2017-01-21 18:05:00

Kimbembe! Yesu alifundisha, akahubiri na kuponya!


Jumapili iliyopita tulikuwa Bethbara (Betania iliyo ng’ambo ya mto Yordan) katika mkoa wa Yudea. Huko Yohane mbatizaji alimtambulisha Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu.  Yohane alituonesha Mwanakondoo tuliyetakiwa kumfuata mwaka mzima ili tukitaka kufanikiwa katika maisha. Mwanakondoo huyo atatuongoza kuelekea ulimwengu mpya wa ufalme wa Mungu. Fasuli ya leo inaanza hivi: “Basi Yesu aliposikia ya kwamba Yohane amefungwa, alikwenda zake mpaka Galilaya.” Kwa hiyo Yesu aliyekuwa Yudea sasa amerudi mkoani kwake Galilaya, akipitia Nazareti kumsalimia kifupi mama yake kisha akaenda “Kapernaum mji ulioko pwani ya ziwa lile la Galilaya, mipakani mwa Zabuloni na Naftali.” Hapo Kapernaumu Yesu akafanya makazi yake nyumbani kwa Petro na Andrea akifanya kazi yake ya kufundisha, kuhubiri na kuponya. Kuna sehemu nyingine muhimu tutakazozisikia katika injili kama vile Betsaida uliokuwa kaskazini kabisa ya ziwa la Galilea. Huko Betsaida wanatoka mitume watano lakini leo tutawasikia wanne tu. Hata Petro na Andrea, walitokea Betsaida lakini kwa hoja za kiuvuvi, walihama hapo na kwenda kuishi Kapernaumu. Mji huu ulikuwa na wakazi wengi hasa wavuvi na wa wakulima. Kumbe Korazini ni mji uliokuwa pembeni ya Galilea.

Yesu aliacha kukaa na Mama yake Nazaret, akaondoka: “akaja akakaa Kapernaumu.” Kadiri yangu naona kama Yesu angeendelea kuishi Nazareti na Mama yake, angedumaa kifikra na kusingepatikana mapato mazuri ya utume aliowania kuuleta duniani. Hoja ilikuwa ni kwamba watu wa Nazareti (mlimani) walikuwa na fikra finyu za kushindwa kupokea mabadiliko na mafundisho mapya ya Yesu. Kwa hiyo Yesu akahamia Kapernaumu kulikoonekana kumekucha kibiashara, kimwingiliano wa dini, wa fikra na wa tamaduni tofauti za watu. Mwinjili Mateo anaongeza kigezo kingine kilichomfanya Yesu aende kukaa Kapernaumu. Kigezo chake anakitegemeza kwenye Agano la Kale inaposema: “Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa.” (Isaya 9:1).

Kwamba, katika Agano la Kale zabuloni, Naftali na Galilaya ya wapagani inajitokeza mara sita tu. Kwa sababu sehemu hiyo hawakuwa watu wanafuata sana imani kama watu wa Yudea. Aidha kisiasa tunaweza kuwafananisha raia wa Galilaya kuwa kama vyama vya upinzani, kwa sababu Wagalilaya walikuwa daima wanaingia mitaani kufanya migomo. Hivi hata Yesu hakuwa na jina zuri kwa vile alitoka Galilaya. Aidha, nabii Isaya aliiishi wakati ambapo mkoa wa Galilaya ulikuwa unatawaliwa na Waasiria. Hao walikuwa wakatili sana, waliowatesa na kuwatawala raia wao kwa mabavu. Hivi aina hiyo ya utawala mkali, mbovu na ya watu walikuwa katika hali ngumu ya maisha akailinganisha na giza nene la usiku iliyotawala nchi hiyo. Kwa hiyo Isaya anatoa unabii wake akisema: “Watu waliokuwa wanatembea katika giza, mwanga mkuu umewazukia. Nao waliookuwa katika nchi na uvuli wa mauti mwanga mkubwa umewazukia.” (Isaya 9:1). Kwa hiyo, kwa kufika Yesu Kapernaumu, nuru kutoka mbinguni imeingia Kapernaumu. Watu, wapagani waliokuwa wanaishi katika giza la kuonewa, na kukandamizwa, rushwa na makwazo, sasa wameona mwanga. Yesu alisema: “mimi ni mwanga wa dunia.” Tunahitaji mwanga wa Injili katika ulimwengu wa giza la matatizo ya maisha.

