2017-01-07 10:09:00

Askofu mkuu Ruwaichi: Matendo ya huruma: kiroho na kimwili!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni nafasi ya kulitafakari tena Fumbo la huruma ya Mungu ambalo ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani kwa kutambua kwamba, huruma ni daraja linaloaunganisha Mungu na binadamu na hivyo kumfungulia mlango wa matumaini ya kupendwa, licha ya dhambi na udhaifu wa kibinadamu!

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema,  huruma ni msingi thabiti wa uhai, maisha na utume wa Kanisa ndiyo maana Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni nafasi ya kuhamasisha waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kiroho na kimwili! Anasema, matendo ya huruma kiroho ambayo kimsingi ni ushauri kwa wenye shaka, kuwafundisha wajinga, kuwaonya wakosefu; kuwafariji wenye huzuni; kusamehe makosa; kuvumilia wasumbufu pamoja na kuwaombea walio hai na wafu ni fursa ya kuwa karibu na wale wanaojisikia kuwa mbali na Kanisa au kusukumizwa pembezoni mwa maisha na utume wa Kanisa!

Askofu mkuu Ruwaichi anaendelea kufafanua kwamba, kuna sababu mbali mbali ambazo zinaweza kumpelekea mwamini kujikuta katika hali na mazingira haya! Hizi ni sababu binafsi au hata wakati  mwingine, Kanisa halikufanikiwa kuwa karibu na watu hawa katika shida na mahangaiko yao ya ndani! Kumbe, kuna haja kwa Kanisa mahalia kuwa na sera na mikakati ya shughuli za kichungaji itakayoliwezesha Kanisa kuwa karibu na watu hawa ili kweli waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini, licha ya changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha!

Askofu mkuu Ruwaichi anasema, kauli mbiu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ilikuwa ni “Wenye huruma kama Baba” ili kuwashirikisha wengine furaha, amani, matumaini na utulivu wa ndani. Matendo ya huruma kimwili ni: kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu; kuwavika walio uchi; kuwakaribisha wasiokuwa na makazi; kuwatembelea wagonjwa; kuwatembelea wafungwa na kuwazika wafu! Matendo ya huruma kimwili ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa tangu mwanzo.

Hii ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma ya elimu na afya hasa vijijini ambako wengi hawapendi kwenda kwani hakuna “mshiko wa kutosha”. Anakumbusha kwamba, wafungwa ni watoto wa Mungu licha ya kwamba wamenyang’anywa uhuru wao, lakini bado wana haki ya kupata huduma ya kiroho, ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu, ili wanapohitimisha adhabu yao, waweze kuwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani. Kanisa kwa njia ya taasisi zake limekuwa mstari wa mbele kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa Ukimwi; watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Limejenga linaendesha nyumba za wazee na wagonjwa. Askofu mkuu Ruwaichi anahitimisha mahojiano haya kwa kusema,  huu ndio uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa katika kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.