2017-01-10 13:46:00

Mchango wa Papa Francisko katika majadiliano ya kiekumene


Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2016 ameshiriki katika matukio makubwa ya kiekumene ambayo yanaendelea kukoleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene yaliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Haya ni majadiliano yanayojikita katika sala, huduma, damu mambo msingi yanayowaunganisha Wakristo. Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani tangu mwaka 2010 anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kiekumene kama ilivyojidhihirisha hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani huko Lund, nchini Sweden.

Uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya anasema Dr. Junge ni ushuhuda wa matumaini katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani. Hii ni chachumuhimu sana katika mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene yaliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka 50 iliyopita. Dr. Junge anakaza kusema anaheshimu sana uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika ushuhuda, ukweli na uwazi.

Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, Makanisa yamebahatika kuwa na viongozi ambao wamekuwa na mwelekeo mpana zaidi na nia ya kutaka kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anaendeleza jahazi la majadiliano haya kutoka kwa watangulizi wake kazi kubwa iliyofanywa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa mstaafu Benedikto XVI ambaye amesaidia mchakato wa kuyakwamua Makanisa kutoka katika kinzani na misigano kuelekea katika mchakato wa umoja na maridhiano.

Dr. Martin Junge anasema, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa mstari wa mbele katika kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, uhakika, usalama na maisha bora zaidi. Kwa bahati mbaya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa sasa linaonekana kuwa ni kero badala ya fursa ya ustawi, maendeleo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Papa Francisko anaendelea kujipambanua kuwa ni “Baba na mtetezi wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote”.

Hii inatokana na ukweli kwamba, athati za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Anasema, ameshuhudia mwenyewe mchango mkubwa wa Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” juu ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote wakati wa mkutano juya mazingira uliofanyika mwaka 2015 huko mjini Paris, Ufaransa, “Cop21”.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwachangamotisha viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanafanya maamuzi magumu katika sera na mikakati yao ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi zinazowaathiri maskini zaidi katika jamii. Kwa hakika, viongozi wengi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaguswa na vipaumbele na wasi wasi za Baba Mtakatifu Francisko katika ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu!

Dr. Martin Junge anasema, Papa Francisko anaendelea kutoa dira na mwelekeo mpya wa mchakato wa majadiliano na mahusiano ya kiekumene kati ya Makanisa. Uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko huko Lund, Sweden umeleta mwamko mpya wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani. Ni mwelekeo mpya kutoka katika kinzani na kuanza hija ya pamoja na katika sala na huduma kwa maskini na wanyonge duniani. Majadiliano ya kiekumene yanapaswa kusonga mbele, kamwe Makanisa hayawezi kurudi tena nyuma kwa kuambata mambo msingi yanayoyaunganisha zaidi kuliko yale mambo yanayowatenganisha kutokana na sababu za kihistoria au kitamaduni.

Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani anaendelea kufafanua kwamba, majadiliano kati ya Makanisa ya Kiorthodox na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri, yanaweza yakategemezana na kukamilishana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene! Majadiliano yanapaswa kusimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kwa walimwengu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.