Yesu alianza kuhubiri Kapernaumu akisema: “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Kutubu maana yake ni kubadilika, hasahasa kubadilika namna ya kufikiri. Namna ya kufikiri inayotawala ulimwenguni ni ile ya ukuu na utawala, ya fedha, ya mafanikio nk. Kumbe thamani za fikra za utawala wa mbingu ni upendo, kujitoa, kutumikiana nk. Kwa hiyo kutubu maana yake kubadili fikra hizo na kupokea fikra mpya za Kristo. Mbele ya mwanga mtu unaweza kufungua macho kuona au kukataa kufungua. Baada ya mwito huo wa kuongoka, Yesu anaita jozi mbili za wa watu ili kutuonesha namna ya kuongoka tunakotakiwa kuwa nako. Mosi Yesu aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini, kwa maana walikuwa wavuvi” Mwito huu wa Yesu ni tofauti kabisa na ule alioamriwa kuufanya Abrahamu: “Nenda katika nchi nitakayokuonesha” Haikujulikana alikoambiwa kwenda labda angefunuliwa polepole pahala pa kwenda. Kumbe kwa Yesu, mwito huo siyo tena wa “Nendeni” bali anasema: “Nifuateni mimi.” Huu siyo mwito wa nadharia, bali ni wa matendo. Kumfuata mtu asiye wa ulimwengu, bali wa mbingu yaani Mwana kondoo.

Aidha, Yesu hatoi ahadi kama vile ya kuwa matajiri, au kuwa wenye nguvu. Bali anawapa kazi moja tu. “Nifuateni nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.” Kuwavua watu maana yake ni kuwatoa kutokana katika mazingira mabaya, maovu yasiyo ya kiutu, ya ulimwengu wa kale na kuwaingiza ulimwengu mpya. Kisha wao “mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.” Maana yake, unapotoa uamuzi fulani yabidi kuufanyia kazi mara moja bila kuhoji maswali. Wavuvi wale wanaacha nyavu zile zinazotunasa katika ulimwengu wa kale. Aidha, Petro na Andrea walikuwa wavuvi kama kazi yao ya maisha iliyokuwa inawaletea riziki.

Hawakuwa wameambiwa kuacha ile kazi, la hasha, wangeweza bado kuendelea na kazi yao, lakini malengo na namna ya kufanya kazi ile ilibadilika. Unapoacha ulimwengu wa kale, ngazi ya uthamani wa mambo inabadilika. Mabadiliko ya thamani ya mambo na kazi ya mfuasi wa Kristu, ni kule kufikiri jinsi ya kuwapa wengine furaha katika kazi na katika shughuli zako, kuliko kufikiria kiasi gani cha mshahara utakipata. Lengo linakuwa ni kufanya ulimwengu uwe na raha, amani na furaha.

Jozi ya pili ya kuongoka ni mwito wa Yakobo na Yohane: “Yesu anaendelea mbele, Yakobo na Yohane wako na baba yao Zebedayo wakitengeneza nyavu zao. Akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao”. Kuachana na baba maana yake kuachana na mapokeo kwani baba ni mtunza utamaduni na mila. Chombo (mashua) kina maana ya jumuia. Hivi wanaacha jumuia ya kale na kuingia (mashua mpya) yaani jumuia mpya ya ufalme wa Mungu. Aidha kuacha chombo cha kazi ni kubadili namna ya kufanya mambo, au shughuli, au kazi inayokuingizia mshahara. Hatima ya fasuli inatudokezea matendo matatu yanayohitimisha kazi nzima ya Yesu aliyofanya Galilea nzima kwamba: “Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi, akihubiri Habari njema ya Ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.” Kufundisha, mwanga mpya kwa kila mtu. Kuhubiri Habari njema, ni kutoa matumaini mapya ya maisha na Kuponya wagonjwa na udhaifu. Hiyo ni alama ya uponyi wa kiroho, kutoka ugonjwa wa kikatili. Injili ni mwanga unaotuponya na wivu, rushwa, uovu, na hali hii isiyo ya kibinadamu. Tuuache mwanga uingie ndani mwetu na kutuangaza katika maisha yetu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.