2017-01-06 13:50:00

Salam za heri, udugu na mshikamano kwa Makanisa ya Mashariki


Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana ni ushuhuda wa mwanga angavu wa Yesu unaowangazia watu wote wa mataifa! Huu ni mwanga unaopania kumwangazia kila mtu katika hija ya maisha yake kama ilivyokuwa ile nyota iliwaongoza Mamajusi kutoka Mashariki hadi kwenda mjini Bethlehemu alikozaliwa Mtoto Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiaminisha katika mwanga wa nyota ya Kristo Yesu!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 6 Januari 2017 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hata katika maisha kuna mianga ambayo inang’ara na kuwaongoza watu! Kuna mwanga unaokuja na kuondoka, kama mambo yanayotosheleza hamu ya maisha hata kama ni mazuri kiasi gani, kwani yanadumu kwa kitambo kidogo na kamwe hayawezi kuacha amani ya kudumu ambayo binadamu anaitamani katika maisha!

Kuna mwanga mkubwa wenye kuangaza watu kuwa na tamaa ya fedha, mali na mafanikio ya chapuchapu katika maisha! Lakini, ni mwanga usiokuwa endelevu kwani mwanga huu unawawezesha watu kuwa ndoto ya utukufu inayowatumbukiza katika giza totoro. Mamajusi wanawaalika waamini kufuata nyota angavu isiyofifia kamwe kwani hii ni nyota kutoka mbinguni inayong’aa moyoni mwa mtu! Mwanga huu angavu ni Kristo Yesu unaowaongoza watu kwenye furaha ya pekee!

Nabii Isaya anasema, Ondoka! Uangaze! Wale wanaofuata nyota angavu ya Kristo watakuwa na furaha ya kweli kama ilivyojitokeza kwa Mamajusi, kwani mahali palipo na Mungu hapo kuna furaha ya kweli! Huu ni mwanga unaofukuzia mbali giza la maisha, mwaliko ni kutokuwa na woga wa kufuata mwanga na kujifunua mbele ya Kristo! Baba Mtakatifu anawahimiza wale wote waliopoteza nguvu ya kuutafuta mwanga huu pamoja na kuelemewa na giza la maisha, ili kweli mwanga wa Kristo uwasaiide kulishinda giza hilo daima wakiwa wanatembea kama walivyofanya Mamajusi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni changamoto ya kutoka katika ubinafsi na hali ya kujitafuta mwenyewe; kwa kuthubutu kushiriki kikamilifu katika maisha badala ya kubweteka na matukio yanayomzunguka mtu! Ikumbukwe kwamba, maisha ya Kikristo ni safari endelevu inayofumbatwa katika matumaini na udadisi wa kuendelea kutafuta hata pale ambapo nyota inaonekana kufifia na hatimaye kupotea kabisa! Hivi ni vikwazo ambavyo viliwazuia Makuhani  kuuona mwanga. Haitoshi kufahamu kwamba Mwenyezi Mungu amezaliwa kama hakuna mtu anayethubutu kuadhimisha Fumbo la kuzaliwa kwa Kristo moyoni mwake!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mamajusi walipomwona Mtoto wakaanguka na kumsujudia kiasi cha kujenga mahusiano ya upendo wa dhati na Yesu na hatimaye, kumpatia zawadi ya: Uvumba, Manemane na Dhahabu; zawadi kubwa walizokuwa nazo kibindoni! Waamini wanahamasishwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu ili kuupata mwanga wake. Kama ilivyokuwa kwa Mamajusi, waamini nao wanapaswa kuanza safari, kwa kujivika mwanga na kufuata nyota ya Kristo Yesu na hatimaye, kumwabudu kweli kweli!

Mwishoni mwa Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu alikumbushia kwamba, Jumamosi, tarehe 7 Januari 2017, Makanisa ya Mashariki yanayofuata Kalenda Juliana, wanaadhimisha Siku kuu ya Noeli. Baba Mtakatifu anasema, katika moyo wa furaha ya udugu na upendo anapenda kuwatakia waamini hao heri na baraka ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, awajaze mwanga na amani!

Siku kuu ya Tokeo la Bwana ni Siku kuu ya Shirika la Utoto Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuendelea kujizatiti katika kutangaza na kushuhudia Injili kwa kuwasaidia watoto wenzao wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Amewashukuru na kuwapongeza waandamanaji waliotembea hadi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama alama ya mshikamano na watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi! Hiki ni kielelezo cha mshikamano na udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.