2017-01-09 08:31:00

Yaliyojiri katika mahojiano na Baba Mtakatifu Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko katika kumbu kumbu ya miaka 80 tangu kuzaliwa kwake hapo tarehe 17 Desemba 2016 alifanya mahojiano ya kina na Bwana Andrea Tornieli, mwandishi wa habari wa Gazeti la “Stampa” na mhariri mkuu wa Tovuti ya “Vatican Insider”. Katika mahojiano haya, anagusia kwa namna ya pekee, hija zilizofanywa na Baba Mtakatifu Francisko sehemu mbali mbali za dunia kama kielelezo cha kuwaimarisha ndugu zake katika imani; kwa kuguswa na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji; kwa kutaka kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; dhana ya Uekumene inayojikita katika: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu amekuwa ni hujaji ambaye wakati mwingine katika hotuba zake amekuwa ni mwiba mchungu kwa watu wote wanaonyanyasa utu na heshima ya binadamu; wanaowatumbukiza wasichana na watoto katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo; mambo ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Amekemea uchumi unaowatenga baadhi ya watu katika jamii; uchumi ambayo unaendekeza utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine! Uchumi unaotafuta faida kubwa kwa gharama ya damu ya watu wasiokuwa na hatia! Huu ndio uchumi unaofumbatwa katika biashara haramu ya silaha duniani na matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu amekemea tabia ya kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema na matokeo yake ni watu kukumbatia utamaduni wa kifo, rushwa na ufisadi; uharibifu wa mazingira nyumba ya wote hali inayopelekea pamoja na mambo mengine wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ambao leo hii mbele ya uso wa Jumuiya ya Kimataifa wanaonekana kuwa ni kero kubwa! Hata hivyo, Baba Mtakatifu amekuwa ni hujaji wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa na kimataifa kama ilivyojitokeza nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, wakaanza kutambua kwamba, tofauti zao ni tunu msingi inayoweza kuwasaidia kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Katika mahojiano haya maalum, Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si mtu anayependa kusafiri sana kwani anapenda na kuthamini kuwa kati ya watu wake! Likizo kwake ni kupata muda wa kuweza kujisomea, kusali na kutafakari zaidi pale alipo pasi na kutafuta sehemu ya “kwenda kuosha macho”. Baba Mtakatifu anasema, anasafiri pale inapombidi na anapoguswa zaidi na mahangaiko ya watu wa Mungu kama alivyofanya kwa kutembelea kwa mara ya kwanza kabisa katika Kisiwa cha Lampedusa ili kujionea mwenyewe mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji ambao walikuwa wanakufa maji na utupu kwa kutafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi!

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, katika ratiba ya mwaka 2013, Khalifa wa Mtakatifu Petro alipaswa kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kule Rio de Janeiro nchini Brazil, anasema alikwenda ili kuwaimarisha vijana katika hija ya maisha yao ya kiroho kwa kupambana kikamilifu na changamoto za maisha pasi na kukata wala kukatishwa tamaa wala kuruhusu wajanja wachache waweze kuwapoka matumaini ya maisha! Safari zote hizi ni kutaka kuwatia shime waamini pamoja na kupandikiza mbegu ya imani, matumaini na mapendo kwa familia ya Mungu!

Baba Mtakatifu Francisko anakiri  kwamba, kufanya hija za kimataifa ni mchakato pevu unaohitaji maandalizi ya kina pamoja na kutambua kwamba, daima kuna shughuli za kutenda kila siku kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni hija zinazodumu kitambo kidogo lakini zinagusa maisha ya watu wengi. Hizi ni safari zinazohitaji pia maandalizi makubwa ya kisaokolojia na kimwili, lakini kwa sasa, Baba Mtakatifu anasema, anamshukuru Mungu kwani amemwezesha kufanya hija hizi na mara anaporejea mjini Vatican, moyoni mwake anabeba shuhuda, sura na mang’amuzi ya watu mbali mbali aliokutana nao; utajiri mkubwa katika maisha na utume wake!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika hija zake za kitume anapenda kusherehekea zawadi ya maisha na familia ya Mungu katika nchi husika, viongozi wa serikali pamoja na kupata muda wa kukaa peke yake na Maaskofu wenzake, ili kushirikishana, furaha ya Injili, changamoto na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza watu wanaomsubiri kwa muda mrefu hawa ni sawa na wale Wayahudi waliokuwa wanamwimbia Yesu, Hosana Juu Mbinguni, mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana!

