2017-01-20 17:05:00

Mnahamasishwa kuchuchumilia utakatifu!


Yesu katika maisha na utume wake, aliwataka wafuasi wake kuwa wakamilifu na watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Yesu mwenyewe ni chanzo na utilimifu wa utakatifu wa maisha, changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba kwa msaada wa neema na baraka ya Mungu wanashika na kutimiza utakatifu katika safari ya maisha yao hapa duniani. Ni watu wanaopaswa kujivika: moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu, daima wakijitahidi kuambata matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yao. Waamini wanakumbushwa kwamba, daima wanahitaji kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kwa kutii mapenzi ya Mungu; kwa kujitoa bila kujibakiza kwa ajili ya utukufu wa Mungu na huduma makini kwa jirani. Na kwa njia hii, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utakatifu wa Taifa la Mungu utazidi kuzaa matunda kedekede kama inavyoshuhudiwa katika historia ya maisha na utume wa Kanisa!

Katika kipindi cha Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, wenyeheri kumi walitangazwa kuwa ni Watakatifu na watumishi wa Mungu 14 walitangazwa kuwa ni wenyeheri katika kipindi cha mwaka 2016. Hawa ni wale wanaotoka Albania, Argentina, Ufaransa, Mexico, Hispania na Sweden. Haya yamesemwa hivi karibuni na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, katika hotuba yake elekezi aliyoitoa kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana.

Kati ya watakatifu wapya: kuna Askofu mmoja na Mapadre wanne; ambao kati yao watatu ni waanzilishi wa Mashirika ya Kitawa duniani. Kuna shuhuda wa imani, aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kutoka Ufaransa pamoja na watawa watatu, kati yao ni Mama Theresa wa Calcutta, “Jembe na shuhuda wa huruma ya Mungu” kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ibada ya kuwatangaza watumishi wa Mungu kuwa wenyeheri imeadhimishwa katika mataifa saba: Albania, Argentina, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Kazakhstan pamoja na Laos. Orodha ya mashuhuda wa imani, waamini walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake ni 79; kati yao kuna Wakleri, Watawa pamoja na waamini walei. Waungama imani waliotangazwa kuwa wenyeheri katika kipindi cha Mwaka 2016 ni 7 kati yao kuna wanawake 4 na wanaume 3.

Kardinali Angelo Amato katika hotuba yake elekezi iliyojikita kwa namna ya pekee katika “Utakatifu na mchakato wake Kikanisa” ni dhamana pevu inayovaliwa njuga na watoa hoja kwa kushirikiana kwa karibu sana na Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Ni kazi inayojikita katika nyaraka zinazoonesha: fadhila za Kikristo, Ushuhuda wa Imani na Miujiza iliyotendwa kama kielelezo cha neema ya Mungu kwa watu wake. Katika kipindi cha miaka 10 yaani kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2016 maombi 351 yamewasilishwa mjini Vatican, kuomba mchakato wa kuwatangaza waamini hawa kuendelea katika ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu. Kutoka Barani Afrika kuna maombi yaliyowasilishwa kutoka katika nchi ya Algeria, Madagascar, Somalia, Afrika ya Kusini na Uganda. Katika maombi 351 kati yao maombi 293 yanaonesha fadhila za Kikristo na 58 ni ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Angelo Amato anasema, katika mwelekeo huu, Kanisa linapenda kuonesha utajiri mkubwa wa maisha ya watoto wake ambao wamejitahidi kuambata utakatifu kiasi kwamba, umekuwa ni chemchemi inayobubujikia katika jangwa la maisha ya binadamu. Hawa ni waamini ambao wamejipambanua kwa kujitoa bila ya kujibakiza katika huduma ya upendo kwa jirani. Mama Kanisa anafundisha na kuhimiza kwamba, utakatifu ni wito kwa Wakristo wote pasi na ubaguzi, kwani wote wanaitwa kuwa ni watakatifu na wakamilifu kama alivyo Baba yao wa mbinguni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.