2017-01-11 13:12:00

Papa Francisko kutembelea Parokia ya S. M. Setteville!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ijayo tarehe 15 Januari 2017, Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani inayoongozwa na kauli mbiu”wahamiaji wadogo ni wahanga pasi na sauti” atatembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Santa Maria a Setteville, Guidonia, pembezoni mwa Jimbo kuu la Roma. Hii itakuwa pia ni fursa kwa Baba Mtakatifu kuonesha moyo wa upendo na mshikamano wa kibaba na kichungaji kwa Padre Giuseppe Berardino, mwenye umri wa miaka 47 ambaye kwa muda wa miaka miwili ni mgonjwa wa kupooza kitandani baada ya kuanguka uwanjani alikokuwa anafanya utume kwa vijana wa Parokia.

Padre Luigi Tedoldi wa Parokia ya Santa Maria a Setteville, Guidonia anasema hii ni Parokia iliyoanzishwa miaka arobaini iliyopita na Kanisa la Parokia kutabarukiwa kunako tarehe 15 Januari 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Hii ni Parokia ambamo waamini wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Parokia. Watoto na vijana wa Parokia wanayo nafasi ya kucheza na kujifunza katekesi kama sehemu ya mchakato wa malezi na makuzi yao katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu.

Vyama vya kitume vinasaidia sana kukuza na kudumisha uhai wa maisha ya Parokia kwa njia ya sala, tafakari pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wahitaji. Kuna wanandoa wanaojisadaka kwa ajili ya katekesi kwa watoto wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Sakramenti za Kanisa. Hii ni Parokia ambayo iko mstari wa mbele kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kuna fungu maalum ambalo limetengwa kwa ajili ya huduma ya upendo anasema, Padre Tedoldi, Paroko wa Parokia ya Santa Maria a Setteville, Guidonia, nje kidogo ya Jimbo kuu la Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.