2017-01-21 09:21:00

Rais Donald Trump: Usiwasahau akina Lazaro wanaohitaji msaada wako!


Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za pongezi na matashi mema Rais Donald Trump wa Marekani aliyeapishwa, tarehe 20 Januari 2017 kuwa ni Rais wa 45 kuwaongoza Wamarekani. Baba Mtakatifu ametua fursa hii kumhakikishia Rais Trump sala na sadaka yake ili Mwenyezi Mungu aweze kumkiria hekima na nguvu katika utekelezaji wa madaraka yake kama Rais. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, katika wakati huu mgumu ambamo familia ya binadamu inakabiliana na changamoto nyingi kuna haja ya kuwa na mwono mpana sanjari na sera shirikishi zinazoweza kukabiliana na changamoto hizi.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maamuzi yatakayotolewa na Rais Donald Trump yataongozwa na utajiri mkubwa wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kanuni maadili; mambo ambayo yamejenga historia ya Watu wa Amerika pamoja na jitihada za taifa hili katika mchakato wa kukuza na kudumisha utu, heshima na uhuru sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anakaza kusema, chini ya uongozi wa Rais Trump, Amerika iendelee kuguswa na mahitaji ya maskini, wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na wahitaji zaidi kama akina Lazaro wanaosimama malangoni kuomba msaada! Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wa salam na matashi mema kwa Rais Donald Trump wa Marekani kwa kumtakia yeye binafsi, familia pamoja na familia ya Mungu nchini Marekani katika ujumla wake, baraka, amani, maridhiano na maendeleo ya kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.