Lakini pia anasema, kuna watu wenye nia tofauti ambao wanaweza kudiriki kusema, “Msulubishe, Mwondoe, Msulubishe” kama ilivyokuwa kwa Yesu. Duniani kuna marafiki wanakupenda na kuwa watu wasiokutakia mema pia! Huu ni ukweli wa maisha ya binadamu! Sifa na shukrani zinapaswa kumwendea Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia na wala si “Punda aliyekuwa amembeba Yesu wakati alipokuwa anaingia Yerusalemu kwa shangwe siku chache kabla ya kukabiliana na Fumbo la Msalaba!

Baba Mtakatifu anasema katika hija zake za kitume ambazo zimeacha alama ya kudumu ni pamoja na ile ya Rio de Janeiro, watoto walipokuwa wanamkimbilia ili kumsalimia na kumshika mkono! Nchini Sri Lanka, alipokutana na umati mkubwa wa waamini wa dini mbali mbali wakiwa wamekuja kumlaki na kumkaribisha nchini mwao, alama ya majadiliano ya kidini katika uhalisia wa maisha. Nchini Ufilippini alikutana na nyuso za wazazi wanaoteseka kutokana na majanga yanayozikumba familia zao; wazazi waliokuwa wanamwomba awabariki na kuaombea watoto ambao ni hazina yao ya maisha! Aliguswa na mahangaiko ya watoto walemavu waliokuwa wanatunzwa vyema na wazazi wao, kielelezo makini cha Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai, huduma na mapendo ya dhati!

Alisali na kuwakumbuka maelfu ya watu waliopoteza maisha na mali nchini Ufilippini kutokana na dhoruba kali ya Hayan! Anasema, hata yeye mwenyewe alionja ugumu wa maisha ya watu kutandikwa na mvua kubwa wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu! Huu ni ushuhuda ambao kamwe hauwezi kufutika katika akili na moyo wake wa Kibaba na kichungaji! Katika shida na mahangaiko yote haya, lakini bado familia ya Mungu nchini Ufilippini ilikuwa na furaha ya kweli iliyokuwa inabubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kusali, kuwakumbuka na kuwaombea watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watu ambao amekutana nao katika hija ya maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anasema, amefanya hija ya Uekumene wa huduma, upendo na mshikamano na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli pamoja Askofu mkuu Yerome wa Jimbo kuu la Athene, Ugiriki ili kuonesha mshikamano wa upendo kwa wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanateseka kwenye Kisiwa cha Lesbos, Ugiriki. Ametembelea pia Bunge la Umoja wa Ulaya kama taasisi.

Lakini Barani Ulaya Baba Mtakatifu anasema, ametembelea nchini Albania, Bosnia-Erzegovina, nchi ndogo ndogo ambazo ziko pembezoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, mahali ambako anasema, anataka kuzitia shime ili kuchangia katika mchakato wa ustawi na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Lengo la hija zote hizi ni kulisaidia Bara la Ulaya kugundua tena asili na mizizi ya utajiri, utambulisho wake na tunu zake msingi tayari kuzifanyia kazi. Changamoto kubwa kwa sasa Barani Ulaya ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, linalopaswa kuvaliwa njuga na nchi zote, ili kupata ufumbuzi wa kudumu!

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, walau vyombo vya ulinzi na usalama mjini Vatican vimeanza kumwelewa na kwamba, si utamaduni wala mazoea yake kupanda magari yenye ulinzi maalum usioweza kupenyeza risasi! Anawashukuru na kuwapongeza kwa kulitambua hilo, lakini pia anatambua kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro ni “Baba” na “Mchungaji mkuu”, kumbe, hakuna sababu msingi za kuweka kuta za utengano na badala yake, ni kujenga madaraja ya watu kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Daima anasema, atasafiri na kwenda mahali ambapo atakuwa na uhuru wa kukutana na kuzungumza na watu wa kawaida! Kuna haja ya kuamini na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu!

Baba Mtakatifu anasema, katika umri wake anadhani kwamba, hakuna kitu ambacho kinaweza kumwogofya, lakini anatambua pia umuhimu wa kuwalinda na kuwategemeza wale wanaosafiri pamoja naye. Ni kweli anao wasi wasi mkubwa kwa watu wanaohudhuria maadhimisho na mikutano yake, kwani duniani kuna mengi, lakini daima Mwenyezi Mungu yuko kwa ajili ya usalama na maisha ya watu wake anasema Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Bwana Andrea Tornieli, mahojiano ambayo yamechapishwa kwenye kitabu na sasa kinapatikana kwenye maduka ya vitabu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.