2017-01-16 11:25:00

Michapo ya Baba Mtakatifu Francisko na waamini Roma!


Baba Mtakatifu Franciko akiwa Parokiani Santa Maria Setteville di Guidonia Jimbo kuu la Roma, Jumapili tarehe 15 Januari 2017 alipata nafasi ya kukutana na makundi mbali mbali Parokiani hapo. Alikutana na Kikundi cha wagonjwa; watoto na vijana; wazazi na walezi wa watoto waliobatizwa katika mwaka 2016, mwishoni amekutana na kuzungumza pia na wahudumu wa shughuli za kichungaji Parokiani hapo! Kila kundi lilipewa ujumbe wa kufanyia kazi katika maisha na utume wa Kanisa.

Akizungumza na wagonjwa, Baba Mtakatifu Francisko anasema, ugonjwa ni Fumbo katika maisha ya mwanadamu, ndiyo maana Yesu alipenda kuwa karibu sana na wagonjwa, ili kuwaponya katika shida na mahangaiko yao pamoja na kuwasamehe dhambi zao. Waamini pia wanahimizwa kuwatembelea, kuwasaidia na kuwafariji wagonjwa, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Kristo unaobubujika kutoka kwenye ushuhuda wa waamini. Amewataka wagonjwa kuwa na imani, matumaini na ujasiri wanapokabiliana na magumu katika maisha yao, kamwe wasisahau kusali kwa ajili yao na kwa ajili ya kuliombea Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na watoto pamoja na vijana amewaonya kwamba, Sakramenti ya Kipaimara si mwisho wa vijana na watoto  kwenda tena Kanisani, watu ambao watauna tena mlango wa mlango wa Kanisa, wakati wakijiandaa kwa ajili ya Sakramenti ya Ndoa! Hili si jambo zuri katika ukuaji wa maisha ya kiroho. Jumuiya ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake, kumbe wanapaswa kujenga na kuimarisha maisha ya Kijumuiya kwa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa: mahali  wanapojichotea utajiri wa Neno la Mungu na kulishwa Mkate wa Malaika, yaani Ekaristi Takatifu, ili kuweza kupata utimilifu wa furaha ya kweli katika maisha!

Baba Mtakatifu anawataka watoto na vijana kujenga ujasiri wa kuzungumza na Kristo Yesu katika maisha yao, kama kielelezo makini cha ushuhuda wa Kikristo unaobubujika kutoka katika kinywa cha mwamini, lakini zaidi kutoka katika sakafu ya maisha na kudumishwa kwa njia ya mikono yenye huruma na upendo! Wakristo wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao, waoneshe moyo wa toba, wongofu wa ndani na msamaha, tayari kuanza kuanza upya katika maisha yao. Waamini wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa jirani zao.

Imani anasema Baba Mtakatifu inapaswa kushuhudiwa katika matendo yanayofafanua kile ambacho kweli mwamini ana amini kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Kusamehe na kusahau ni fadhila inayopaswa kumwandama Mkristo katika maisha yake! Lakini, ikumbukwe kwamba, kusamehe si rahisi, lakini inawezekana. Kuna uwezekano wa kuponya madonda ya ndani katika maisha ya mwanadamu, lakini msamaha wa kweli unapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya maisha ya mwamini.

Zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia binadamu ni Imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu pamoja na maisha ya familia. Imani inapaswa kurutubishwa kila siku kwa njia ya Neno, Sakramenti na ushuhuda amini. Mwamini asipokuwa makini anaweza kutembea katika giza kiasi hata cha kuweza kupoteza imani yake. Baba Mtakatifu amesema, kwamba, shida, magumu na changamoto za maisha, wakati mwingine zinaweza kumpelekea mwamini kukosa imani kwa Mwenyezi Mungu. Jumamosi iliyopita, tarehe 15 Januari 2017, Baba Mtakatifu alitoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga 13 waliozaliwa baada ya tetemeko la ardhi sehemu mbali mbali za Italia. Baadhi ya watoto hawa wamewapoteza wazazi wao. Katika mazingira kama haya, ni rahisi sana kupoteza imani, lakini kimsingi imani inapaswa kulindwa, kuendelezwa na kuhifadhiwa.

Baba Mtakatifu alipokutana na wazazi pamoja na walezi wa watoto waliobatizwa katika kipindi cha Mwaka 2016 amewakumbusha kwamba, watoto hawa ni hazina, amana na furaha ya Kanisa kuona watoto hawa wakikua na kuongezeka, kwani wanayo nguvu ya kupyaisha maisha ya watu, licha ya matatizo na changamoto za maisha. Hata katika misigano na mipasuko ya kifamilia, wanandoa wajitahidi kuhakikisha kwamba, haya yanakuwa ni mambo yao wawili na kamwe watoto wasihusishwe, kwani wanateseka sana kuwaona wazazi wao wakipimana nguvu kwa njia ya maneno na mateke! Hata katika mazingira kama haya, wanandoa wawe na ujasiri wa kuombana msamaha, tayari kusonga mbele katika maisha.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa Parokiani Santa Maria Setteville di Guidonia Jimbo kuu la Roma amekutana na mihimili ya Uinjilishaji Parokiani. Hawa ni wahudumu wa Neno na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa wagonjwa na wazee; ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anasema, hata yeye katika maisha yake ana nyakati za kujipatia mapumziko kwa: kusoma, kuangalia sinema nzuri pamoja na kusikiliza muziki kama ule wa Tango, lakini wa Rock, hapana huu ni muziki kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya!

Baba Mtakatifu anawashukuru waamini walei wanaojisadaka kwa ajili ya kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa mataifa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni wito kutoka kwa Mungu unaowataka waamini hawa kuwa na ujasiri kama ule waliokuwa nao Mitume Siku ile ya Pentekoste, walipotoka kifua mbele na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Tangu wakati huo, kuna wamissionari wengi ambao wamejisadaka kwa ajili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kiasi hata cha kufariki dunia wakiwa katika umri wa ujana! Ni wahudumu wa Injili ambao maisha yao yalizimwa kama “kibatari” kwa magonjwa kama vile Malaria! Hawa ni mashuhuda wa Injili ya Kristo! Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwapatia baraka zake za kitume, wanaparokia waliokuwa wamekusanyika nje ili kumtakia safari njema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.