2017-01-12 08:27:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji 2017


Wahamiaji wadogo ni wahanga pasi na sauti ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani itakayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 15 Januari 2017. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa siku hii, anaangalia kwa jicho la masikitiko mateso na mahangaiko ya watoto wadogo wanaolazimika kukimbia nchi zao na kujikuta wakiwa wanaishi ugenini.

Watoto hawa ambao “hawaonekani” na wala hawana sauti wamejikuta wakiishi katika mazingira magumu na hatarishi yanayowatumbukiza kwa urahisi katika ukahaba na biashara ya ngono; ni kundi linalofanyishwa kazi za suluba pamoja na kupelekwa mstari wa mbele kama askari. Watoto hawa wamekuwa wakibebeshwa mzigo wa biashara haramu ya dawa za kulevya na hatimaye kutumbukizwa katika magenge ya kihalifu. Ni watoto wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, nyanyaso, dhuluma na matokeo yake wanajikuta wakiwa peke yao bila msaada wa wazazi na walezi wao. Maandiko Matakatifu yanaonya kwa ukali wale wote wanaosababisha makwazo kwa watoto wadogo kwamba, iko siku watakiona cha mtema kuni!

Baba Mtakatifu Francisko anaialika familia ya Mungu kuonesha upendo na ukarimu kwa watoto wadogo wanaoishi kama wakimbizi na wahamiaji, kama njia ya kumwilisha Mafundisho ya Kristo Yesu, aliyefanyika mwili, ili kuonesha ukaribu na mshikamano na binadamu, ili kumwelekea Mwenyezi Mungu kwa njia ya imani inayorutubishwa kwa matumaini na mapendo; mambo msingi yanayofumbatwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; tunu ambazo zimekaziwa sana katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2017, anapenda kukazia matendo na mahangaiko ya watoto wakimbizi na wahamiaji, hasa wale ambao wako pweke. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto wanaoishi nje ya mazingira ya familia na nchi zao na hivyo kujikuta wakiwa kama wakimbizi na wahamiaji, changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo. Wakimbizi na wahamiaji na watu wanaotafuta fursa za ajira, maisha bora zaidi lakini kuna watu wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi zao kwa matumaini ya kupata amani na usalama wa maisha.

Baba Mtakatifu anasema, waathirika wakubwa zaidi ni kundi la watoto wadogo wanaokumbana na majanga ya maisha, umaskini pamoja na matukio ambayo yanajikita katika ulimwengu wa utandawazi hasi, kiasi cha kuwatumbukiza katika biashara haramu ya binadamu, nyanyaso za kila aina pamoja na kuwapokonya haki zao msingi kama watoto kadiri ya  Mikataba ya Kimataifa kwa ajili ya watoto wadogo.

Hili ni kundi linalohitaji mazingira ya kifamilia, ili kulindwa na kuendelezwa na wazazi pamoja na walezi wake. Watoto wana haki ya kupata elimu bora kutoka ndani ya familia na shule, ili waweze kukua na kukomaa, tayari kuwajibika barabara katika ustawi na maendeleo ya nchi zao kwa siku za usoni. Inasikitisha kuona kwamba, bado elimu ya msingi ni kwa ajili ya watoto wachache duniani, lakini ikumbukwe kwamba, watoto wana haki ya kupata elimu na kucheza kama watoto. Kundi la watoto wakimbizi na wahamiaji ni wahanga wasionekana wala kuwa na sauti; ni watu ambao hawana nyaraka na hati za kusafiria wala wazazi na walezi wa kuwatetea haki zao msingi, hali inayowatumbukiza pembezoni mwa jamii, na huko wanakutana na mambo ambayo yako kinyume cha sheria na ukatili unaoteketeza matumaini ya watoto hawa wakati ambapo mtandao huu wa ukatili unaonekana kuwa na ngome thabiti.

Baba Mtakatifu anasema, ili kukabiliana na changamoto hizi zote kuna haja ya kutambua kwamba, wakimbizi na wahamiaji ni sehemu ya historia ya ukombozi hata Waisraeli wanakumbushwa katika Agano la Kale kwamba, kuna wakati hata wao walikuwa ni watumwa katika nchi ya kigeni, changamoto ya kusoma alama za nyakati, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na watu wanaolazimika kuzikimbia au kuzihama nchi zao.

Watu watambue na kuguswa na mahangaiko ya wakimbizi, ili kuwaonesha ukarimu, tayari kutambua mpango wa Mungu hata katika mazingira kama haya kwani Jumuiya ya Kikristo inawaambata watu wote kutoka katika lugha, jamaa na taifa. Kila mtu ana thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba, utu na heshima ya binadamu kamwe hauwezi kulinganishwa na vitu! Ubora wa taasisi yoyote ile unapimwa kutokana na jinsi inavyotoa kipaumbele chake kwa utu na heshima ya binadamu, lakini zaidi jinsi inavyowahudumia wanyonge ndani ya jamii na katika mazingira kama haya watoto wakimbizi na wahamiaji.

