2017-01-19 15:51:00

Sitisheni mgomo, wananchi wanakufa kwa magonjwa!


Maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa na wote. Mama Kanisa anafundisha kwamba, ugonjwa na mateso yamekuwa daima kati ya matatizo mazito sana yanayoyaweka maisha ya mwanadamu katika majaribu mazito. Katika ugonjwa mtu anapata mang’amuzi ya kutokuwa na uwezo, ya mipaka na kikomo chake. Kila ugonjwa unaweza kumfanya mwanadamu achungulie kifo!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwa kuzingatia mateso na mahangaiko ya wagonjwa ambao kwa sasa wengi wao wanachungulia kifo kutokana na mgomo wa madaktari na wauguzi nchini Kenya, linarudia tena wito na mwaliko wa kuwasihi wahudumu wa sekta ya afya nchini Kenya kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma kwa wagonjwa ambao kwa sasa wanachungulia kifo! Wafanyakazi hawa kuanzia tarehe 5 Desemba 2016 wamekuwa wakifanya mgomo hali ambayo imesababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa wagonjwa na familia. Baraza la Maaskofu Katoliki linakaza kusema, hali ni mbaya zaidi vijijini na wanaoteseka zaidi ni maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Askofu Philip A. Anyolo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anapenda kuwapongeza wahudumu katika sekta ya afya ya umma na binafsi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa licha ya hali ngumu ya mazingira ya kazi na uchumi wanayokabiliana nayo. Askofu Anyolo anazipongeza taasisi binafsi zinazoendeleza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, hasa pale maskini ambao ni wagonjwa wanashindwa kupata huduma ya afya kutokana na uwezo wao wa kiuchumi kuwa mdogo!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaiomba Serikali pamoja na viongozi wa wafanyakazi katika sekta ya afya kukaa kwa pamoja na kuzungumza, ili tatizo na changamoto ya afya nchini Kenya iweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Maaskofu wanasikitishwa na uamuzi wa wafanyakazi katika sekta ya afya kuwatelekeza wagonjwa kwa kudai kwanza masilahi yao kwani maisha yanapaswa kupatiwa kipaumbele cha kwanza kuliko mambo mengine yote! Wafanyakazi katika sekta ya afya wanakumbushwa kwamba, walikula kiapo cha kutegemeza maisha ya binadamu, kumbe, kushindwa kutekeleza dhamana na kiapo hiki ni kwenda kinyume kabisa cha maadili ya kazi. Maaskofu wanasikitishwa na ukimyaa unaofanywa na Serikali katika sakata hili wakati watu wengi wanaendelea kuhatarisha maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.