2017-01-14 10:10:00

Hati ya Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa Vijana 2018


Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwezi Oktoba, 2018 yataongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na mang’amuzi ya Miito”. Maandalizi haya tayari yameanza kwa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kutoa Hati ya Maandalizi ya Sinodi ya XV ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Hati hii ni mwaliko wa kumfuasa Yohane, mwanafunzi aliyependwa zaidi na Yesu.

Hati inaangalia hali ya vijana duniani: utambulisho na ushiriki wao; mambo rejea binafsi na taasisi pamoja na mchakato wa kuunda vijana wa kizazi kipya wanaoshikamana zaidi. Sura ya pili inajikita katika imani, mang’amuzi na wito kwa kuzingatia umuhimu wa imani na wito katika maisha ya vijana; zawadi ya kufanya mang’amuzi ya miito ili kutambua, kutafsiri na kuchukua maamuzi ya maisha. Sura ya tatu inapembua kwa kina na mapana shughuli za kichungaji kuhusu miito kwa kuwataka viongozi wa Kanisa kufanya hija na vijana katika maisha yao, ili hatimaye waweze kutoka, kuona na kuitikia wito wa kumfuasa Kristo Yesu. Walengwa wakuu ni vijana wote pasi na ubaguzi; Jumuiya inayojihusisha na malezi ya miito pamoja na kuwa na watu ambao ni mfano bora wa kuigwa. Shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito zinatekelezwa katika maisha ya kila siku sanjari na ushiriki mkamilifu katika masuala ya kijamii. Hati inachambua maeneo maalum ya shughuli za kichungaji bila kusahau ulimwengu wa mitandao ya kijamii, ambamo vijana wengi wanapenda kuogelea huko.

Lugha, elimu makini na mikakati ya Uinjilishaji; ukimya, tafakari na sala ni mambo ambayo pia yanapewa kipaumbele cha pekee kwenye hati ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018. Mwishoni, Hati hii inamwangalia Bikira Maria aliyehifadhi, akatafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yake, ili aweze kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha ya miito yao! Kuna maswali dodoso yatakayosaidia kuandaa Hati ya Kutendea Kazi, maarufu kama “Instrumentum Laboris”, kwa kuangalia hali ya kila bara. Namna ya kukusanya takwimu, kuzitafsiri na kuzifanyia kazi.

Katika utangulizi wake, Hati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 inatoa mwaliko kwa vijana wote ili waweze kupata utimilifu wa furaha ya maisha, kwani Kanisa limekabidhiwa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili. Huu ni mwaliko wa kuwasaidia vijana ili kupata mang’amuzi kuhusu miito mbali mbali ndani ya Kanisa kama: watu wa ndoa, watawa na mapadre, ili kwa njia ya mwanga wa imani, wawe tayari kushuhudia utimilifu wa furaha katika miito yao! Kanisa linatambua na kuthamini nguvu ya furaha inayobubujika kutoka kwa vijana ambao kimsingi ni jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Baada ya hati hii kuchapishwa, sasa Kanisa limeanza rasmi mchakato wa kupata ushauri kutoka ndani na nje ya Kanisa ili hatimaye kuliwezesha Kanisa kupata mawazo makuu yatakayofanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Vijana wanahamasishwa kufuata mfano wa Mtakatifu Yohane na wenzake waliojitaabisha kwenda kumtafuta Yesu, wakamwona, akawakaribisha na kujenga nao uhusiano wa urafiki wa kudumu, mwaliko kwa vijana pia kuwa kweli ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu!

Sura ya kwanza: Hali ya Vijana Duniani! Sura hii inapembua hali ya vijana duniani ili kugusa undani wa maisha ya vijana kimaadili na kiroho, tayari kufanya mang’amuzi ya maisha na wito wao. Kuna hali ya kutojaliana, idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa; tamaduni na mapokeo ya imani ya Kanisa toka nchi moja hadi nchi nyingine. Bado kuna ubaguzi kati ya watoto wa kike na wavulana. Vijana wanaojadiliwa ni wale wenye umri kati ya miaka 16- 29 lakini pia umri huu unategemea na mahali walipo vijana.

Dunia inabadilika kwa kasi kubwa jambo ambalo linahitaji kuwa na sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa muda mrefu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna idadi kubwa ya vijana ambao hawana fursa za ajira; kuna athari za mabadiliko ya tabianchi; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji lakini pia wapo vijana wachache wanaofaidika na ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Pamoja na maendeleo yote haya lakini kuna vijana wengi bado wanajikuta wakiwa wametumbukia katika upweke hasi na hali ya kukata tamaa kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Rasilimali ya dunia inatumika kwa ajili ya mahitaji ya watu wachache na kwamba, kuna uharibifu mkubwa wa mazingira hali inayotishia usalama na maisha ya kizazi kijacho!

