2017-01-07 09:53:00

Papa Francisko: Yesu ni zawadi ya huruma ya Baba wa milele!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, Ijumaa, tarehe 6 Januari 2017 amesema kwamba, Mamajusi kutoka Mashariki walipokwenda Bethlehemu walimwona Mtoto Yesu wakamwangukia na kumsujudia na hatimaye, wakafungua hazina walizokuwa nazo kibindoni! Zawadi hizi ni uvumba unaonesha Umungu wa Kristo; manemane ubinadamu wa Kristo na dhahabu ni kielelezo cha ufalme wa Kristo unaofumbatwa katika: ukweli, haki, uzima; utakatifu na neema; haki, upendo na amani!

Lakini, Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Yesu Kristo Mwana wa Mungu ndiyo zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa huruma ya Baba wa milele anayewasubiria waja wake, ili kuwapokea na kuwakumbatia kama alivyofanya Baba mwenye huruma, tayari kuwasamehe na kuwapatia neema ya kuanza tena upya safari ya maisha yao ya kiroho!

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, kamwe hawatendi binadamu kutokana na dhambi, makosa au mapungufu yao ya kibinadamu! Ni Mungu anayetenda haki ambayo ni huruma isiyokuwa na mipaka kwa waja wake. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na zawadi zilizotolewa na Mamajusi kwa Mtoto Yesu, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, alitoa zawadi ya Kitabu cha mfukoni kinachoonesha mashuhuda wa huruma ya Mungu kadiri ya Mwanga wa Injili.

Lengo ni kuwawezesha waamini kuendelea kufanya kumbu kumbu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kumwilisha huruma hii katika uhalisia wa maisha ya watu! Maskini, wakimbizi na wahamiaji; watawa na watu wa kujitolea waligawa vitabu hivi kwa maelfu ya waamini, mahujaji na watalii waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuhudhuria Siku kuu ya Tokeo la Bwana!

Baba Mtakatifu amewatakia wote heri na baraka kwa Mwaka 2017, kweli uwe ni mwaka haki na amani; utulivu na msamaha, lakini zaidi, uwe ni mwaka unaoendelea kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha ya watu! Kitengo cha Sadaka ya kitume katika taarifa yake kinasema, hii ni zawadi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Ni kitabu chenye tafakari na sala kuhusu huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani. Kinaelezea watu mashuhuri katika Injili, walioguswa na huruma ya Mungu, wakabadilika na kuwa ni watu wema zaidi na mfano bora wa kuigwa! Hawa ni yule Mwanamke mzinzi aliyeokolea na Kristo Yesu dhidi ya adhabu ya kifo kwa kupigwa mawe hadi kufa! Zakayo mtoza ushuru, aliyetubu na kumwongokea Mungu akawa ni mfano bora wa watoza kodi! Ni kitabu kinachomzungumzia pia Mathayo mtoza ushuru aliyeacha yote na kuanza kumfuasa Kristo Yesu, leo hii ni Mwinjili anayethubutu kusimulia wema, huruma na upendo wa Mungu ulivyomletea mageuzi makubwa katika maisha yake! Ni kitabu kinachomwelezea Mwanamke Msamaria aliyenyweshwa maji ya uzima na Kristo chemchemi ya ukweli, wema na utakatifu wote.

Bila shaka wengi wanamkumbuka yule mwizi aliyekuwa ametundikwa Msalabani, akaona Uso wa huruma ya Mungu na kuomba upendeleo kutoka kwa Kristo atakapokuwa ameingia kwenye Ufalme wake wa mbinguni! Mtakatifu Petro mtume ni kati ya watu walioonja huruma na upendo wa Kristo katika maisha yake! Wote hawa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.