepo endelevu unaofanya mageuzi na uongofu uwezekane kila siku. Sisi nafasi yetu ni kusikia sauti ya Mungu na kutimiza mapenzi yake – Mt. 7: 21-29. Mtu mmoja alimwuliza Padre ni jinsi gani ajitolee maisha yake kwa Mungu, jinsi gani afanye ili apate kuongoka. Yule padre alitoa karatasi nyeupe isiyoandikwa cho chote na kumwambia inatosha kuandika jina lako na kuweka saini sehemu ya chini ya karatasi na kumwacha Mungu ajaze mapenzi yake sehemu iliyobaki wazi.

Nasi pia hatuna budi kumwachia Mungu aandike upya ukurasa wa maisha yetu. Hilo ndilo dai la maisha ya ufuasi. Sisi tunamtaka Mungu katika maisha yetu lakini tunataka kutimiza kwanza mapenzi yetu wenyewe. Haiwezekani kumwekea Mungu masharti. Tunaalikwa tuyapokee na kuishi mapenzi yake. Yesu ameweka wazi katika injili ya leo. Yesu kwanza. Je katika kushiriki kwetu katika ujenzi wa taifa la Mungu tukoje? Mahali fulani katika Injili tunasikia habari ya mtu aliyetaka kumfuata Yesu, mwingine anataka kumfuata lakini anataka kwanza akazike wafu wake au yule aliyetaka kwanza kwenda kuaga familia yake ndipo aje amfuate Bwana. Yesu anaweka wazi taratibu za ufuasi. Nasi tuombe daima neema na baraka ya roho wake ili tuwe waaminifu katika kumtumikia yeye.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.