Vijana wa kizazi kipya wana mwelekeo mpya, matamanio na jinsi ya kujenga mahusiano yao na wengine mambo ambayo yanaathari zake katika mchakato wa mafungamano ya kijamii na utambulisho wa vijana wa kizazi kipya. Kuna mwingiliano mkubwa wa tamaduni za watu kutokana na sababu mbali mbali kama vile changamoto ya wahamiaji, wakimbizi pamoja na elimu. Vijana wanakumbana na hali ngumu ya maisha, ujinga, umaskini, magonjwa na hali ya kubaguliwa. Baadhi yao wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi; ni wahanga wa utumwa mamboleo; biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya na kwamba, kuna baadhi yao wanatumbukizwa katika uhalifu wa magenge na ujambazi.

Kimsingi vijana wengi wanataka kuwa wadau wakuu katika mchakato wa mageuzi ya kijamii, lakini kwa bahati mbaya wanakosa dira na mwelekeo sahihi katika maisha kutokana na kukosa elimu, ajira, ujuzi au maarifa; hali ambayo inawapelekea vijana wengi kukosa imani na matumaini katika maisha yao. Vijana wanataka kuona mifano ya watu na taasisi ambazo zitakuwa ni mfano bora wa kuigwa katika hija ya maisha yao. Hawa wanaweza kuwa ni wazazi, walezi na taasisi ambazo iko karibu sana na watu. Kutokana na mwelekeo huu, vijana wengi wanajikuta wanashindwa kushiriki katika maisha ya kiimani! Ni vijana wanaojifunza kuishi bila ya uwepo wa Mungu, Injili na Kanisa kwa kujidanganya kwamba, wanaweza kujiokoa wao wenyewe na matokeo yake ni kutumbukia katika ubinafsi! Vijana wa kizazi kipya wanaunganishwa kwa kiasi kikubwa na mitandao ya kijamii ambayo ina faida na hasara zake kwani kuna kiasi kikubwa cha mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema.

Kumbe, hapa kuna haja ya kujenga utamaduni unaokidhi maisha na wito wa vijana. Vijana wanapaswa kufanya maamuzi magumu na machungu katika maisha yao kwa kujikita katika ujasiri na kujiaminisha kwa Kristo Yesu. Vijana wakati mwingine wanashindwa kufanya maamuzi magumu kutokana na ukosefu wa fursa za ajira, hali mbaya ya kiuchumi na ukosefu wa ujuzi; hali mbaya ya maisha ya familia pamoja na tabia ya vijana wengi kutengwa kutokana na sababu mbali mbali: za kiuchumi, kijamii na kidini. Hata hivyo, vijana wengi wanaweza kupata fursa ya maisha bora zaidi kwa kuwa na sera na mikakati mipya ya maendeleo.

Sura ya pili: Imani, Mang’amuzi na Miito! Mama Kanisa katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana anataka kukutana, kuwasindikiza na kuwasaidia vijana pasi na ubaguzi ili kweli vijana waweze kupata utimilifu wa maisha kwa kutambua kwamba maisha na imani ni zawadi ya Mungu. Ili kuwahudumia vyema vijana anasema Baba Mtakatifu Francisko kunahitajika: wema, upole na majitoleo ya dhati kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu, mtu mwenye haki, jasiri na mchapakazi; aliyeonesha huruma na upendo. Kuna uhusiano wa pekee kati ya imani  na wito, kwani hapa vijana wanajisikia kupendwa na kuthaminiwa.

Imani inawasaidia vijana kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa dhati, tayari kushuhudia tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, matokeo ya majadiliano ya kina katika dhamiri nyofu! Wito na mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu, umesheheni furaha na majitoleo ya dhati ambayo yanapaswa kutakaswa, kuwekwa huru ili kutambua jambo jema na kulitenda. Vijana wanapaswa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kusoma alama za nyakati na kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu katika historia; kwa kung’amua kilicho chema na kukifuata, ili kupata utimilifu wa maisha. Mkazo ni kutambua, kutafsiri na kuchagua kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka katika maisha ya kijana!

Mchakato wa mang’amuzi ya wito ni hija ndefu katika maisha yenye milima na mabonde kama ilivyokuwa kwa Abramu, Baba wa imani. Wito daima unaambatana na utume unaopaswa kupokelewa kwa uchaji, ari na moyo mkuu, tayari kujisadaka na kuchukua Msalaba wako, ili kumfuasa Kristo Yesu. Hapa kuna haja ya kuondokana na ubinafsi tayari kuambata tunu msingi za Kiinjili kuelekea ukomavu katika wito. Katika mchakato wa kuwasindikiza vijana katika mang’amuzi ya wito wao, ikumbukwe kwamba vijana hawa wanapaswa kutenda kadiri ya mwanga wa imani kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu anatenda kazi ndani mwao; kwa kusikiliza kwa makini wanaweza kung’amua wito wao, lakini wakumbuke kwamba, dhambi daima itaendelea kumwandama mwanadamu, kumbe, hapa kijana anapaswa kufanya maamuzi magumu katika maisha yake. Vijana wajenge utamaduni wa kumsikiliza Roho Mtakatifu kwa makini; wajenge mahusiano ya dhati na Kristo Yesu kwa kuimarisha na kudumisha maisha ya kiroho: kwa njia ya Tafakari ya Neno, Ibada ya Kuabudu, Matendo ya huruma na ushuhuda makini wa tunu msingi za maisha ya Kikristo pasi na woga. Vijana wanapaswa kusindikizwa kwa njia ya sala na kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu anayeangaza na kuwaongoza waja wake.

