2017-01-12 13:33:00

Sinodi ya Maaskofu 2018: Vipaumbele: Furaha, Mang'amuzi & Kusindikiza


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, kuna uhusiano mkubwa kati ya Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” na Sinodi ya Maaskofu kuhusu: Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito” itakayoadhimishwa kunako mwaka 2018. Maadhimisho haya yanafumbatwa katika maneno makuu matatu: furaha, mang’amuzi na usindikizaji.

 

Sektretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuchapishwa wosia huu wa kitume, iliwatumia barua Maaskofu Katoliki duniani ili kupata taarifa ya jinsi ambavyo Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu “Furaha ya upendo ndani ya familia ulivyopokelewa na familia ya Mungu katika majimbo yao, sera na mikakati itakayotumika ili kuhakikisha kwamba, Wosia huu unamwilishwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia! Kimsingi, huu ni Wosia ambao umepokelewa kwa mikono miwili na familia ya Mungu duniani kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya maisha na utume wa familia na ndoa. Ili familia ya Mungu kuweza kufahamu kwa kina na mapana ujumbe uliokuwa umefumbatwa katika Wosia huu, Maaskofu mahalia wameandaa semina, warsha na makongamano ili kuweza kuwasaidia waamini kufahamu changamoto, fursa na vikwazo vinavyobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kukuza, kudumisha na kushuhudia Injili ya familia duniani.

Kardinali Baldisseri anakiri kwamba, katika kipindi cha mwaka mzima, amepata pia fursa ya kuweza kufafanua maudhui yanayofumbatwa katika wosia huu wa kitume na jinsi ambavyo Maaskofu wanavyoendelea kuyamwilisha katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya ndoa na familia hususan katika sura ya sita ambamo Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa familia za Kikristo kupewa kipaumbele cha pekee katika sera, mikakati na shughuli za kichungaji, ili kweli wanandoa waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia.

Baba Mtakatifu katika sura ya nane, anakazia umuhimu wa kuwasindikiza, kung’amua na kuwashirikisha wanafamilia wanaoogelea katika udhaifu, magumu na changamoto za maisha ya ndoa na familia, ili kuweza kufikia utimilifu wa maisha ya ndoa mintarafu mwanga wa Injili! Hapa kila kesi inapaswa kushughulikiwa kikamilifu. Hapa wadau mbali mbali wanajumuishwa na kushirikishwa katika utume wa familia, ili kweli familia ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya haki, amani, upendo, msamaha, ushirikiano na ukarimu. Wosia wa Kitume, Furaha ya upendo ndani ya familia unaonesha mwelekeo mpya wa Kanisa katika maisha yake kwa kujikita katika dhana ya Sinodi inayowawezesha waamini kutembea kwa pamoja katika kuibua, kupanga na kutekeleza maamuzi ya maisha na utume wa Kanisa kwa mwanga wa Injili. Waamini wafanye upembuzi wa kina katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, kuibua sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa familia.

Baba Mtakatifu Francisko katika sura ya saba anakazia umuhimu wa elimu, malezi na majiundo makini kwa watoto ndani ya familia. Mambo msingi ni kuiwezesha familia kuwa ni shule ya msamaha, ukomavu wa kiutu na kimaadili, tayari kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai. Familia ni mahali pa sala na huduma; madhabahu makini ya kurithisha imani, matumaini na mapendo! Familia ni mahali pa katekesi makini ya tunu msingi za maisha ya Kikristo na Kiutu! Kumbe, familia zinaalikwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anasema, kwa watu wanaodai ufafanuzi wa kina kuhusu Wosia huu ambao kwa baadhi ya waamini wameupokea kwa shingo upande ni kukumbuka kwamba: Kanisa ni chombo cha huruma ya Mungu na daima malango yake yako wazi kwa wale wanaotubu na kumwongokea Mungu, dhamana ya kichungaji inayopaswa kutekelezwa na viongozi wa Kanisa ili kuwasaidia wanandoa kutangaza na kushuhudia utakatifu na uzuri wa maisha ya ndoa na familia ya Kikristo. Wosia huu unafumbata majibu msingi ya changamoto, matatizo na fursa zinazoweza kuibuliwa na waamini katika utume wa ndoa na familia.

Wosia wa kitume, Furaha ya upendo ndani ya familia unajikita katika utakatifu, uzuri na nguvu ya familia katika kuzima kiu ya maisha ya binadamu na umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa bila kusahau kwamba, familia pia ni kiini cha maisha ya kijamii. Kumbe, inapaswa kusaidiwa ili kweli iweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake msingi. Sinodi ya Maaskofu itakayoadhimishwa kunako mwaka 2018 ni kuwasaidia vijana kujifunza jinsi ya kufikia kilele na utimilifu wa furaha ya maisha yao katika upendo, kwani vijana wengi wanataka kujenga familia na kuwa na mwenza wa ndoa.

Vijana wanapaswa kusaidiwa ili kuweza kukamilisha ndoto hii katika maisha, kwa kujifahamu wenyewe pamoja na kuwa na vigezo vitakavyowasaidia kuwachagua wenzi wa maisha, ili kufurahia, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Mambo makuu yanayopewa kipaumbele kama sehemu ya mwendelezo wa Wosia wa Baba Mtakatifu Francisko, Furaha ya upendo ndani ya familia na Sinodi ya Maaskofu itakayoadhimishwa kunako mwaka 2018 ni: furaha, mang’amuzi na kusindikiza. Itakumbukwa kwamba, ari na mwamko miongoni mwa vijana wa kutaka kujenga na kuendeleza Injili ya familia miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni kubwa.  Haya ni kati ya mambo msingi yatakayopembuliwa na Mababa wa Sinodi kwa mwaka 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa , C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.