2017-01-07 11:45:00

Dr. Mariella Enock kuendelea kuongoza Bambino Gesù hadi mwaka 2020


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa mamlaka aliyokabidhiwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko amemthibitisha Dr. Mariella Enoc, kuendelea kuwa Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kwa kipindi kingine cha miaka minne, yaani kuanzia mwaka 2017- 2020. Kardinali Parolin amependa kutumia nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Dr. Enoc kwa niaba ya Vatican kutokana na kazi kubwa anayoendelea kufanya Hospitalini hapo tangu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kunako mwaka 2015.

Ni kiongozi ambaye ameendelea kutekeleza wajibu na dhamana yake kwa usimamizi, weledi, uadilifu na uwajibikaji sanjari na sadaka pamoja na majitoleo makubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Hospitali ya Bambino Gesù iliyoko mjini Roma. Amekuwa kweli ni chachu ya mageuzi kwa kuhakikisha kwamba, Hospitali ya Bambino Gesù inakuwa ni kielelezo cha huduma ya upendo kwa watoto wagonjwa pamoja na wazazi inayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Itakumbukwa kwamba, Hospitali ya Bambino Gesù ilianzishwa kunako mwaka 1869 na kunako mwake 1924 ikakabidhiwa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tangu wakati huo, ikawa chini ya usimamizi wa Vatican. Hospitali hii ina uwezo wa kulaza watoto 607 katika matawi yake manne yaliyoko mkoani Lazio. Hii ni hospitali kubwa Barani Ulaya kutoa huduma ya tafiti na tiba kwa watoto wadogo. Ni hospitali ya rufaa kwa watoto wagonjwa kutoka ndani na nje ya Italia. Itakumbukwa kwamba, Hospitali ya Bambino Gesù kwa miaka kadhaa imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Tanzania kwa ajili ya huduma kwa watoto waliokuwa na matatizo ya moyo! Watoto kadhaa waliweza kufanyiwa huduma ya upasuaji na wengi wao wanaendeleo vyema na maisha nchini Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.