2017-01-08 14:47:00

Papa Francisko anakutana na Mabalozi na Wanadiplomasia mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 9 Januari 2017 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican wapatao 182. Katika masuala ya kidiplomasia na ushirikiano wa kimataifa, Vatican inapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa haki, amani, ustawi na mafao ya wengi kwa kuheshimu na kuzingatia haki msingi za binadamu! Inataka kudumisha amani kwa njia ya majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro ni sauti ya kinabii inayosimama kwa ajili ya kuwatetea wanyonge na maskini duniani! Hana nguvu ya kisiasa, lakini anayo nguvu ya kimaadili inayomfanya aweze kusikilizwa na wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa katika kukuza, kudumisha na kuenzi utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu!

Professa Agostino Giovagnoli kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki, Jimbo kuu la Milano, Italia anasema, Viongozi wakuu wa Kanisa katika karne ya ishirini, wamesimama kidete na kujielekeza zaidi katika kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya mataifa. Injili ya amani duniani inawagusa watu wote pasi na ubaguzi wa aina yoyote ile hali ambayo inamwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kuweza kusikilizwa kwa makini na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake!

Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya viongozi wachache kwenye Jumuiya wanaodiriki kusema kwamba, leo hii dunia iko kwenye Vita ya tatu ya Dunia iliyotawanyika sehemu mbali mbali za dunia, ndiyo maana kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Umefika wakati wa kuondokana na kirusi cha uadui wa kimataifa, ili kujenga utamaduni wa haki, amani na maridhiano. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuachana na mazoea ya vita na kuvifanya kuwa ni jambo la kawaida katika maisha ya mwanadamu anasikitika kusema, Professa Agostino Giovagnoli.

Baba Mtakatifu amekuwa ni sauti ya watu walioathirika kwa vita sehemu mbali mbali za dunia! Ni mtetezi wa haki msingi za binadamu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaoteseka na kufariki dunia katika utupu na baridi, huku wakitafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Ni Baba wa maskini na faraja kwa watu wanaoteseka! Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi ambaye anaendelea kusoma alama za nyakati, ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika Ulimwengu mamboleo kwa jicho la imani, matumaini na mapendo thabiti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.