2017-01-11 10:21:00

Familia ya Mungu nchini Ethiopia imarisheni amani na maendeleo!


Viongozi wakuu wa Makanisa mbali mbali nchini Ethiopia wamewataka waamini wao pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo kuendelea kujikita katika misingi ya haki, amani, upatanisho na maendeleo endelevu kwani Fumbo la kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu imekuwa ni chachu ya amani na maridhiano kati ya watu! Maadhimisho ya Noeli na Mwaka Mpya 2017 iwe ni fursa ya kuendeleza mchakato wa upatanisho; upendo na mshikamano na maskini pamoja na watu wanaoteseka zaidi, ili hatimaye kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa.

Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa ambaye pia ni Rais wa Shiriko la Mabaraza la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA amewataka waamini katika Kipindi cha Noeli na Mwaka mpya kujenga na kudumisha upendo na mshikamano. Anasema, wananchi wa Ethiopia wanatarajia kutoka kwa Serikali yao utawala wa sheria, haki na amani; mambo msingi yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo yao kama watu binafsi na kama taifa. Wakristo wametakiwa kuwa ni chachu ya maendeleo endelevu na vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu.

Kwa upande wake, Mchungaji Waq Seyoum Edosa, Rais wa Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Anglikani nchini Ethiopia amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema hata baada ya maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli ambayo nchini Ethiopia imeadhimishwa hapo tarehe 7 Januari 2017 kuendelea kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika: amani, maridhiano, utulivu, upendo na mshikamano wa dhati; tunu msingi zinazoambata na kuzaliwa kwa Kristo Yesu. Waamini pamoja na wananchi katika ujumla wao, wawe mstari mbele katika kutekeleza dhamana, wajibu na majukumu yao kama raia wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.