Sura ya Tatu: Mikakati ya shughuli za kichungaji: Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa vijana inapaswa kujielekeza mahali waliko vijana katika maisha yao ya kila siku, ili kuwasaidia kujenga historia ya maisha yao. Yesu apewe nafasi ya kuweza kutembea na vijana hatua kwa hatua ili aweze kusimama na kuwaangalia kwa jicho lenye huruma na upendo, ili kwa kufunga safari na vijana, Jumuiya nzima ya waamini iweze kujengwa na kuimarishwa. Vijana wapewe nafasi ya kuonesha na kushirikisha kipaji chao cha ugunduzi; kwa kuwa na mwono na mwelekeo mpya na mpana zaidi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji.

Hapa, Mama Kanisa anakazia mambo makuu matatu: kutoka, kuona na kuitwa! Utume kwa vijana ni mchakato unaopaswa kuwashirikisha vijana wote pasi na ubaguzi kwa kutambua kwamba, Jumuiya ya waamini nayo inawajibika barabara katika malezi, makuzi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya. Jambo la msingi ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa vijana kwa kuwashirikisha vijana katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa linawataka wazazi, walezi na familia; viongozi wa Kanisa pamoja na walimu kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya.

Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa vijana inapaswa kujikita katika uhalisia wa maisha ya vijana na utekelezaji wa majukumu yao katika jamii. Vijana wanapaswa kujifunza kutumia vyema rasilimali muda, fedha, mali na mahusiano binafsi na ya kijamii. Vijana wawe na vipaumbele katika maisha, ili hatimaye kuwa na mwelekeo wa kuweza kufanya maamuzi magumu na machungu katika maisha. Imani ya kweli ni nyenzo msingi inayoweza kumsaidia kijana kufanya maamuzi mazito katika maisha yake hasa pale anapokabiliana na kinzani na magumu ya maisha. Hapa kuna haja ya kujenga mshikamano wa huruma na upendo kwa maskini, tayari kushiriki katika mchakato wa maboresho ya maisha yao.

Sera na mikakati shughuli za kichungaji itaendelea kutekelezwa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani na katika maadhimisho yanayofanywa katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Parokia ni mahali muafaka pa shughuli za kichungaji kwa vijana wakati wa maandalizi ya kupokea Sakramenti za Kanisa; kwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa mahalia pamoja na vituo vya michezo vinavyosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa. Vyuo vikuu, taasisi za elimu ya juu na shule ni sehemu muafaka pa kumwilisha utume wa vijana sanjari na ushiriki wa vijana katika shughuli mbali mbali za kijamii; vyama vya kitume! Seminari na nyumba za malezi ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha mang’amuzi ya miito ndani ya Kanisa bila kusahau pia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, mahali ambako vijana wengi wanapenda kuogelea huko kwa raha zao wenyewe!

Vyombo vya umwilishaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji vinapaswa kuzingatia lugha katika mazingira ya Kibiblia, Kiliturujia, Kisanaa, Katekesi na njia za mawasiliano ya jamii, kwa kugundua na kuthamini mchango wa vijana. Kuna haja ya kusaidiwa kukua na kukomaa  katika uhuru kamili kwa kuzingatia elimu makini. Ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika haki, huduma, upendo, umoja na mshikamano ni muhimu sana katika malezi na makuzi ya vijana. Jumuiya ya wakristo inahamasishwa kuwasikiliza na kuwakumbatia wale wote wanaotaka kuonana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao.

Vijana wanaweza kufanya mang’amuzi ya miito yao kwa kujenga na kudumisha utamaduni ukimya, tafakari ya kina na sala ili kujenga urafiki aminifu na dumifu na Kristo Yesu. Kanisa linapenda kuuweka mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria aliyehifadhi, akatafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yake, ili kila kijana aweze kujifunza kutoka kwa Bikira Maria mtindo wa kusikiliza, ujasiri wa imani, mang’amuzi ya maisha na sadaka katika huduma, daima wakijitahidi kujiaminisha mbele ya Mungu.

Mwishoni, Hati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018 inatoa maswali dodoso ya jinsi ya kukusanya takwimu; kusoma na kutafasiri takwimu za vijana wanaohudhuria maeneo ya Kanisa, wale ambao wako nje au wale wanaojisikia kuwa ni wageni kabisa katika maeneo ya Kanisa. Maswali ya utume kwa vijana kuhusu miito; walezi na waalimu na mwishoni maswali msingi kwa kila bara pamoja na kushirikisha wengine takwimu zilizopatikana yamekaziwa kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.