2017-01-07 15:28:00

Wasichana zaidi 800 wakeketwa Kaskazini mwa Tanzania


Tarehe 4 Januari 2016  tulitoa habari kuhusu “Kanisa la Ethiopia kupinga ukeketetaji wa wasichana” wakati wa Semina iliyoandaliwa na Baraza la maaskofu nchini humo na wito wa Baraza la maaskofu hao kwa wanajamii wa Ethiopia ulikuwa ni kubainisha njia inayoweza kutumika ambayo ni “elimu”, hasa katika mashule ya  kikatoliki kuanzia utekelezaji wa kupambana na ukeketaji huo kwa wasichana, kwa kuweka mpango huo ndani ya mtahala wa shule, wakiwahusisha moja kwa moja wanafunzi na wazazi wao.Lengo la kufanya hivyo ni kuongeza utambuzi na ufasaha wa tatizo hilo katika jamii.

Lakini kwa mapana  bado hali ya ukeketaji kwa upande wa Afrika inazidi kupamba moto kwani taarifa nyingine tena tunazipata kutoka Misri, Kenya na Tanzania ya kwamba wasichana zaidi ya 800 walikeketwa kaskazini mwa Tanzania mwezi uliopita, taarifa kutoka kwa  mkuu wa wilaya ya Tarime Glorious Luogama alisema, “vitendo hivyo vinafanyika ingawa polisi wamekuwa wakikabiliana na utamaduni huo”.

 

Mkuu wa Wilaya hiyo akiwaeleza wandishi wa habari akisema” Wanawake 12 wanaotuhumiwa kuhusika katika kuwakeketa wasichana hao wamekamatwa na maafisa wa polisi, na kuendelea ;"Operesheni ya polisi bado inaendelea. Hatutatulia hadi wote waliohusika wakamatwe na kushtakiwa.
Eneo la Tarime, wasichana hukeketwa wakiwa na umri kati ya miaka 12 na 17 na inakadiriwa kwamba nchini Tanzania, wasichana na wanawake 7.9 milioni wamekeketwa. Lakini kwa upande wa nchi ya Misri wamepitisha sheria kali dhidi ya Ukeketaji, wakati huo nchini kenya wasichana pia wa shule walikimbia ukeketeji huo.


Aidha Novemba, kabla ya kuanza kwa msimu wa ukeketaji Tarime, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Tarime, Thomas Mapuli alikuwa ametangaza kwamba polisi wamejiandaa kuwakamata mahusika  wote ambao wangejaribu kukeketa watoto wa kike; "Tumejipanga vizuri na hatutakuwa na huruma kwa atakayekutwa anatenda kosa la ukeketaji," alisema Bw Mapuli.


Wasichana takriban 140 milioni wamekeketwa maeneo ya Afrika, Mashariki ya Kati na Bara Asia.Jamii zinazotekeleza utamaduni huu huutazama kama njia ya kuwatakasa wasichana na kuwaandaa kwa maisha ya ndoa na kufikiri kwamba wasipowafanyia hivyo hawastahili kuolewa. Wengine wanatambua athari  nyingi , na wengine hawatambui , na kuendelea na fikraza utamaduni potofu , unaosababisha matatizo mengi ya kiafya, kwasababu wengi hufariki wakikeketwa na baadaye wengi hukabiliwa na matatizo sana wanapojifungua.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii Bi. Sihaba Nkinga kiwango cha ukeketaji wa wasichana na wanawake Tanzania ni asilimia 32.

 

Sr Angela Rwezaula

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.