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba inajikita katika sera ambazo zitasaidia kuwalinda, kuwaingiza watoto katika maisha ya kijamii sanjari na kuivalia njuga changamoto ya wakimbizi na wahamiaji duniani, ili watoto hawa wasitumbukie mikononi mwa watu waliofilisika kiroho, kimaadili na kiutu! Hapa kuna haja ya kutofautisha kati ya biashara haramu ya binadamu na wakimbizi, ingawa wakati mwingine inakuwa ni vigumu kuweza kutenganisha mambo haya mawili. Kuna mambo kadhaa yanayochangia watoto kujikuta wakiwa ni wakimbizi au wahamiaji: hali ngumu ya maisha, matamanio ya maisha bora zaidi yanayooneshwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya kijamii, kiwango kidogo cha elimu; kutofahamu sheria, tamaduni na lugha za nchi hisani. Mambo yote haya yanagumishwa kwa kiasi kikubwa maisha ya watoto wakimbizi na wahamiaji, hali inayochangia kwa watoto hawa kujikuta wakitumbukizwa katika mazingira hatarishi, wasiposaidiwa kujinasua kwenye mtego huu watapotelea kwenye ombwe la utumwa mamboleo!

Mosi, hapa wahamiaji na wakimbizi wanapaswa kushirikiana kwa ukamilifu na Jumuiya zinazowahifadhi, kwa kuonesha pia moyo wa shukrani  kwa wadau mbali mbali wanaowahudumia na kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso pamoja na kubadilishana taarifa ili kupambana na mitandao inayowatumbukiza watoto katika majanga kama haya. Jumuiya za Kikristo ziendelee kushirikiana kwa njia ya sala, umoja na udugu.

Pili, kundi la watoto wahamiaji na wakimbizi ni tegemezi, kumbe, linahitaji sera makini zitazojikita katika ukarimu, huduma pamoja na kuwaingiza watoto hawa katika maisha ya jamii husika, lakini kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu Francisko, watoto hawa wamekumbana na pazia la chuma kiasi cha kushindwa kupokelewa na matokeo yake, wanakimbilia katika makundi yanayokwenda kinyume cha sheria au wakati mwingine kurudishwa katika nchi zao za awali bila kuwa na uhakika wa hatima ya maisha yao kwa siku za usoni.

Watoto hawa wanakabiliwa na changamoto kubwa hasa pale wanapojikuta kwamba hawana nyaraka za kusafiria au wakiwa wametumbukizwa katika makundi ya magenge ya uhalifu, hali yao inakuwa mbaya zaidi kwani wanakamatwa na kufungwa; au wanahifadhiwa kwenye vituo vya utambulisho kwa muda mrefu na huko mara nyingi wanakutana na nyanyaso mbali mbali. Serikali mbali mbali licha ya kujizatiti kulinda masilahi ya kitaifa, lakini pia hazina budi kuwa na sera makini zinazodhibiti wimbi la wakimbizi na wahamiaji watoto, kwa kulinda na kutetea utu na heshima yao sanjari na kuwasaidia kupata mahitaji yao msingi pamoja na mafao ya familia nzima.

Baba Mtakatifu anashauri kwamba, kuwepo na ushirikiano wa dhati kati ya nchi wanakota wakimbizi na wahamiaji pamoja na nchi wahisani, ili kuhakikisha kwamba, changamoto zinazosababisha wimbi kubwa la wakimbizi zinadhibitiwa kikamilifu, ili kufuta mambo yale yanayosababisha watoto wadogo kukimbia familia na nchi zao. Mikakati ya kudumu ipewe kipaumbele cha kwanza kwa kusitisha kabisa: vita, uvunjaji wa haki msingi za binadamu; rushwa, ufisadi na umaskini; mipasuko ya kijamii sanjari na athari za uchafuzi wa mazingira; kwani mambo yote haya yanasababisha mateso makubwa kwa watoto: kimaadili, kimwili na kisaikolojia kwa kuwaachia watoto hawa makovu ya kudumu.

Sababu zinazopelekea watu kukimbia au kuzihama nchi zao ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwa: kusitisha mapigano na kinzani za kijamii zinazopelekea makundi makubwa ya watu kuzikimbia nchi zao. Kuwepo na sera makini na endelevu kwa ajili ya nchi ambazo zimekuwa na migogoro na kinzani za kijamii, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu, kwa kukuza maendeleo na ustawi wa watoto pamoja na kujenga matumaini kwa wengi.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake kwa Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa mwaka 2017, anapenda kuwashukuru wadau wote wanaosimama kidete usiku na mchana kuwasaidia na kuwahudumia watoto wakimbizi na wahamiaji kuendelea kuonesha ushuhuda wa Kiinjili kwa kumpokea na kumhudumia Kristo Yesu, anayejitambulisha miongoni mwa watoto wadogo. Baba Mtakatifu anawaweka wadau wote hawa pamoja na watoto ambao ni wakimbizi na wahamiaji chini ya ulinzi na tunza ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.